NA GODFREY NNKO
WAKALA wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) umesema umeendelea kuboresha mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (BPS) ili kuendelea kupata bei halisia kutoka kwenye soko la Dunia.
Sambamba na kuongeza kiwango cha mafuta kupitia Mfumo wa Uagizaji kwa Pamoja na kuvutia waletaji wengi zaidi kushiriki katika mfumo huo hasa nchi zilizotuzunguka ambazo zinategemea bandari zetu.
Hayo yamesemwa Desemba 11, 2023 na Mtendaji Mkuu wa PBPA, Erasto Mulokozi katika kikao kazi baina ya wakala huo na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Amesema, wanapokea wawakilishi wa nchi mbalimbali wanaofika kujifunza kuhusu Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (Bulk Procurement System – BPS).
Mulokozi amesema, miongoni mwa nchi ambazo zimekuja kujifunza kuhusu mfumo huo na wengine wapo mbioni kuja nchini ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Uganda, Rwanda, Namibia na Msumbiji.
“Wenzetu wa nchi jirani wanakuja kujifunza kuhusu mfumo huu ambao una mafanikio makubwa kwa nchi yetu, Msumbiji wao walikuwa nao, lakini huu wetu umeboreshwa zaidi, hivyo wanakuja kujifunza,”amesema Mulokozi.
Amesema, tangu Serikali ilipoanzisha wakala huo, yamepatikana mafanikio mengi ikiwemo uhakika wa upatikanaji wa mafuta ambayo yanayotosheleza mahitaji ya nchi na yenye viwango vya ubora unaotakiwa wakati wote.
Katika hatua nyingine amesema,wakala utaendelea kushirikiana na taasisi wadau katika kuboresha zaidi mfumo huu ili uendelee kuongeza tija kwa maslahi mapana ya Taifa kwa ujumla.
Historia
Akitoa historia fupi kuhusu Sekta ya Mafuta nchini, Mulokozi amesema,mwaka 1977 hadi 1997, sekta ndogo ya mafuta Tanzania ilidhibitiwa na Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Amebainisha kuwa,uagizaji wa mafuta ghafi, usafishaji na usambazaji wa mafuta safi ulifanywa na TPDC.
“Katika kipindi kile mafuta ghafi yaliyoagizwa na TPDC yalisafishwa katika kiwanda cha kusafisha mafuta cha TIPER.Bei ya mafuta ilipangwa na kupitiwa mara kwa mara na Serikali.”
Afisa Mwandamizi wa Habari na Mawasiliano kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina,Sabato Kosuri akifafanua jambo wakati akifungua kikao kazi baina PBPA na wahariri kilichoratibiwa na ofisi hiyo jijini Dar es Salaam Disemba 11, 2023. Kushoto ni Mkaguzi wa Petroli PBPA, Bruno Tarimo na katikati ni Mkaguzi wa Ndani, Juma Hamidu.
Pia amebainisha kuwa, kampuni zote za biashara ya mafuta zilinunua mafuta kutoka TPDC kulingana na kiwango cha umiliki wa biashara katika soko (market share).
Mulokozi amefafanua kuwa, kutokana na mabadiliko ya sera yaliyotokea mwishoni mwa miaka ya tisini Serikali ilianzisha sera ya uchumi huria na hivyo kubadili mfumo wa biashara ya mafuta kuwa ya soko huria kupitia Kanuni za Mpito za Mafuta (Interim Petroleum Regulations);
Kwa kuingia katika mfumo wa soko huria, Mtendaji Mkuu huyo amesema Serikali ilitarajia kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za mafuta nchini kwa kuhamasisha ushindani katika sekta kwa manufaa ya watumiaji na uchumi wa nchi.
Vile vile, kupunguza gharama za ununuzi, utunzaji, usafirishaji na usambazaji mafuta kwa kuondoa mapungufu yaliyokuwepo kwenye mnyororo wa sekta ya mafuta.
