Ujumbe wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi watembelea Benki Kuu jijini Dar es Salaam

DAR ES SALAAM-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kama mhimili wa mfumo wa fedha nchini ina mchango mkubwa kuhakikisha maendeleo na uhimilivu wa kiuchumi, ambayo ni misingi muhimu ya usalama wa taifa.

Wanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi wakifuatilia wasilisho kuhusu Wajibu wa Benki Kuu katika kukuza usalama wa taifa lililotolewa na Meneja, Utafiti kutoka Kurugenzi ya Utafiti and Sera za Uchumi, Dkt. Deogratias Macha.

Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Sera za Uchumi na Fedha, Dkt. Yamungu Kayandabila amesema hayo wakati akiukaribisha ujumbe wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi ulipotembelea Benki Kuu jijini Dar es Salaam. Ujumbe huo uliongozwa na Mkuu wa Chuo hicho, Balozi Meja Jenerali Wilbert Ibuge, wakufunzi na wanafunzi 53.

Dkt. Kayandabila amesema, katika mazingira ya dunia ya sasa yanayobadilika, wajibu wa benki kuu duniani ni zaidi ya majukumu yanayohusu fedha.
Naibu Gavana wa BoT, Sera za Uchumi na Fedha, Dkt. Yamungu Kayandabila, akizungumza wakati akiukaribisha ujumbe wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi ulipotembelea Benki Kuu jijini Dar es Salaam.

“Sisi hapa Benki Kuu ya Tanzania tunaelewa sana kuhusu uhusiano wa karibu kati ya utulivu wa uchumi na usalama wa taifa letu kwa ujumla,” alisema na kuongeza kuwa uchumi imara siyo tu kwa ajili ya kukidhi malengo ya kifedha au kibajeti, bali pia ni muhimu sana katika usalama wa taifa.
Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi , Balozi Meja Jenerali Wilbert Ibuge, akikabidhiwa zawadi na Naibu Gavana wa BoT, Sera za Uchumi na Fedha, Dkt. Yamungu Kayandabila, wakati wa ziara ya wanafunzi wa chuo hicho Benki Kuu jijini Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo, Benki Kuu ilifanya wasilisho kuhusu Wajibu wa Benki Kuu katika kukuza usalama wa taifa (Role of the Bank of Tanzania in promoting national security). Wasilisho hili lilifanywa na Meneja, Utafiti kutoka Kurugenzi ya Utafiti and Sera za Uchumi, Dkt. Deogratias Macha, na kufuatiwa na kipindi cha maswali na majibu kutoka kwa wanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi.
Mkurugenzi wa Utafiti and Sera za Uchumi, Dkt. Suleiman Missango, akizungumza wakati wa ziara ya wanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Benki Kuu jijini Dar es Salaam.

Chuo cha Taifa cha Ulinzi kilianzishwa mwaka 2012 na huwaleta pamoja maofisa wa ngazi za juu wa serikali na taasisi zingine kupata mafunzo ya kimkakati yanayohusu usalama wa taifa.
Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi , Balozi Meja Jenerali Wilbert Ibuge, akizungumza wakati wa ziara ya wanafunzi wa chuo hicho Benki Kuu jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo ya mafunzo, Mkuu wa Chuo hicho Balozi Meja Jenerali Ibuge alisema kati ya wanafunzi 53, Watanzania ni 31 na maafisa waandamizi 22 wanatoka nchi marafiki barani Afrika na Asia.
Meneja, Utafiti kutoka Kurugenzi ya Utafiti and Sera za Uchumi, Dkt. Deogratias Macha, akiwasilisha mada kuhusu Wajibu wa Benki Kuu katika kukuza usalama wa taifa kwa ujumbe wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi ulipotembelea Benki Kuu jijini Dar es Salaam

Balozi Maj. Jenerali Ibuge alisema wanafunzi hao wameanza kujifunza masuala ya uchumi na uhusiano na usalama wa taifa na kuona ni muhimu kutembelea Benki Kuu ya Tanzania ili kujifunza kazi zake.

Ameishukuru Benki Kuu kwa kuwakaribisha na kueleza matumaini yake kwamba ushirikiano huo utaendelea.
Naibu Gavana wa BoT, Sera za Uchumi na Fedha, Dkt. Yamungu Kayandabila, akikabidhiwa zawadi na Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi , Balozi Meja Jenerali Wilbert Ibuge, wakati wa ziara ya wanafunzi wa chuo hicho Benki Kuu jijini Dar es Salaam.

Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Uthabiti wa Sekta ya Fedha, Bi Sauda Msemo, menejimenti na wafanyakazi kadha wa Benki Kuu pia walikuwepo kuwapokea wageni hao.

Chuo cha Taifa cha Ulinzi kinatoa mafunzo ya muda mrefu na ya muda mfupi yanayohusiana na usalama wa taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news