ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake madarakani, Serikali imechukua hatua mbalimbali kuimarisha sekta ya elimu kwa kufanya jitihada kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha utoaji wa elimu bora na kuchochea maendeleo katika nyanja zote.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa vyuo vya Serikali, binafsi pamoja na taasisi nyingine za elimu Zanzibar zinafanya kazi nzuri kwa kuandaa wataalamu kushika nyadhifa mbalimbali za utumishi Serikalini na taasisi binafsi.
Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo katika Mahafali ya 21 ya Zanzibar University (ZU), kampasi ya Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja leo Desemba 5,2023.
Kwa upande mwingine Rais Dkt.Mwinyi amesema elimu ni agenda muhimu katika ilani ya uchaguzi ya CCM 2020-2025 na imesisitizwa ili kuongeza kasi ya maendeleo kwa taifa na wananchi.