Sambamba na kuvutia uwekezaji katika mkondo wa chini wa sekta ya mafuta ili kuwa na miundombinu toshelezi ya uhifadhi na usambazaji wa mafuta na kuhakikisha upatikanaji wa mafuta nchini kote;
Mtendaji Mkuu huyo amefafanua kuwa, uamuzi wa Serikali wa kuacha kusimamia sekta ya mafuta ulifanyika katika vipindi vikuu viwili ambavyo vinajumuisha kati ya mwaka 1997 na 1999.
Anasema, TPDC iliendelea kuagiza mafuta ghafi, kuyasafisha katika kiwanda cha TIPER na kuyauza kwa Kampuni za Biashara ya Mafuta (OMCs).
"Hata hivyo, mafuta hayakukidhi mahitaji ya soko. Kutokana na upungufu huo, OMCs waliruhusiwa kuagiza mafuta safi kutoka nje ya nchi kufidia upungufu kulingana na mahitaji yao.
"Uagizaji wa mafuta kupitia OMCs uliratibiwa na Serikali kupitia Sekretarieti ya Kikosi Kazi cha Ufundi (Technical Task Force (TTF) Secretariat) chini ya Wizara ya Nishati na Madini."
Kipindi cha kuanzia Januari, 2000 anabainisha kuwa, Sera ya Soko Huria ilianza kutekelezwa rasmi ambapo OMC’s waliruhusiwa rasmi kuagiza mafuta popote katika soko la Dunia na kupanga bei za mafuta hayo nchini kwa kuzingatia misingi ya nguvu ya soko kwa maana ya ugavi na uhitaji (demand and supply).
Mulokozi anasema kuwa, katika kipindi hiki biashara ya mafuta iliachwa katika mikono ya kampuni binafsi bila kuwa na usimamizi wa serikali.
Changamoto zilizojitokeza
Mtendaji Mkuu huyo amebainisha kuwa,pamoja na ongezeko la uwekezaji kwenye sekta lililotokana na sera ya biashara huria, changamoto kadhaa ziliendelea kujitokeza.
Miongoni mwa changamoto hizo anazitaja kuwa ni kukosekana kwa sheria na kanuni thabiti ya kusimamia sekta ndogo ya mafuta katika kipindi hicho cha soko huria.
Pia, kutotekelezwa kwa Sheria ya Udhibiti wa Nishati na Maji ya Mwaka 2001 (Sura ya 414) na kuibuka kwa wimbi la uwekezaji ulio chini ya kiwango katika miundombinu ya mafuta katika mkondo wa chini.
Nyingine ni kuchakachua mafuta kwa kuchanganya mafuta ya taa na mafuta ya dizeli kwa sababu mafuta ya taa yalikuwa yanatozwa kodi ndogo kuliko dizeli na kuyauza kama dizeli.
"Changamoto nyingine ni kampuni za mafuta kuuza mafuta bei ya juu kwa kisingizio cha kupanda kwa bei za mafuta kwenye soko la dunia wakati wao wanakuwa na bakaa ya zamani ambayo ni ya bei ya chini.
"Hata hivyo pale ambapo bei ya mafuta ilikuwa inashuka waliendelea kuuza mafuta kwa bei ya juu, na waagizaji wa mafuta kuweka gharama kubwa za uagizaji (premium) ambazo zilikuwa hazina uhalisia wa bei halisi katika soko/
"Aidha,mafuta yalikuwa yanaletwa nchini kwa shenena ndogo ndogo za tani 5,000 hadi tani 10,000 hivyo kusababisha mrundikano wa meli zinazosubiri kupakua mafuta. Meli zilikuwa zinasubiria kati ya siku 30 mpaka 60."
Amesema, pia kulikuwa na gharama kubwa za demurrage ambapo wastani wa gharama za demurrage zilifikia Dola za Marekani 45 kwa tani.
Mbali na hayo, anafafanua kuwa, viliibuka vitendo vya ukwepaji kodi kupitia udanganyifu wa kiasi na aina ya mafuta iliyotetwa pamoja na kuuza mafuta ya transit katika soko la ndani.
