ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameelezea kuridhishwa kwake na uungwaji mkono kutoka kwa jumuiya mbalimbali nchini katika uongozi wake.
Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo wakati akizungumza kwa njia ya simu na Mheshimiwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Mohamed Mussa mara baada ya kupokea hundi yenye thamani ya shilingi 2,000,000 iliyotolewa na Jumuiya ya JUWASEZA kwa lengo la kumuunga mkono katika mbio za urais 2025.
Amesema,amefarijika kuona jumuiya hiyo inathamini jitihada zinazofanywa za kuwaletea maendeleo wananchi.
Aidha,ameahidi kuendelea na jitihada za kuimarisha Sekta ya Elimu kwa kushughulikia kwa karibu changamoto zinazoikabili sekta hiyo.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar,Mhe.Lela Muhammed Mussa amewataka walimu wakuu kusimamia utendaji wa majukumu katika skuli zao.
Amesema, walimu wakuu kuacha tabia ya muhali kwa walimu wao pale wanaposhindwa kuyatekeleza ipasavyo majukumu yao
Naye Mkuu wa Wilaya ya Micheweni, Bi.Mgeni Khatibu Yahya amesema kutokana na jitihada za Mh. Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi Micheweni imeweza kubadilika na kua ya kisasa na yenye maendeleo.
Aidha,amewataka walimu wakuu wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ili waweze kushiriki katika kufanya maamuzi.
Mkutano wa 11 wa JUWASEZA umefunguliwa rasmi ambapo mada mbalimbali zitajadiliwa katika mkutano huo.