Ujenzi wa Shule ya Msingi Mahaha,Kibondo waishukuru Serikali

KIGOMA-Ujenzi wa Shule ya Msingi Mahaha umetajwa kuwaondolea adha ya kutembea zaidi ya kilomita 20 wanafunzi kutoka Kitongoji cha Mahaha kilichopo kijiji cha Magalama wilayani Kibondo mkoani Kigoma.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa shule hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Afisa Elimu Awali na Msingi Oliver Mgeni amesema Miundombinu imekamilika na kuanzia Januari 2024 shule itapokea wanafunzi wa Elimu Awali na Msingi kuanzia Darasa la kwanza hadi la Saba.

"Tunaishukuru serikali kupitia mradi wa BOOST kwa kutenga fedha kiasi cha Shilingi 361,500,000 ili kujenga Shule hii kwani watoto wote kutoka kitongoji cha Mahaha waliokuwa wakisoma katika kijiji cha Magalama watarejeshwa hapa ili wasome katika shule hii ya kisasa iliyojengwa jirani na makazi yao," amesema Oliver Mgeni kupitia taarifa hiyo.

Aidha,kukamilika kwa Shule hiyo kutaongeza ari ya wanafunzi kusoma, kuongeza namba ya usajili wa wanafunzi pamoja na kupunguza idadi ya wakazi wasiojua kusoma na kuandika kupitia MEMKWA katika eneo hilo.

Baadhi ya wakazi katika kitongoji hicho wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwasogezea huduma hiyo jirani kwani itaimarisha Usalama wa watoto wao kwenda na kurejea kutoka shule.

"Watoto wengi walikuwa watoro, wengine waliacha shule na hata baadhi ya wazazi kuhofia kuwaandikisha watoto Elimu awali na Msingi kutokana watoto hao kutomudu kutembea umbali huo pamoja na kuhofia usalama wao wakiwa njiani kwani kuna nyakati hurejea nyumbani usiku au hunyeshewa na mvua," ameeleza Theresia Kanwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news