"Wamiliki wa hifadhi za mafuta waliweka bei kubwa za utunzaji wa mafuta zilizofikia hadi Dola za Marekani 20 kwa mita za ujazo kwa waliohitaji kutunziwa mafuta katika hifadhi hizo na kukosekana uratibu thabiti kwa wadau muhimu wa sekta ndogo ya mafuta."
Amewataja wadau hao kuwa ni Mamlaka ya Maoato Tanzania (TRA), Makampuni ya Uagizaji wa Mafuta (OMC), Shirika la Viwango nchini (TBS), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA), walaji, wauzaji rejareja, watoa huduma kwenye sekta na wengineo.
Utatuzi
Mulokozi anasema, kutokana na changamoto zilizojitokeza baada ya kuanza kwa soko huria katika biashara ya mafuta, Serikali ilianzisha mifumo mbalimbali ili kuzitatua.
Hatua zilizochukuliwa na Serikali ni kuanzishwa kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji nchini (EWURA),kutunga Sheria ya Petroli, kuanza kupanga bei za mafuta, kuanzisha kwa Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja, kuongeza kodi katika mafuta ya taa na uanzisha kwa utaratibu wa kuweka vinasaba katika mafuta.
Mfumo wa BPS
Mtendaji Mkuu huyo akizumgumzia kuhusu kuanzishwa kwa Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja Bulk Procurement System-BPS) anasema,Sheria ya Petroli ya mwaka 2008 iliekeleza kuwa mafuta yote yatakayotumika nchini lazima manunuzi yake yafanyike kwa ufanisi (Efficient Procurement of Petroleum Products).
Aidha, sheria hiyo imeweka hiari kwa mafuta ya transit kutumia mfumo huu au njia nyingine binafsi. "Hata hivyo kutokana na ufanisi mzuri wa mfumo zaidi ya asilimia 95 ya mafuta ya transit huagizwa kupitia BPS.
"Ili kuhakikisha kwamba ununuzi wa mafuta unafanyika kwa ufanisi, Serikali kupitia iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini iliandaa Kanuni za Kusimamia Ununuzi wa Mafuta kwa Pamoja (Petroleum (Bulk Procurement) Regulation-2011);
Mulokozi anafafanua kuwa, BPS ni mfumo wa usimamizi wa uagizaji wa bidhaa za mafuta ya petroli kwa pamoja (Bulk Importation) ambapo ulianzishwa ili kutatua changamoto mbalimbali.
Anazitaja changamoto ambazo zinatatuliwa na mfumo huo kuwa ni kampuni za mafuta kuuza mafuta bei ya juu kwa kisingizio cha kupanda kwa bei za mafuta kwenye soko la dunia, waagizaji wa mafuta kuweka gharama kubwa za uagizaji.
Nyingine ni kuoandoa changamoto ya mafuta kuletwa nchini kwa shehena ndogo ndogo za kati ya tani 5,000 hadi tani 10,000 hivyo kusababisha mrundikano wa meli zinazosubiri kupakua mafuta kwa muda mrefu.
Pia, kuondoa gharama kubwa za demurrage ambapo wastani wa gharama za demurrage zilikuwa Dola za Marekani 45 kwa tani na kudhibiti vitendo vya ukwepaji kodi kupitia udanganyifu wa kiasi na aina ya mafuta iliyoletwa pamoja na kuuza mafuta ya transit katika soko la ndani.
Kampuni ya PICL
Mtendaji Mkuu huyo amefafanua kuwa, katika utekelezaji wa Sheria ya Petroli, Kanuni ya Petroleum (Bulk Procurement System) Regulation ya Mwaka 2011 ilitungwa na hivyo kuruhusu kuanza kwa Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (Bulk Procurement System-BPS).
BPS ilianza kuratibiwa na Petroleum Importation Coordinator Ltd (PICL) ambayo ilikuwa kampuni binafsi isiyo na mtaji (private entity limited by guarantee with no share capital) ambapo wanahisa wa kampuni hiyo walikuwa OMCs.
