NA GODFREY NNKO
SERIKALI imetangaza kuyafuta na kuzivunja baadhi ya taasisi na mashirika ya umma yaliyopo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina nchini.
Uamuzi huo umetangazwa leo Desemba 15, 2023 katika Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (Mb.).
Katika mkutano huo mbele ya waandishi wa habari, Mheshimiwa Waziri ameambatana na Katibu Mkuu, Dkt.Tausi Kida na Msajili wa Hazina, Nehemiah Kyando Mchechu.
“Sasa huu ndiyo uamuzi mgumu zaidi, kwa wale ambao wanafutwa. Mashirika na taasisi za umma zinazofutwa ama kuvunjwa, kuna tofauti kati ya kufutwa ama kuvunja.
“Moja, Shirika la Uzalishaji la Jeshi la Polisi linafutwa, pili Taasisi ya Chakula na Lishe inafutwa.Tatu, Bodi ya Pareto inafutwa, na shughuli zake zitahamishiwa katika Mamlaka ya Usimamizi wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko.
“Namba nne, shirika ambalo tunalivunja, kuna tofauti hapo. Shirika la Elimu Kibaha linavunjwa na kuunda Shule ya Sekondari Kibaha ama kwa jina ambalo mamlaka husika zitaamua na chuo cha ufundi.
“Shirika la Elimu Kibaha lilikuwa na taasisi tatu ndani yake, tulikuwa na Shule ya Sekondari Kibaha na chuo cha ufundi.
“Lakini,walikuwa pia na Hospitali ya Tumbi Kibaha maarufu, sasa hapa hatufuti, ndiyo maana nimesema tunavunja.
"Hizi taasisi zinaendelea kuwepo, tunabadilisha muundo kwa hiyo sekondari itaendelea kuwa sekondari chini ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI.
“Shule ya Sekondari Kibaha ama jina ambalo mamlaka husika zitaamua, Chuo cha Ufundi kinaendelea kuwa chuo cha ufundi kama kawaida na Hospitali ya Tumbi Kibaha inakuwa Hospitali ya Mkoa wa Pwani chini ya Wizara ya Afya.
“Hilo ni badiliko kubwa, kwa sababu mwanzoni zote zilikuwa chini ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI.Kwa hiyo tunaiondoa Hospitali ya Tumbi Kibaha moja haitakuwa chini ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa taratibu ya muundo wa sekta ya afya.
“Sasa itakuwa chini ya Wizara ya Afya na kwa sababu hiyo Wizara ya Afya wameshaamua kuipandisha hadhi, itakuwa ndiyo Hospitali ya Mkoa wa Pwani.
“Na tumeshamwelekeza Msajili wa Hazina tayari akamilishe utaratibu wa kuhamisha Hospitali ya Tumbi Kibaha kwenda Wizara ya Afya mapema iwezekanavyo.
“Kwa sababu tumeshafanya uamuzi na mchakato wa kuhamisha unaendelea na upo chini ya Msajili wa Hazina, hilo alikamilishe.
“Kwa hiyo, ndugu zangu hayo ndiyo maamuzi ya msingi ya Serikali ambayo Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameridhia na ameniagiza leo niyatangaze kwa umma wa Watanzania,”amefafanua Waziri Prof.Mkumbo.