NA FRESHA KINASA.
WASICHANA sita kati ya 10 wanaoishi Mkoa wa Mara kutoka katika familia zisizojiweza kiuchumi waliokuwa wakifadhiliwa na Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Rhobi Samwelly kusomea fani ya Hoteli na Ukarimu kwa kipindi cha miaka miwili ngazi ya cheti katika Chuo cha Help to Self Help kilichopo jijini Arusha wamefanikiwa kuhitimu.
Kufuatia hatua hiyo, wememshukuru Rhobi Samwelly kwa kuwasaidia huku wakiomba wadau mbalimbali wenye uwezo kuendelea kuwashika mkono watoto wa kike kielimu, kifani na kuwapa mitaji waweze kujitegemea kiuchumi.
Waliohitimu mafunzo hayo ni Zena Maingu Maharage(22) Mkazi wa Kijiji Cha Bulinga kata ya Bulinga Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Sheila Juma Aduwe (23) Mkazi wa Kijiji Cha Nyamasanda Wilaya ya Rorya.
Pia Rosemary Dominick (19) Mkazi wa Kata ya Iringo Manispaa ya Musoma, Nyangi Chacha Mwita Mkazi wa Kijiji cha Bisarwi kata ya Manga Wilaya ya Tarime, Butoto Amos Mwita Mkazi wa Mtaa wa Misitu Wilaya ya Serengeti na Mariam James Kiraka Mkazi wa Nyankanga Wilaya ya Butiama. Huku wengine wanne walishindwa kutokana na sababu zao binafsi.
Wakizungumza na waandishi wa habari Decemba 18, 2023 Kuelezea furaha yao Wamesema kuwa, kwa sasa wanaona nuru mbele yao kwani pasipo ufadhili wa Mkurugenzi huyo matumaini yao ya kusomea fani hiyo yasingetimia kutokana na uwezo wa familia zao kuwa mdogo kiuchumi.
Zena Maingu Maharage (22) Mkazi wa Kijiji Cha Bulinga Kata ya Bulinga Wilaya ya Musoma amesema kuwa anafuraha kubwa na faraja kuhitimu fani hiyo kwani anaamini kwamba ataweza kuajili ama kujiajiri akapata fursa hiyo na hivyo kuwa msaada kwa familia na Jamii.
"Nilihitimu kidato cha nne mwaka 2019 na kupata daraja la nne alama 27, lakini kutokana na hali ngumu ya kiuchumi katika familia yetu Wazazi walishindwa kuniendeleza. Lakini mwaka Jana mwezi wa sita nilipata fursa ya kuitwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa (UWT) Wilaya ya Musoma Vijijini ambaye alikuwa anatambua hali ya familia yetu, aliniunganisha na Rhobi Samwelly nikakutana naye na kumweleza shauku yangu nachotaka kusomea," amesema na kuongeza kuwa.
"Aliweza kuniweka katika programu ya ufadhili miongoni mwa wasichana 12 tuliobahatika nikaenda Jijini Arusha nikiwa miongoni mwa wasichana hao, nimeweza kusomea fani ya Usimamizi wa Hotel na pia kwa muda wote nilikuwa nikilipiwa ada, pesa ya matumizi, nauli na pia nimeweza kusoma Lugha ya kifaransa, Kiingereza na ninauwezo, amesema Zena.
"Pasipo ufadhili huo nisingeweza kufika hapa nilipo na huenda ningeolewa katika umri mdogo na ndoto yangu kupoteza kabisa. Huyu mama (Rhobi Samwelly) amekuwa msaada mkubwa sana kwangu na kwa wenzangu ambao ametusaidia Mungu azidi kumbariki sana." amesema Zena Maingu.
Rosemary Dominick Mkazi wa Kata ya Iringo Manispaa ya Musoma amesema kuwa "nilihitimu Baruti Sekondari 2021 nikawa nipo nyumbani tu kwani nilipata daraja la nne alama 28, Nilipopata fursa hii ya kufadhiliwa na Rhobi Samwelly nikaenda Jijini Arusha kusomea fani ya Upishi kwa Sasa ninauwezo wa kupika vyakula mbalimbali naamini huu ni mtaji ambao nimeupata kupitia ufadhili wake, Hali ya Wazazi wangu haikuwa nzuri kiuchumi bila kishikwa mkono na huyu mama." amesema na kuongeza kuwa.
"Nimepata elimu ambayo naamini kabisa itanisaidia maishani mwangu, nitajihudumia Mimi Mwenyewe na pia Wazazi wangu na ndugu zangu nao wataneemeka. Namshukuru Mkurugenzi Rhobi Samwelly kwa moyo wake wa upendo na kujali Watoto wa kike hasa kuwaendeleza, wapo wengi wenye fedha nao wananafasi kutumia kipato chao kupeleka tabasamu kwa ambao hawana uwezo wa kusoma hasa fani ambazo huhitaji fedha nyingi." amesema Rosemary Dominick.
Nyangi Chacha Mwita (19) Mkazi wa Kijiji Cha Bisarwi Wilaya ya Tarime ameomba Wadau mbalimbali kuendelea kuwashika mkono Watoto wa kike kwa kuwasaidia kiuchumi hasa waliosoma fani mbalimbali kusudi waweze kuanzisha biashara na kujiajiri, huku akimpongeza Rhobi Samwelly kwa uthubutu wake mkubwa wa kuwasaidia wasichana ikiwemo kupambana na ukatili kwa ajili ya Ustawi wa maisha yao.
Veronica Mageta ni Mzazi wa Zena Maingu ambapo amesema anamshukuru Rhobi Samwelly kwa kuwasaidia wasichana hao kitendo ambacho amesema kinawapa nuru ukurasa mpya katika harakati za kujitegemea na kujikwamua kiuchumi.
Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania,Rhobi Samwelly amesema programu ya kuwasaidia wasichana hao aliifanya kupitia Wenyeviti wa UWT Wilaya ambapo aliwaambia wachague kila mmoja msichana anayetoka familia isiyojiweza na ndipo alipopewa majina yao na yeye kuchukua jukumu hilo la kuwasomesha.
Rhobi amesema, anafarijika kuona wasichana hao sita wametimiza malengo yao na pia amesema programu hiyo ya kuwasaidia iitwayo 'Erasto Widows Empowerment Programme' ni endelevu kuwasaidia wasichana na wanawake, huku akiomba Wazazi na walezi nchini kuwaendeleza wasichana katika vyuo mbalimbali ili wapate ujuzi kuweza kuwasaidia kuajiriwa na kujiajiri.
"Wasichana hawa wanajua kupika vyakula vya kiafrika na vya mataifa mbalimbali, wapo wahitimu wengi ambao ni mabinti wako majumbani Wazazi wanasubilia waolewe hii si sahihi. Niombe Wazazi wawaendeleze katika vyuo mbalimbali wanapoajiliwa ama kujiajili hata vitendo vya ukatili wa Kijinsia vinapungua kwani wanakuwa na kipato. tuwape uzito sawa Watoto wa kike kielimu sawa na watoto wa kiume kuimarisha Usawa katika Jamii yetu," amesema Rhobi Samwelly.
Tags
Habari
HGWT
Hope for Girls and Women in Tanzania
Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT)
Mara Region