Serikali yachukua hatua za awali maafa Katesh

MANYARA-Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu imechukua hatua za haraka kwa wahanga wa maafa yaliyosababishwa na maporomoko ya tope yaliyotokea Desemba 3, 2023 ambapo yalitoka mlima Hanang' uliopo Mkoa wa Manyara na kusababisha vifo vya watu, majeruhi na uharibifu mkubwa wa miundombinu mbalimbali yakiwemo mashamba na makazi ya wananchi wa eneo hilo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama, Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi pamoja na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wamefika katika Kijiji cha Gendabi katika Kata ya Gendabi Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara eneo yalipotokea maporomoko ya tope leo Desemba 4,2023.

Viongozi hao wameongozwa na Mkuu wa Mkoa Manyara, Mhe. Queen Sendiga kufika katika Kijiji cha Gendabi ambalo ni eneo liliothirika Maporomoko ya tope kutoka Mlima wa Hanang yaliyotokea usiku wa kuamkia tarehe 03 Disemba 2023.

Akiwa eneo la tukio hilo, Waziri Mhagama, amewaomba wananchi hao kupokea pole ambazo zinatoka kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ambaye aliagiza lazima KUfika eneo la tukio na kuona nini kifanyike kwa dharura kuhusu uokoaji pamoja na makazi kwa waathirika hao.

“Mambo haya yakitokea kuna mambo ya haraka yanatakiwa yafanyike kwa dharura hivyo tumekuja na kushauriana namna ya kujipanga kwa pamoja ili kufanikisha jambo hilo kwa uharaka,"ameongeza Mhagama.

Ameongeza kuwa, maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwanza kuona namna gani wanaweza kuendelea kuokoa watu na kazi hiyo wanaendelea nayo vikosi vya uokoaji, pia kuangalia namna gani ya kuweza kuwasitiri wenzetu waliotangulia mbele ya haki.

Aidha, Waziri Mhagama amesema kuwa Serikali imeshaleta wataalamu wa Miamba watatoa taarifa ya nini kilichotokea na nini kifanyike katika mlima wa Hanang'.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema kazi ya kufungua miundombinu ya barabara inaendelea ili kurahisia kazi za uokoaji na kufikisha huduma muhimu za kijamii katika meneo yaliyoathirika.

Amesema Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) tayari wamefungua Barabara ya Singida-Babati ambayo awali ilikuwa haipitiki kutokana na kujaa tope na magogo ya miti kutoka milimani.

Naye Mbunge wa Hanang’, Mhe. Samwel Hayuma aliipongeza serikali kwa namna inavyoendelea kuchukua hatua za haraka za kuokoa na kusaidia wahanga wa maafa hayo, huku akiwasisitiza wananchi hao kuendelea kuchukua tahadhari kwa maeneo yote yaliyoathirika na tope hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news