DODOMA-Serikali imejipanga kuongeza virutubisho vya vitamini na madini kwenye vyakula ambavyo vitasadia kuimarisha kinga ya mwili ikiwa ni jitihada za kuhakikisha changamoto ya ukosefu wa lishe yanayowakabili Watanzania hususani wakinamama wajawazito ambao upelekea kuzaa watoto wa vichwa vikubwa na mgongo wazi inatoweka.
Kauli hiyo imetolewa Desemba 14,2023 jijini Dodoma na Mtafiti na Mratibu wa shughuli za uongezaji virutubishi kitaifa, Selestine Mgoba wakati alipokuwa kwenye warsha ya utiaji maoni kanuni za kuongeza virutubisho kwenye vyakula iliyoandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara na kuwakutanisha wanakamati kutoka Wizara mbalimbali na Sekta binafsi.
"Tunaona kwenye Taifa letu upungufu wa Damu ambao unasababishwa na upungufu wa madini chumvi, zaidi ya asilimia 59 ya watoto wa kitanzania chini ya umri wa miaka mitano wana upungufu wa Damu, kwa hiyo wazalishaji vyakula wakiwa na utaratibu wa kuongeza madini chumvi kwenye vyakula tulivyo vibainisha ikiwemo unga wa ngano, unga wa mahindi,mafuta ya kula na chumvi itasaidia," amesema Mtafiti Mgoba.
Aidha, Mgoba amesema katika kuboresha lishe nchini kuna kiwanda ambacho kinaanzishwa ili kurahisisha upatikanaji wa virutubisho kwa wakati tofauti na hapo awali ambavyo ilitakiwa kuagiza nje ya nchi.


Naye Tumsime Nkyando Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Kimataifa lisilo la Kiserikali la TechnoServe amesema Kanuni zinazojadiliwa zitaleta tija kubwa katika kujenga afya njema kwani watu wasipokuwa na lishe inaweza kupelekea kutokuwa na uwezo mkubwa wa kimaamuzi na kufikiria zaidi.