Kwa kipindi ambacho BPS ilikuwa chini ya PICL, Mulokozi anasema, kuna mafanikio kadhaa yalipatikana katika sekta ya mafuta ikiwa ni pamoja na kupungua kwa gharama za meli kusubiri kushusha mafuta (demurrage costs) na hivyo kuleta unafuu wa bei kwa walaji wa mwisho.
Hata hivyo, anasema PICL ilikumbana na changamoto za msingi katika kuratibu mfumo wa BPS zikiwemo za kiutawala, kwani serikali iliweka wajumbe watatu kwenye Bodi ya PICL ikiwa ni pamoja na Mwenyekiti kutoka serikalini.
Lengo la kufanya hivyo,lilikuwa ni kulinda maslahi ya Taifa, ambapo hii ilikuwa kinyume na taratibu za uendeshaji wa kampuni binafsi.
Changamoto nyingine anasema, ni migongano ya maslahi kati ya wamiliki wa PICL (OMCs) na waletaji wa mafuta (Suppliers) kwani wengi wa waletaji mafuta walikuwa na uhusiano na OMCs.
Nyingine ni kufikia ukomo wa wanahisa (50) kulingana na sheria ya uanzishwaji wa kampuni binafsi na hivyo kuzinyima kampuni nyingine fursa ya kujiunga na PICL ili kuweza kuagiza mafuta kupitia mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja.
"Changamoto hizi, ziliuweka mfumo wa BPS katika hatari ya kushindwa au kuhujumiwa kwa maslahi binafsi, hali ambayo ingehatarisha uhakika wa upatikanaji wa mafuta nchini (security of supply)."
Ujio wa PBPA
Mtendaji Mkuu huyo amefafanua kuwa, katika kutafuta suluhisho la changamoto zilizoikabili PICL, wizara yenye dhamana kwa kushirikiana na wadau muhimu iliutafakari upya muundo wa chombo kitakachohusika na uratibu wa BPS.
Aidha,iliangalia uwezekano wa kuweka jukumu hilo kwenye moja ya taasisi zinazohusika na mafuta ikiwa ni pamoja na kuanzisha kitengo chini ya Wizara ya Nishati na Madini, kuanzisha kitengo chini ya TPDC au kuanzisha kitengo chini ya EWURA.
"Tathmini iliyofanyika ya kuweka BPS katika moja ya taasisi tatu tajwa hapo juu, ilibainisha uwepo wa mgongano wa kimaslahi kwa TPDC na EWURA kutokana majukumu yao kama yalivyoanishwa kwenye Sheria ya Petroli ya mwaka 2015 (Petroleum Act, 2015)."
Aidha, pamoja na changamoto za kiutendaji, ilibainika kuwa BPS kuratibiwa na wizara ingepelekea ugumu kwa EWURA kutekeleza majukumu yake ya udhibiti wa sekta.
"Hivyo kufuatia tathmini hiyo, ilionekana ni busara mfumo huo kusimamiwa na Serikali kupitia wakala. Kwa kuzingatia hilo mamlaka za Serikali ziliridhia kuanzishwa kwa wakala."
Mulokozi anasema, mwaka 2015 Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (Petroleum Bulk Procurement Agency-PBPA) ulianzishwa kwa Kanuni ya Wakala wa Serikali, ya mwaka 2015 kupitia Tangazo la Serikali Na. 423 la tarehe 25 Septemba 2015.
Kanuni hii iko chini ya Sheria ya Wakala wa Serikali (The Executive Agencies Act, Cap. 245); ndipo PBPA ikachukua majukumu ya iliyokuwa PICL na kuanza kusimamia mfumo wa BPS kuanzia Januari 2016.
Anasema,Kanuni na Agizo la Serikali la kuanzisha PBPA limeainisha majukumu ya jumla ya taasisi hiyo ambayo ni kusimamia mfumo wa Uagizaji wa Pamoja wa Mafuta nchini na kuhakikisha mafuta yanaletwa kwa njia yenye ufanisi na kwa wakati ili kukidhi mahitaji ya nchi wakati wote.
Mtendaji Mkuu huyo anasema,majukumu ya msingi ya wakala ni kusimamia Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (BPS), kukusanya mahitaji ya mafuta na kutangaza zabuni kwa ajili ya kuleta mafuta nchini.
