FRANCIS TOWN-Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam nchini Tanzania imeshindwa kuonesha umahiri wake ugenini katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika.
Ni baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana dhidi ya wenyeji, Jwaneng Galaxy FC ya nchini Botswana.
Mtanange huo wa Kundi B umepigwa leo Desemba 2, 2023 katika Dimba la Francistown lililopo Francistown nchini Botswana.
Simba SC walishindwa kutumia nafasi walizozipata kutoka kwa wenyeji hao huku wakiwa na Kocha wao mpya Abdelhak Benchikha licha ya mara nyingi kuonekana kuutawala mtanange huo.
Aidha, kwa matokeo hayo Simba wamefikisha alama mbili baada ya kutoka sare ya kufungana bao 1-1 na ASEC Mimosas ya Ivory Coast huku Jwaneg Galaxy wanafikisha alama nne.
Watswana hao wiki iliyopita walianza kwa ushindi wa ugenini wa 1-0 dhidi ya Wydad Athletic jijini Marrakech nchini Morocco.
Hata hivyo, wawakilishi hao wa Tanzania katika michuano ya Kimataifa watashuka tena dimbani Desemba 9, mwaka huu kucheza na wenyeji Wydad Casablanca nchini Morocco.
Wakati huo huo,Jwaneng ya Botswana watakuwa wenyeji dhidi ya ASEC Mimosas siku hiyo katika Dimba la Francistown nchini Botswana.