NA GODFREY NNKO
WAKALA wa Barabara Tanzania (TANROADS) imerejesha mawasiliano ya barabara Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam kupitia Bagamoyo.
Ni baada ya daraja la Mpiji linalounganisha mikoa hiyo kupata changamoto ya kumomonyoka kutokana na mvua za El-nino. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Desemba 9, 2023 na Kitengo cha Uhusiano, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, daraja hilo ambalo lipo mpakani mwa mikoa hiyo lilifungwa Desemba 8, 2023 kwa ajili ya usalama wa wasafiri.
Aidha, daraja hilo limefunguliwa Desemba 9, 2023 saa 12 asubuhi baada ya wataalam kufanya jitihada za kutengeneza hitilatu iliyojitokeza.
Vile vile, TANROADS imeruhusu watumiaji wa barabara hiyo kupitia upande mmoja wa daraja baada ya matengenezo kukamilika huku timu ya wataalam wa TANROADS wakiendelea kufanya matengenezo mengine ya haraka kulirejesha daraja hilo kwenye hali yake ya awali na kulifanya liwe na uimara zaidi.
“TANROADS inaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza kuanzia Ijumaa tarehe 8 Desemba, 2023,”imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.