Pia, kusimamia mikataba ya uagizaji mafuta na kuhakikisha mafuta yaliyoagizwa yanafika nchini kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa kulingana mikataba husika.
Jukumu lingine ni kuhakikisha mafuta ya kutosha yanakuwepo nchini wakati wote na kusimamia taratibu za uagizaji zenye ufanisi katika kuleta mafuta nchini.
Taratibu hizo, Mulokozi anasema hujumuisha usajili wa Kampuni za Biashara ya Jumla ya Mafuta nchini (OMCs), usajili wa Wazabuni (Prequalification of Suppliers, upokeaji wa mahitaji ya mafuta kutoka kwa OMCs, uchakataji wa mahitaji yaliyopokelewa, utangazaji na ufunguzi wa zabuni za kiushindani wa Kimataifa.
Vile vile, PBPA inahusika na usimamizi wa utekelezaji wa mikataba, kupanga ratiba za meli zinazoleta shehena za mafuta na kutunza taarifa za meli zilizoleta mafuta.
Leseni
Anasema ili kampuni za biashara ya mafuta (OMCs) ziweze kushiriki kwenye mfumo zinapaswa kupata leseni ya EWURA ya biashara ya jumla ya mafuta, leseni ya TRA ya biashara ya jumla ya mafuta na kusajiliwa na wakala kama muagizaji mafuta kupitia mfumo.
Sambamba na kuwasilisha kwa wakala bank guarantee yenye thamani ya asilimia tano ya wastani wa uagizaji mafuta.
Mtendaji Mkuu huyo wa PBPA anasema kuwa, hadi kufikia Novemba 2023 kuna jumla ya OMCs 59 waliojisajiliwa na wakala nchini.
Akizungumzia kuhusu utaratibu wa kuwapata waletaji mafuta (Suppliers Prequalification) anasema, hufanyika kwa kuzingatia Kanuni za Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja za mwaka 2017 na miongozo ya Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja ya mwaka 2020.
Mulokozi anafafanua kuwa,kampuni zinazoshiriki katika zabuni za BPS hupatikana kwa kuleta maombi ya kuwekwa katika orodha ya wazabuni (Prequalified Suppliers).
"Maombi hayo hufanyiwa tathmini, kampuni zinazokidhi vigezo huingizwa katika Orodha ya Wazabuni waliosajiliwa (Prequalified Suppliers) baada ya kufanyiwa Uhakiki wa Kina (Due Diligence)."
Vigezo vinavyotumika kusajili Wazabuni kwenye orodha ya wazabuni anasema ni pamoja na kampuni yenye nia kuwasilisha barua ya maombi, uthibitisho kuwa imesajiliwa na chombo chenye dhamana ya usajili katika nchi yake.
"Na taarifa za kifedha zilizokaguliwa kwa miaka mitatu ya karibuni zinazoonyesha mapato yasiyopungua Dola za Marekani milioni 100 kwa mwaka kwa kampuni za nje mali (Asset base) zenye thamani ya shilingi za Ki-Tanzania bilioni 30 kwa kampuni za ndani."
Nyingine ni taarifa za kampuni zikionyesha ujuzi na uwezo wa wafanyakazi wa kampuni husika ikiwemo maelezo yanayoonyesha chanzo cha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuleta mafuta nchini
iwapo kampuni husika itashinda zabuni.
Pia, amesema nyingine ni cheti cha uhakiki wa kampuni kuwa hakuna tishio linaloweza kuathiri uwezo wa kampuni husika kushindwa kutekeleza mikataba kwenye Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja.
Vigezo vingine ni uthibitisho wa kutokuwa katika mazingira ya kufilisika au kufunga shughuli za kampuni na kitambulisho au cheti cha ulipaji kodi.
Mtendaji Mkuu huyo anasema, utaratibu wa kutangaza na kufungua zabuni za BPS umeanishwa katika Petroleum Bulk Procurement Implementation Manual.
