Rais Dkt.Samia:Serikali itarejesha huduma zote za msingi Katesh

MANYARA-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wakazi wa mji mdogo wa Katesh walioathirika na mafuriko makubwa kuwa Serikali itarejesha huduma zote za msingi za kijamii.

Rais Dkt.Samia amesisitiza kuwa serikali itaendelea kufanya tathmini ya uharibifu wa mali huku akiiagiza Wizara ya Nishati kuangalia uwezekano wa upatikanaji wa umeme wa dharura baada ya miundombinu kuharibika na maafa haya ili shughuli za uopoaji zifanyike usiku na mchana.

Rais Samia ametoa kauli hiyo Desemba 7, 2023 wakati akizungumza na wananchi na waathirika mara baada ya kutembelea maeneo yaliyoathirika na mafuriko hayo na kushuhudia hali halisi ya uharibifu wa maafa.

Aidha, Rais Dkt.Samia ameongeza kuwa mbali na michango mbalimbali iliyotolewa ndani ya nchi, lakini pia kumetolewa takribani shilingi bilioni 2.5 kutoka kwa wahisani walioshiriki kwenye mkutano wa COP 28, Dubai.

Miongoni mwa maeneo aliyotembelea Rais Samia ni Hospitali ya Tumaini wilayani humo kwa ajili ya kuwajulia hali na kuwafariji majeruhi na pia Shule ya Sekondari ya Katesh ambapo ndipo makazi ya muda yalipowekwa ili kuwastiri waathirika hao.

Vile vile, Rais Samia ametaka tahadhari zote za msingi zichukuliwe ili kusitokee janga jingine la mlipuko wa magonjwa hivyo kuheshimu kanuni za usafi kwani amesema majanga wakati mwingine huzua maradhi kama kipindupindu.

Hivyo Rais Samia ameielekeza Wizara ya Maji kuhakikisha huduma za maji safi na salama zinaendelea kupatikana muda wote huu hususan maeneo yaliowekwa makambi ya kustiri waathirika wa janga hilo.

Mafuriko mazito yaliotokea yamesababisha vifo vya Watanzania 76 hadi sasa, huku kaya 1,150 zikiwa zimeathirika na watu 5,600.

Pia, kumekuwa na majeruhi zaidi ya 117 pamoja na uharibifu wa miundombinu ya barabara, maji na umeme katika mji huo mdogo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news