SHANGHAI-Muungano wa BRICS unatarajiwa kuunda sarafu mpya ili kutoa changamoto kwa dola ya Marekani katika biashara ya Kimataifa.
BRICS inalenga kung'oa ukuu wa dola ya Marekani kwa kubadilisha na sarafu yao ambayo itatolewa hivi karibuni.
Kupitia mkutano ujao wa kilele wa BRICS ambao utafanyika Oktoba,2024 katika eneo la Kazan nchini Urusi, hoja ya sarafu mpya ni miongoni mwa ajenda kuu.
Wakati nchi tano wanachama huhudhuria mkutano huo kila mwaka, mataifa 10 yatakuwa sehemu ya umoja huo mwaka ujao.
Muungano huo uliingiza nchi nyingine tano za Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE),Misri, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Ethiopia.
Mkutano wa 16 wa kilele wa BRICS mnamo 2024 unaweza kuazimia rasmi kuhusu kuunda sarafu mpya ambayo inatarajiwa kuchukua nafasi ya dola ya Marekani.
Kubadilika kwa dhana hiyo kutazifanya Marekani na nchi za Magharibi kupigana kudumisha ukuu wao wa kimataifa huku BRICS ikizishawishi nchi nyingine zinazoendelea kutumia sarafu yao na si dola.
Mwanauchumi wa Urusi, Sergey Glazyev alithibitisha kuwa BRICS tayari inafanya kazi katika kuunda sarafu mpya.
Alidokeza kuwa itakuwa ni hoja kuu ya mjadala katika mkutano ujao wa BRICS mwaka 2024 nchini Urusi.
Ikiwa nchi 10 wanachama zitakubali kuzindua sarafu mpya ya BRICS, dola ya Marekani itakabiliwa na mshindani mkubwa.
Jumuiya hiyo inarekebisha sarafu yao ambayo bado haijatolewa na kujenga miundombinu sahihi ya malipo kabla ya kuzinduliwa katika masoko ya kimataifa.
Hata hivyo, tarehe ya kutolewa kwa sarafu ya BRICS bado haijajulikana. Dola ya Marekani hivi karibuni italazimika kukabiliana na ushindani na kundi ambalo linalenga kuiangusha.
Miaka michache ijayo itaamua hatima na matarajio ya dola ya Marekani katika soko la Kimataifa. (News Agencies)