TFRA yaipongeza Premium Agro Chem Ltd kwa kutoa chakula bure shule 35 kila siku Dar

DAR ES SALAAM-Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent amepongeza huduma ya chakula inayotolewa na Kampuni ya Mbolea ya Primium Agro Chem Ltd kwa wanafunzi wa shule za msingi zinazozunguka eneo yaliko maghala wanayohifadhia mbolea kabla ya kupeleka sokoni.
Amesema, kutoa huduma hiyo kunaongeza kuwepo kwa mahusiano mazuri na ushirikiano baina ya wafanyabiashara na wananchi wanaowazunguka na hivyo kurahisisha utendaji wao.

Aidha, Laurent ameziasa kampuni nyingine za mbolea kuwa na mipango inayotekelezeka wanayoifanya kwa jamii zinazowazunguka ili kuwa na mahusiano mazuri baina yao.
Laurent ametoa pongezi hizo mwishoni mwa wiki alipotembelea ghala la Kampuni ya Mbolea ya Premium na kuoneshwa jiko linalotumika kuandaa chakula cha mchana kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi na kukisambaza ili kuwa na muda mrefu wa kusoma badala ya kurudi majumbani kwa ajili ya kushiriki chakula cha mchana.

Akizungumza wakati wa ziara iliyofanywa na Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA na wasaidizi wake katika ghala lao, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mbolea ya Premium, Brijesh Barot alisema kwa siku huwa wakiandaa chakula kiasi cha kilo za mchele 1700, maharage, kunde, choroko kilo 170 - 180 ambapo hulisha kwa siku tano za wiki yaani Jumatatu hadi Ijumaa.
Ameeleza kuwa wanazifikia shule 35 za msingi ikiwa ni pamoja na Shule ya Buyuni, Nyeburu, Mgeule, Kimanga, Tumaini, Darajani, Liwiti, Misewe, Tabata (P), Tabata (J), Mtambani, Buguruni, Buguruni (M), Buguruni (K), Buguruni (S), Hekima, Kombo na Mtakuja.

Shule nyingine ni Bahati, Ruvuma, Temeke, Zimbiri, Bonyokwa, Magoza, Segerea, Maendeleo, Bwawani, Umoja, Yombo, Mwale, Kiwalani, Kigilagila, Muungano, Vingunguti, Kizinga, Uhuru na Zimbiri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news