DODOMA-Msemaji Mkuu wa serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari -Maelezo Bw.Mobhare Matinyi amesema serikali itaendelea kuheshimu haki za binadamu katika zoezi la kuhamisha watu wanaojiandikisha kuhama kwa hiyari kutoka eneo la hifadhi ya Ngorongoro kwenda maeneo mengine nchini.
Matinyi ametoa kauli hiyo akizungumza na Wanahabari jijini Dodoma kufuatia msimamo wa baadhi ya wabunge wa Bunge la Ulaya uliotolewa wiki hii kuhusu zoezi la kuhamisha wananchi wa Ngorongoro kwa hiari ambapo Matinyi amesisitiza msimamo wa Serikali kuwa inawahamisha wananchi wanaojiandikisha wenyewe kuhama katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro na kwamba hakuna ukiukwaji wowote wa haki za binadamu unaofanyika katika utekelezaji wa zoezi hilo.
Ameeleza kuwa serikali ya Tanzania inatekeleza mpango huo ikiamini katika kutimiza malengo ya dunia ya milenia ya kuhakikisha usalama wa watu wake, huduma bora za kijamii ikiwemo elimu, afya na maji huku akisema kwamba serikali itaendelea kuhamasisha wananchi hao kukubali kuhama kwa hiyari.
Bw.Matinyi ameeleza kuwa mtu yoyote au kundi linalotaka kutembelea eneo la hifadhi ya Ngorongoro wanakaribishwa na wanachotakiwa kufanya ni kufuata taratibu ili waweze kuruhusiwa kwa kuwa Serikali haina sababu ya kumzuia mtu yeyote kufika eneo hilo.
Akizungumza hoja ya kuwepo kwa watu asili nchini Tanzania Bw.Matinyi amesema kuwa watanzania wote wanatambulika kwa utaifa wao ambapo kuna Zaidi ya makabila 120 na hivyo suala la kuhamisha watu katika hifadhi hiyo lisitazamwae katika kuhamisha kabila fulani bali wananchi wote waliopo huko wanahamisishwa kuhama kadri wanavyojiandikisha.