DAR ES SALAAM-Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetangaza ajira 500 za wauguzi wa kike ambao wataajiriwa na Serikali ya Saudi Arabia mapema mwezi Januari mwaka 2024.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea na dhamira yake thabiti ya kuhakikisha Watanzania wananufaika na fursa za ajira zinazojitokeza kutokana na mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Tanzania na Mataifa mbalimbali duniani.
Mhandisi Luhemeja amesema, mwishoni mwa mwezi Novemba na mwanzoni mwa mwezi Desemba, 2023, Serikali ya Tanzania imesaini hati mbili za makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya kazi na ajira na Serikali ya Saudi Arabia pamoja na Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu.
Vile vile, amesema hati za mashirikiano zilizosainiwa zinatoa fursa za ajira kwenye Mataifa husika kwa kada na sekta zenye kutumia ujuzi wa chini, ujuzi wa kati na ujuzi wa juu.
Amesema,Watanzania wote wenye sifa na ujuzi uliobainishwa wanataarifiwa kuomba kazi husika kwa kujisajili jobs.kazi.go.tz na kutuma wasifu binafsi (CV) kwa njia ya barua pepe esu@taesa.go.tz ambapo mwisho wa kutuma maombi ni Desemba 27,2024.