"PBPA hutoa tangazo la zabuni za mafuta kwenda kwa Prequalified Suppliers, siku kumi kabla ya tarehe ya kufungua zabuni.
"Utaratibu unaotumika katika ufunguaji wa zabuni shindanishi za kimataifa ni wa wazi ambapo Wazabuni na OMCs hualikwa kushuhudia hatua ya ufunguzi hadi upatikanaji wa mshindi.Aidha, zoezi lote la ufunguzi wa zabuni huwekwa katika kumbukumbu ya picha na video."
Kuhusu taratibu za upokeaji wa mahitaji ya mafuta na utangazaji wa zabuni, Mulokozi anasema,
PBPA hupokea mahitaji ya mafuta ya mwezi kwa matumizi ya ndani na nje ya nchi kutoka kwa OMCs
Anasema, mahitaji ya mafuta yaliyopokelewa hugawanywa katika viwango vidogo kulingana na ukubwa wa meli kwa kuzingatia uwezo wa miundombinu ya upakuaji wa mafuta katika bandari zetu.
"Kwa wastani mahitaji ya mafuta kwa mwezi hugawanywa katika meli 7 hadi 12, kwa kuzingatia mahitaji hayo nyaraka za zabuni huandaliwa na kutangazwa kwa Prequalified Suppliers."
Gharama na ushindanishi katika zabuni za Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja, Mulokozi anasema, wazabuni hushindanishwa katika gharama za uletaji mafuta ambazo hujumuisha gharama za usafiri, bima, mikopo (financing cost), bandari, taasisi, uendeshaji na faida kwa mzabuni.
Anasema, gharama halisi za mafuta (FOB) ni wastani wa bei za mafuta katika soko la dunia kwa mwezi mmoja kabla ya mwezi wa kuwasili shehena husika (M-1) ambapo wakati wa kufungua zabuni husika gharama hizo hazijulikani.
"Wastani wa bei katika soko la dunia hupatikana kutoka katika bei zinazotangazwa kwa soko la Arab Gulf katika mtandao wa PLATTS unaomilikiwa na kampuni ya S&P GLOBAL.Gharama za mafuta huwekwa katika Dola za Marekani ingawaje ulipiaji unaweza kufanyika katika aina nyingine ya fedha kwa makubaliano na mshindi wa zabuni,"
Uletaji mafuta
Mtendaji Mkuu huyo anasema kuwa, mshindi wa zabuni (Supplier) hufuata taratibu za mkataba za kufikisha mafuta nchini katika muda husika.
Pia, mafuta yote yanayoletwa nchini yanatakiwa kukidhi viwango vya ubora kama vilivyotangazwa na TBS.
"Na mshindi wa zabuni (Supplier) anatakiwa kuwasilisha nakala za nyaraka za shehena ya mafuta kwa Kampuni za Bishara ya Mafuta (OMCs) siku 10 kabla ya meli kuwasili nchini. Nyaraka zinazowasiliwa ni Ankara kifani (Profoma invoice),Endorsed bill of lading, Load port Certificate of Quality na Certificate of Origin."
Manufaa
Mulokozi anasema, kuna manufaa mengi yaliyopatikana kutokana na kuanzishwa kwa Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (BPS) ikiwemo uhakika wa upatikanaji wa mafuta yanayotosheleza mahitaji ya nchi na yenye viwango vya ubora unaotakiwa wakati wote.
"Pia kuna unafuu wa gharama za uletaji wa mafuta kutokana na uagizaji wa pamoja (economies of scale) kwa wastani zaidi ya Dola za Marekani milioni 200 sawa na shilingi bilioni 500 huokolewa kila mwaka kupitia mfumo wa BPS."
Manufaa mengine ni kupungua kwa bei ya mafuta kutokana na uagizaji wenye ufanisi, kuongezeka kwa mapato ya kikodi yatokanayo na bidhaa ya mafuta.
Aidha, mfumo umewezesha kupunguza vitendo vya ukwepaji kodi kutokana na udanganyifu uliokuwa unafanywa na baadhi ya OMCs nakKuthibiti udanganyifu katika gharama za mafuta katika soko
la dunia na gharama za uletaji wa mafuta.
