Taaluma ya habari lazima iheshimiwe na kuthaminiwa, kwani mchango wenu ni mkubwa-RC Mtanda

NA FRESHA KINASA

MKUU wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Said Mohamed Mtanda amesema, anathamini mchango na kazi za waandishi wa habari mkoani humo.

Pia, amesema ataendelea kushirikiana nao kwani wana mchango mkubwa katika kuchangia maendeleo ya mkoa huo ikiwemo kutangaza fursa na miradi inayotekelezwa na Serikali.
Mheshimiwa Mtanda ameyasema hayo Desemba 29, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani humo katika Ukumbi wa Uwekezaji uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo Mjini Musoma.

Katika hotuba yake kwa waandishi wa habari Mheshimiwa Mtanda amewahimiza waandishi wa habari kuandika habari za ukweli ambazo zitachangia kuibua changamoto na Serikali kuzifanyia kazi kwa maslahi mapana ya wananchi.

Huku akiwataka pia viongozi wote wa Serikali na mashirika ya umma mkoani humo kuwathamini waandishi wa habari na kushirikiana nao.

"Natamani kuona waandishi wa Mkoa wa Mara mnafanya kazi kwa uhuru, na pia mnapopata taarifa zenye matishio toeni taarifa kwa viongozi wa serikali.

"Taaluma ya habari lazima iheshimiwe na kuthaminiwa, kwani mchango wenu ni mkubwa na Serikali ya mkoa itaendelea kuheshimu na kuthamini mchango wenu katika kuwahabarisha wananchi na pia kuibua changamoto na Serikali kufanyia kazi."
Pia,Mheshimiwa Mtanda amewataka Maafisa Habari wa Halmashauri zote za Mkoa wa Mara kuwa wabunifu na pia kuvitumia vyombo vya habari vya kijamii,kwani vina mchango mkubwa wa kuhabarisha na kutoa taarifa ambazo zinawahabarisha wananchi juu ya mambo mbalimbali ambayo serikali imekuwa ikifanya.

Aidha, Mtanda amewahimiza waandishi wa habari kuendelea kuzingatia weledi na maadili ya taaluma yao na kuwa daraja zuri kati ya wananchi na Serikali, kwa kuwapasha habari wananchi zenye ubora na pia zitakazochangia kuutangaza vyema Mkoa wa Mara na fursa zilizomo.

Aidha, Mheshimiwa Mtanda amewaomba wananchi wa Mkoa wa Mara,viongozi wa serikali,wazawa wa Mkoa wa Mara,wabunge , wanasiasa, viongozi wa mashirika na viongozi wa dini kuungana kwa pamoja kuleta maendeleo ya nkoa huo na kuachana na ubinafsi.

"Mkoa wa Mara ni mkoa kinara kwa siasa za Taifa hili, umemtoa kiongozi mahairi na Mwasisi wa Taifa la Tanzania kwa hiyo niwaombe tuungane sote kwa pamoja tuwe na ushirikiano wa pamoja hakuna kiongozi pekee anaweza kuleta maendeleo peke yake pasipo ushirikiano,"amesema Mhehimiwa Mtanda.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Mtanda amesema anaandaa mpango wa kutembelea vijiji vyote vya Mkoa wa Mara ambavyo havijatembelewa na Mkuu wa Mkoa kwa muda miaka mingi kusikiliza changamoto zao, huku akiwataka wananchi kujitokeza.

Raphael Okello ni Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara amesema, Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara (MRPC) itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wote pamoja na kusimamia maadili ya waandishi wa habari ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news