NA GODFREY NNKO
SERIKALI imetangaza kuyaunganisha mashirika na taasisi 16 ambazo zipo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina ili kuongeza ufanisi kwa ustawi bora katika kuhudumia wananchi na Taifa.
Uamuzi huo umetangazwa leo Desemba 15, 2023 katika Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (Mb.).
Katika mkutano huo mbele ya waandishi wa habari, Mheshimiwa Waziri ameambatana na Katibu Mkuu, Dkt.Tausi Kida na Msajili wa Hazina, Nehemiah Kyando Mchechu.
“Moja, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inaunganishwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) na kuunda taasisi moja inayohusika na utambuzi wa matukio muhimu maishani.
“Kwa hivyo, kutoka kuzaliwa mpaka kufariki tunataka tuwe na taasisi moja ambayo itahusika na utambulisho wake.
“Kwa hiyo, NIDA na RITA zinaunganishwa, lengo ni kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya kuwa na Namba Moja ya Utambulisho kama mnakumbuka.
“Single Identification Number, tunataka Mtanzania iki-click namba yake iwe ni kwa taarifa zote.Kwa hiyo ni shirika la kwanza ambalo Serikali imefanya uamuzi, naomba muupokee.”
Akizungumzia kuhusu shirika la pili, Mheshimiwa Waziri Prof.Mkumbo amesema kuwa, “Benki ya Kilimo Tanzania (TADB) na Mfuko wa Pembejeo wa Kilimo zinaunganishwa ili kuwa na taasisi moja itakayohusika na mikopo na ugharamiaji wa maendeleo ya kilimo nchini.
“Kwa sababu taasisi hizi zote zinahusika na ugharamiaji mikopo kwa sekta ya kilimo, kwa hiyo tumeona hakuna sababu ya kuwa na taasisi mbili, kwa hiyo zimeunganishwa itakuwa taasisi moja kwa jina ambalo baadaye litapatikana kulingana na sekta husika.”
Chai
“Hatua ya tatu, Bodi ya Chai Tanzania inaunganishwa na Wakala wa Maendeleo ya Wakulima wadogo wa Chai Tanzania, zinaunganishwa ili kuwa na bodi moja.Kwa hiyo kutakuwa na bodi moja ya chai ambayo itachukua majukumu ya hizo taasisi mbili.
Nyama
“Nne, Bodi ya Nyama inaunganishwa na Bodi ya Bodi ya Maziwa ili kuunda taasisi moja ya kuendeleza na kusimamia mazao ya mifugo yakiwemo ya nyama na maziwa.
“Namba tano, hap ani taasisi tatu zinaunganishwa kwa pamoja, Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMATEC) kipo Arusha hiki, Taasisi ya Uandisi na Usanifu wa Mitambo (TEMDO) na yenyewe ipo Arusha na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) zinaunganishwa ili kuunda taasisi moja.
“Sita, Kituo cha Uwekezaji (TIC) kipo ofisini kwangu hiki.Kwa hiyo, Kituo cha Uwekezaji (TIC) kinaunganishwa na Mamlaka ya Uzalishaji wa Mauzo ya Nje (EPZA) ili kuunda taasisi moja itakayoratibu uwekezaji wa sekta binafsi wa ndani na kutoka nje ya nchi.
“Kwa hiyo tunakwenda kuwa na wakala mmoja wa Taifa ambaye anawajibika kwa sekta binafsi katika uwekezaji.
“Saba, Taasisi ya Utafiti wa Chai Tanzania na Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku Tanzania na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa zinaunganishwa na kuwa sehemu ya muundoa wa taasisi ya utafiti wa kilimo Tanzania (TARI).
“Mnaifahamu TARI, tumeona zote zinazohusiana na tafiti za mazao tuwe na taasisi moja inayohusika na kilimo, inatosha.
“Ukihesabu hayo yote ni mashirika 16 yataunganishwa na tutabaki na mashirika machache ambayo ukihesabu hapo utayaona.”