"Na kupunguza msongamano wa meli bandarini. Katika hili wastani wa Dola za Marekeni milioni 170 sawa na shilingi bilioni 425 huokolewa kila mwaka ikilinganishwa na gharama za demurrage zilizokuwa zikilipwa kabla ya mfumo wa BPS.
"Mfumo kutumika na nchi jirani katika ununuzi wa mafuta kwa nchi hizo, hivyo kuipatia serikali mapato kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya bandari.
"Kwa sasa uagizaji wa mafuta kwa ajili ya nchi jirani umefikia wastani wa asilimia 55 ya kiwango cha mafuta kinachoagizwa kupitia BPS kutoka wastani wa asilimia 33 za awali."
Nyingine amesema ni kupungua kwa upotevu wa mafuta wakati kwa kupakua mafuta kutoka melini ambapo wastani wa tani 1100 (sawa na lita 1,300,000) huokolewa kila mwezi, sawa na takriban shilingi bilioni 4.16 kwa bei kikomo za Disemba 2023. Hivyo kwa mwaka takribani shilingi bilioni 49.9 huokolewa.
Maghala
Anasema, Tanzania ina maghala 22 yenye uwezo wa kupokea mafuta kutoka kwenye meli katika Bahari ya Hindi.
"Maghala hayo 22 yana uwezo wa kupokea jumla ya takribani lita bilioni 1.31 kwa aina nne za mafuta ya petroli ikiwemo dizeli, petroli, mafuta ya ndege na mafuta ya taa."
Vile vile anafafanua kuwa, magahala hayo yamegawanyika Dar es Salaam upande wa Kurasini ina jumla ya maghala 11 yenye uwezo wa kupokea takriban jumla ya lita milioni 570.
Dar es Salaam upande wa Kigamboni ina jumla ya maghala nane yenye uwezo wa kupokea jumla ya takribani lita milioni 522 huku Mtwara ina maghala mawili yenye uwezo wa kupokea jumla ya takribani lita milioni 35.
Kwa upande wa Bandari ya Tanga, Mtendaji Mkuu huyo anasema ina ghala moja lenye uwezo wa kupokea jumla ya takriban lita milioni 182.
Tathmini ya bei
Mulokozi anasema, katika Mikataba ya Uagizaji wa Mafuta nchini wakala hutumia tathmini ya bei ya soko inayofanywa Kampuni ya S&P Global ambayo ndiyo hutumiwa na nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika kupata tathmini ya bei ya mafuta katika soko la dunia.
Anasema, S&P Global ni kampuni pekee ya kutathmini bei ya soko la mafuta yenye ofisi duniani kote ikiwepo Afrika. Katika Bara la Afrika S&P Global wana ofisini nchini Afrika Kusini.
"Hivyo Kampuni zote zinazofanya biashara ya mafuta nchini na nchi jirani hutumia tathmini ya kampuni hii katika kujua bei za mafuta kwenye soko la dunia.
"Pia Kampuni mbalimbali zinazoendesha biashara au kutegemea kuwekeza katika soko la Afrika hutumia tathmini za S&P Global kupima kiwango cha mitaji ya uwekezaji wao."
Pamoja na mafanikio makubwa ya Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja,Mtendaji Mkuu huyo ansema zimekuwepo changamoto kadhaa katika uendeshaji wake.
Miongoni mwa changamoto hizo anasema, wakati wa kipindi cha janga la UVIKO-19 ambapo mahitaji ya mafuta yalipungua sana kutokana na kusimama shughuli nyingi za kiuchumi.
Hali hii ilipelekea meli kutumika kama hifadhi za mafuta, hivyo kusababisha uhaba wa meli na kufanya gharama za usafirishaji kuongezeka kwa kanuni ugavi na uhitaji (Supply and Demand). Aidha, katika kipindi hicho bei ya mafuta (FOB) ilishuka kwa kiwango kikubwa sana.
"Aidha, vita inayoendelea baina ya Urusi na Ukraine imesababisha bei ya mafuta (FOB) na gharama za kuyafikisha nchini (premium) kuongezeka kwa kiwango kikubwa.
