NA CATHERINE SUNGURA
WAKALA ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imejipanga kujenga madaraja 189 kwa kutumia teknolojia ya mawe katika mikoa yote ishirini na sita nchi nzima kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Mhandisi Mshauri Pharles Ngeleja akimueleza Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa namna wanavyotumia teknolojia mbadala kujenga madaraja na barabara nchini.Katikati ni Rais wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET),Mhandisi Dkt. Gemma Modu wakati wa Kongamano la Kitaifa la 32 la Wahandisi Tanzania jijini Arusha.
Hayo yameelezwa na Mratibu wa madaraja hayo, Mhandisi Pharles Ngeleja wakati Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa alipotembelea banda la TARURA kwenye Kongamano la Kitaifa la 32 la Taasisi ya Wahandisi Tanzania lililofanyika kwa siku mbili katika Kituo cha Kimataifa cha Mkutano Arusha (AICC).
Mhandisi Ngeleja alisema hadi sasa wameweza kujenga madaraja 56 ya mawe ambapo utaratibu wa ujenzi wa madaraja mengine unafanyiwa kazi.
Mtendaji Mkuu wa AICC, Bw. Ephraim Mafuru akisaini kitabu cha wageni kwenye banda la TARURA wakati wa Kongamano la Kitaifa la 32 la Wahandisi Tanzania lililofanyika jijini Arusha.
Alisema, teknolojia ya ujenzi wa madaraja kwa kutumia mawe na matofali ya kuchoma pamoja na ujenzi wa barabara kwa kutumia mawe ilikuja baada ya kuwa na mtandao mkubwa wa barabara na hivyo kuweza kutumia teknolojia hiyo ili kupunguza gharama za ujenzi.
“Ulinganifu wa barabara zetu zina mtandao wa Km 144,429.77, mtandao huu ni mkubwa sana hivyo tuliona tutumie teknolojia hii ya mawe ili tuweze kuwafungulia njia wananchi kuweza kufika maeneo yao ya huduma za jamii."
Mtendaji Mkuu wa AICC Bw. Ephraim Mafuru akipata maelezo kutoka kwa maofisa uhusiano na mawasiliano wa TARURA wakati akipotembelea banda la Wakala huo wakati wa Kongamano la Kitaifa la 32 la Wahandisi Tanzania lililofanyika jijini Arusha.
Ameongeza kuwa,tangu mwaka 2017 hadi sasa TARURA imeweza kujenga madaraja 212 yenye gharama ya shilingi Bilioni 8.2 na kama wangejenga kwa kutumia zege wangetumia zaidi ya shilingi 36. “Teknolojia hiyo imeweza kupungunguza gharama mpaka asilimia 80."
Aidha, amesema mawe pamoja na matofali wanayoyatumia hupimwa maabara na kiwango cha chini cha ugumu wa mawe (MPA) huwa zaidi ya 25 na matofali ‘MPA’8 ndio hujengea madaraja.
Naye, Rais wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET) Mhandisi Dkt. Gemma Modu alisema Uhandisi una mchango mkubwa wakuleta maendeleo nchini.
Pia ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza kasi ya maendeleo nchini na kuongeza wahandisi wazawa na kuwafungulia fursa wahandisi na mafundi na kuahidi kushirikiana bega kwa bega na Serikali.