ARUSHA-Wataalamu wa mionzi kutoka nchi 35 barani Afrika wapo jijini Arusha katika mkutano wa siku tano unaolenga kujadili hi usalama wa mionzi kwa wafanyakazi wanaofanya kazi katika vyanzo vya mionzi kama hospitalini, viwandani na migodini.
Akizungumza kando ya mkutano huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania, Prof. Lazaro Busagala, Mkurugenzi wa Teknolojia na Huduma za Ufundi TAEC, Dkt. Remigius Ambrose Kawala amesema, mkutano huo ni mahususi kwa ajili ya kutathmini na kujengeana uwezo kwa nchi wanachama wa Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomu ili kuhakikisa usalama wa wafanyakazi unazingatiwa sehemu za kazi.
Pia, mkutamo huu una lengo la kuweka maazimio na vigezo vya tathmini vya pamoja vya namna bora ya kuwalinda wafanyakazi wanaofanya kazi katika vyanzo vya mionzi.
Akizungumza kwa njia ya mtandao Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomu, Prof. Abdul Razak Shaukat amesema,kuna nchi bado hazifanyi vizuri katika usalama kwa wafanyakazi wanaofanya kazi katika vyanzo vya mionzi, hivyo mkutano huo usaidie kupeana mbinu za kuimarisha utendaji.
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo kutoka Nigeria, Kenya, Zimbabwe na Ethiopia wamesema,wanafurahia kuwa nchini Tanzania na mkutano huo utazaa matunda mazuri katika kusimamia usalama wa wafanyakazi wanaofanya kazi katika vyanzo vya mionzi sehemu wanazotoka.