Viongozi 2,686 Zanzibar wawasilisha Fomu za Tamko la Mali na Madeni

ZANZIBAR-Jumla ya viongozi 2,686 waliwasilisha Fomu za Tamko la Mali na Madeni ambayo ni sawa na asilimia 107 ya lengo lililopangiwa pamoja na orodha ya majina yote ya viongozi wa umma waliowasilisha taarifa zao.
Hayo yamesemwa huko Baraza la Wawakilishi Chukwani, nje kidogo ya Mji wa Zanzibar na Mhe. Mussa Fuom kwa niaba ya Mwenyekiti wa Tume Hiyo Assaa A. Rashid wakati alipokuwa akiwasilisha Ripoti ya Saba ya utekelezaji wa kazi za Tume ya Maadili ya viongozi wa umma mwaka 2022 -2023.

Alisema, katika mwaka 2022/2023 jumla ya viongozi 2,686 waliwasilisha fomu ya tamko la mali mapato na madeni sawa na asilimia 107 ya shabaha iliyopangwa.

Aidha,alifahamisha kuwa katika Gazeti la Serikali kupitia tangazo la Kisheria nambari 20 la mwaka 2023 ya utekelezaji, tume imewafanyia uhakiki viongozi 233 sawa na asilimia 117 ya lengo lililokusudiwa.

Alieleza,katika ripoti hiyo ya saba ya utekelezaji wa kazi za Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma inaelezea kazi za tume kwa mwaka 2022/2023 zilizofanywa kwa kuzingatia mpango kazi.

Hata hivyo, mipango mikuu ya Kitaifa ikijumuisha Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050, Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar kwa 2021-2026 na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025.

Amesema,Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Namba 4 ya 2015 imeweka utaratibu wa utayarishaji na uwasilishaji wa Ripoti ya Utekelezaji wa Kazi za Tume ya Maadili kwa mujibu wa kifungu cha 29 cha sheria hiyo.

Alifahamisha ndani ya kipindi cha miezi mitatu baada ya mwisho wa mwaka wa fedha kumalizika kutoa Ripoti ya mwaka wa utekelezaji wa kazi za tume inatakiwa kuwasilishwa kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ripoti hiyo, kupitia kwa Waziri anayehusika na masuala ya Maadili na huwasilishwa mbele ya Baraza la Wawakilishi katika kikao kinachofuata.

Alisema, katika kipindi cha miaka saba tokea kuanzishwa kwake Aprili 2016, Tume ya Maadili imeweza kuwasilisha kwa wakati Ripoti za Utekelezaji wa Kazi zake kwa kila mwaka.

“Hupokelewa kupitia Fomu ya Tamko la Mali na Madeni ambapo husajiliwa na kufanyiwa uhakiki ili kuthibitisha usahihi wake,”amesema Mhe.Mussa.

Kwa upande mwengine alieleza kuwa, tume imepewa jukumu la kupokea malalamiko au tuhuma za ukiukwaji wa maadili dhidi ya viongozi wa umma ambapo tume hulazimika kufanya uchunguzi kuhusu malalamiko na kutoa maamuzi katika juhudi za kukuza uelewa wa masuala ya maadili.

Pamoja na hayo alisema, katika kipindi hiki cha utekelezaji, tume imeendelea kuimarisha Mfumo wa Kieletroniki wa Usajili wa taarifa za Mali na Madeni ambao matumizi yake yamerahisisha kazi ya upokeaji wa fomu na upatikanaji wa ripoti muhimu zinazotumika katika kuisaidia tume kutekeleza majukumu yake ya kila siku.

Lengo ni kuhakikisha kuwa taarifa katika mfumo zinaendelea kuwa salama.

Alisema, tume imeimarisha usiri wa taarifa zinazohifadhiwa katika mfumo kwa kuongeza“server” yenye uwezo mkubwa ikiwa ni hatua ya mkakati wa kukabiliana changamoto.

Sambamba na hayo pia tume inategemea kuanza maandalizi ya kupokea
Fomu kupitia Mfumo wa Kielektroniki kwa kuanzia huduma hiyo imepangwa kupatikana kwa viongozi ambao taasisi zao zimeunganishwa katika Mkonga wa Taifa.

“Hatua hii itaongeza ufanisi na kutoa fursa kwa viongozi kuingiza taarifa zao za mali, mapato na madeni, kidogo kidogo bila ya kusubiri kipindi cha mwisho wa mwaka," amesema Mheshimiwa Mussa.

Kwa upande wa malalamiko au madai yanayohusiana na uvunjwaji wa maadili jumla ya malalamiko 19 yamepokelewa na kufanyiwa kazi sawa na asilimia 95 ya shabaha iliyokadiriwa.

Kwa upande wa maeneo ambayo yamelalamikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya madaraka, unyanyasaji, uonevu,lugha za matusi na moja kutelekeza familia katika hatua tofauti za kufanyiwa kazi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news