Tanzania yanadi fursa za uwekezaji Korea

NA DIRAMAKINI

BALOZI wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Korea Kusini, Mheshimiwa Togolani Mavura amewakaribisha Wakorea kuja kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali.

Hayo ameyabainisha muda mfupi jijini Busan nchini humo baada ya wasilisho lake kuhusu fursa zinazopatikana ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa vikao vya Mkutano wa Saba wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea Kusini na Nchi za Afrika (KOAFEC).

"Leo nimepata fursa ya kufanya wasilisho katika mkutano huu ambapo nchi nne zilipewa nafasi ya kufanya wasilisho kutoka Afrika ambao ni Tanzania, Jamhuri ya Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Jamhuri ya Ivory Coast.

"Katika wasilisho letu, kwanza tumejaribu kuonesha Tanzania ni nchi ambayo iko stable ni nchi iliyotulia yenye utulivu wa amani na kiusalama, lakini yenye utulivu wa kiuchumi, yenye jografia ya kimkakati ambapo nchi sita zinategemea Tanzania kama mlango wa bahari.

"Lakini, ni nchi ambayo ina ardhi kubwa, inayoweza kutupeleka kwenye kilimo endelevu kinachojali mazingira, lakini vile vile nchi yenye vyanzo vingi vya kuweza kuzalisha umeme kwa nishati jadidifu kwa maana ya uwezo mkubwa wa umeme wa jua, umeme wa upepo.

"Lakini, kubwa zaidi kuliko yote ni uwepo wa madini ya kimkakati ya graphite, nickel na nithium, ambayo ndiyo madini yanayohitajika zaidi katika kuzalisha miundombinu na mitambo ya kuzalisha umeme wa nishati jadidifu ambao tunao nchini Tanzania.

"Tumezungumzia kuhusiana na sekta ya utalii na uchumi wa bahari (blue economy) kwa sababu kwenye uchumi wa bahari nako siku hizi kuna blue credity zinapatikana kule,kuona ni namna gani Wakorea tumewakaribisha Tanzania kuja kuwekeza ili tuweze kwa pamoja kusukuma kurudumu la maendeleo ya nchi yetu,"amesema Balozi huyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news