Tuongeze nguvu elimu dhidi ya ukatili wa kijinsia-Serikali

NA FRESHA KINASA

SERIKALI imewataka wadau na mashirika yanayojishughulisha na mapambano ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia maeneo mbalimbali hapa nchini kuongeza nguvu hasa utoaji wa elimu kwa jamii kuwezesha kutokomeza vitendo hivyo.
Ambapo, vitendo hivyo vimetajwa kurudisha nyuma juhudi za maendeleo na jitihada za kuleta usawa kutokana na madhara yanayogusa maisha ya mtu mmoja mmoja, familia na jamii kwa ujumla ambayo ni kinyume cha sheria za nchi na haki za binadamu.

Miongoni mwa vitendo vya ukatili ambayo vinapaswa kushughulikiwa ni pamoja na ukeketaji, ndoa za utotoni, ajira za Watoto, vipigo kwa wanawake na watoto, ubakaji, ulawiti, wanaume kukimbia familia zao, rushwa ya ngono na manyanyaso mbalimbali.
Kauli hiyo imetolewa Desemba 10, 2023 na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dkt. Yahya Nawanda wakati akihitimisha kilele cha siku 16 za kupinga ukatili wa Kijinsia katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Nyamongo wilayani Tarime Mkoa Mara ambapo wadau, mashirika Wananchi na Viongozi mbalimbali wa serikali wamehudhuria chini ya kauli mbiu isemayo 'Wekeza Kuzuia Ukatili wa Kijinsia'.

Dkt. Nawanda amesema kuwa, wadau na mashirika wakiongeza nguvu na uwajibikaji katika maeneo yao vitendo hivyo itakuwa rahisi kuvitokomeza kwani Serikali imekuwa ikifanya inahitaji kuona wadau na mashirika yote wakisimama kidete kuhakikisha wanatokomeza kupitia miradi wanayoifanya na kuongeza Kasi ya utoaji wa elimu kwa jamii.
Amesema, Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa wote ambao watabainika kufanya vitendo hivyo na kwamba, Wananchi kwa nafasi yao wanalojukumu la kuwafichua mbele ya vyombo vya dola wahusika wanaofanya vitendo hivyo bila kuwafichua.

Aidha,amelitaka Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara na Wilaya ya Tarime ambako vitendo vya ukeketaji vimekuwa vikifanyika kwa kiasi kikubwa, kuwakamata wahusika na kuwafikisha mahakamani. Akisema kuwa kamwe ukeketaji na vitendo vyote vya ukatili wa Kijinsia havijawahi kuwa na faida kwa jamii bali madhara yake ni makubwa.

Dkt. Nawanda amewapongeza WiLDAF kwa kuendelea kuratibu harakati za Usawa wa Kijinsia kwa kushirikiana na Mashirika mbalimbali kwa ufanisi. ambapo matokeo yameendelea kuwa mazuri na pia amewaomba kuzidi kusonga mbele kwani mchango wao ni mkubwa katika kuleta mabadiliko.
"Ukeketaji haujawahi kuwa na fadia hata kidogo, badala yake kuleta madhara nimeambiwa ukeketaji unafanyika hasa Tarime niwaagize Jeshi la Polisi muwakamate wote wanaobainika.

"Na pia Serikali ya Kenya na Tanzania tusaidiane maana nimeambiwa wapo wakiona Kenya wanakamatwa wanakimbilia upande wa Tanzania tukishirikiana wote tutaimarisha udhibiti,"amesema Dkt. Nawanda.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tarime,Kanali Michael Mtenjele amesema kuwa changamoto kubwa iliyopo katika Wilaya ya Tarime ni ukeketaji umekuwa ukihusisha mipaka. Ambapo wakiona Serikali imechachamaa wapo wamekuwa wakiwapeleka wasichana kukeketwa nchini Kenya na wapo wasichana wa Kenya huja kukeketwa Tanzania.
"Tumekuwa na vikao kati ya Kenya na Tanzania mwezi Agasti mwaka huu, kudhibiti Jambo hili kwani kumekuwa na wengine wanawapeleka Kenya na madhara ya ukeketaji Watoto wamekuwa wakiacha masomo wanaamini kwamba Binti akikeketwa yupo tayari kuozeshwa,"amesema na kuongeza kuwa.

"Jambo jingine pia utayari bado ni mdogo kwa baadhi ya viongozi kulikemea lazime Sasa utayari kwa wote uwepo na Jamii nzima tuungane badala ya Serikali na mashirika pekee. Na pia ikibidi mwakani naomba kambi ya kutoa elimu ya ukatili ifanyike hapa Tarime kwani vitendo vya ukatili hasa ukeketaji bado ni vingi na mwaka huo unagawanyika kwa mbili hivyo ukeketaji iutafanyika kwa kiwango kikubwa," amesema Kanali Mtenjele.

Naye Mkurugenzi wa Jinsia Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia wanawake na Makundi Maalum, Badru Abdunuru amesema kuwa, wizara hiyo itaendelea kuelimisha jamii juu ya madhara ya ukatili wa Kijinsia, kuimarisha haki za binadamu kama yalivyo matakwa ya katiba ya nchi.

Ameongeza kuwa, katika siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kazi mbalimbali zimefanyika ikiwemo utoaji wa elimu ya madhara ya ukatili wa Kijinsia kwa Wananchi yakiwemo maeneo ya mikusanyiko ya watu, makanisani, Mashuleni kwa kuendesha midaharo, makongamano.

Amesema,mikoa iliyofikiwa kupewa elimu hiyo na msafara wa kutoa elimu ya ukatili wa Kijinsia kutoka jijini Dar es laam ni pamoja na Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Kagera, Kigoma, Geita na Mkoa wa Mara.

Mkurugenzi wa WiLDAF, Anna Kulaya amewataka wanaume kujitokeza hadharani wanapofanyiwa vitendo vya ukatili wa Kijinsia badala ya kunyaza na kushindwa kupaza sauti kueleza madhila yanayowasibu.

Kulaya amewaomba wazee wa kimila wa Wilaya ya Tarime na maeneo mbalimbali wasaidie kutoa hamasa kwa wanaume waweze kujitokeza kwani kukaa kimya ni kuvipa nafasi vitendo vya ukatili vizidi kufanyika Jambo ambalo ni kinyume cha sheria na haki za binadamu ambapo Tanzania imeridhia mikataba hiyo na matamko ya Kimataifa na kikanda.

Katika siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia zaidi ya wanafunzi 8,503 wa shule za Sekondari wamefikiwa, klabu 13 za kupinga ukatili zimezinduliwa, vituo 17 vya boda boda vimefikiwa na wadereva boda boda zaidi 347 wameelimishwa, watu wenye ulemavu zaidi ya 252 na walimu 2 wenye ulemavu wamefikiwa, misikiti mitano na makanisa manne yamefikiwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news