"Hali hii imesababisha uhitaji mkubwa wa Dola za Marekani kuliko uwezo uliopo na kupelekea kiasi kikubwa cha mafuta kuwa kwenye financial hold na kusababisha gharama za kuleta mafuta kuongezeka."
Changamoto nyingine anasema, ni ongezeko la kiasi cha mafuta kinachoagizwa kutoendana na uwezo wa miundombinu ya upokeaji mafuta.
Miundombinu iliyopo imekuwa ikitumika toka kuanza kwa BPS wakati kiasi cha mafuta kilichokuwa kinaagizwa kwa mwezi ilikuwa ni wastani wa tani 200,000 hadi 250,000. Kwa sasa kiasi cha mafuta kinachoagizwa kwa mwezi ni wastani wa tani 450,000 – 600,000;
Pia, kutokuwepo kwa ghala kubwa la kupokelea mafuta kwa pamoja hivyo kupelekea meli kuchukua muda mrefu kupakua mafuta. Dar es Salaam pekee ina jumla ya maghala 19.
Utatuzi
Anasema, wakala kwa kupitia Wizara ya Nishati imekuwa ikishirikiana na Wizara ya Fedha pamoja na Benki Kuu ili kupunguza makali ya uhaba wa Dola za Marekani ambapo maamuzi kadhaa yamefanyika na kuleta unafuu.
"Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) imekanilisha taratibu za kumpata mkandarasi atayeboresha miundombinu ya upokeaji mafuta katika bandari ya Dar es Salaam. TPA inatarajia kusaini mkataba na mkandarasi huyo mwezi huu wa Disemba 2023."
Serikali
Mtendaji Mkuu huyo anasema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan imekuwa na mchango mkubwa katika Mfumo wa Uagizaji
Mafuta kwa Pamoja.
"Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha nishati ya mafuta inapatikana wakati wote na kwa bei nafuu. Katika kutekeleza hili Serikali ya Awamu ya Sita imefanya mambo mengi ikiwa ni pamoja na
"Serikali kutoa ruzuku kwenye gharama ya mafuta kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Julai 2022 hadi Disemba 2022 ili kupunguza bei ya mafuta kwa wananchi iwe stahimilivu. Hii ilifanyika baada ya athari ya bei ya mafuta kupanda sana katika soko la dunia kutokana na vita baina ya Urusi na Ukraine.
"Serikali kupitia Benki Kuu imekuwa ikitoa kiasi fulani cha Dola za Marekani kwa benki za biashara ili ziweze kulipia mafuta yanayotumika nchini.
"Serikali kupitia Benki Kuu ilibadilisha baadhi ya miongozo ya udhibiti wa Dola za Marekani ili kuwezesha benki za biashara kupata fedha hizo kutoka sokoni."
Mtendaji Mkuu huyo ansema, Serikali kupitia PBPA ilibadilisha mikataba ya uagizaji mafuta na kuruhusu matumizi ya fedha nyingine za kigeni katika ulipiaji mafuta yaliyoagizwa kwa ajili ya matumizi ya ndani ya nchi.
"Serikali kwa kupitia taasisi wadau imefanya mapitio ya nyaraka mbalimbali zinazosimamia Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja ili kuimarisha usimamizi wa Sekta Ndogo ya Mafuta.
"Serikali kupitia mamlaka zake imekuwa ikifanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maghala ya kuhifadhia mafuta ili kuhakikisha taratibu za uendeshaji wa maghala hayo zinazingatiwa."
Mulokozi amefafanua kuwa, Serikali imewezesha ushirikiano mzuri baina ya taasisi wadau katika Sekta ya Mafuta ili kuboresha ufanisi wa Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja.
Taasisi anazitaja kuwa ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), Wakala wa Vipimo nchini (WMA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na PBPA huku ikipokea maoni ya wadau mbalimbali kwa maboresho zaidi.
Tags
Habari
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)
Makala
Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja
Ofisi ya Msajili wa Hazina
Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA)