DAR ES SALAAM-Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kushirikiana na Kampuni ya Udalali ya Mahakama imeanza zoezi la kuwaondoka kwenye nyumba zake wapangaji wadaiwa sugu ambao ni Watumishi wa umma na viongozi wa Serikali.
Kaimu Meneja wa TBA Mkoa wa Dar es Salaam,Arch. Bernard Mayemba amesema wameanza kuondoa wapangaji wa nyumba za XNMC zilizopo Mbezi Beach.
Ameeleza kuwa zoezi hilo, lilipaswa kuanza rasmi nchi mzima Desemba 1, 2023, lakini kwa Mkoa wa Dar es Salaam wameamua kuanza Novemba 29,mwaka huu na hakuna cha kusubiri kwani notisi imeshaisha muda wake.
“Mkoa wa Dar es Salaam una jumla ya Nyumba 1200 za watumishi wa umma waliopangisha, na kiasi kinachodaiwa kutoka kwa wapangaji ni shilingi bilioni 1.1,” amesema Arch. Mayemba.
Amesema kuwa,zoezi hilo litafanyika kwa takribani wiki tatu na kuwa hawataangalia sura ya mtu na kwamba fedha watakazopata kupitia madeni hayo yatawasaidia kukarabati nyumba na miundombinu mingine ili kuhakikisha kunakuwa na mazingira mazuri kwa wapangaji.