Vita dhidi ya dawa za kulevya nchini yashika kasi, DCEA yapewa kongole

NA GODFREY NNKO

KAMATI ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam imeipongeza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kutokana na kazi nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha kuwa, dawa za kulevya nchini zinadhibitiwa ili kuokoa kizazi cha sasa na kijacho nchini.
Pongezi hizo zimetolewa Desemba 28,2023 na Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert Chalamila baada ya kufika ofisi ya mamlaka hiyo akiwa ameambatana na kamati yake.

“Siku chache zilizopita mmeona wamekamata dawa za kulevya si chini ya tani tatu, ambapo dawa hizi za kulevya zilipaswa kusambazwa katika Mkoa wa Dar es Salaam na pengine nchi nzima,Kamishna Jenerali wa mamlaka hii, yeye pamoja na watumishi wote, Kamishna Jenerali Lyimo amedhibiti mtandao huo na kuwakamata watu wanaohusika na dawa hizo.

“Hii ni operesheni endelevu katika mkoa wetu wa Dar es Salaam ambao ndiyo lango kubwa la karibu kila kitu, kibiashara, kidplomasia, kiuchumi na hata uwekezaji mwingine mwingi wa kimkakati.

“Lakini, pia siku chache zilizopita mliona operesheni kubwa ambayo waliifanya ambapo pia, walikamata baadhi ya viwanda vikitengeneza biskuti ambapo zile biskuti zilikuwa zina mchanganyiko wa dawa za kulevya.

“Tumeona, sisi…mimi Mkuu wa Mkoa na wenzangu ambayo ni Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam tufike hapa kwenye ofisi hizi, tuwape neno la pongezi na waendelee kwa kasi kubwa na kazi kubwa wanayoendelea kuifanya kwa maslahi mapana ya maendeleo ya Taifa letu.

“Kamishna Jenerali amenieleza na kunithibitishia kwamba hakuna mtu yeyote atakayeonewa na kwamba kila mmoja atakayekamatwa atakamatwa kwa ushaidi wa yeye kuhusika au yeye kuwa mnunuzi, au yeye kuwa muuzaji wa dawa za kulevya,”amefafanua Mwenyekiti wa Kamati hiyo, RC Chalamila.
Pongezi hizo zinakuja ikiwa ni siku moja imepita baada ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) kutangaza kuwa, imekamata zaidi ya kilo 3,182 (tani 3.182) za dawa za kulevya aina ya Heroin na Metamphetamine.

Hayo yalisemwa Desemba 27,2023 na Kamishna Jenerali wa Mamlaka hiyo,Aretas Lyimo wakati akizungumza na wanahabari ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Alisema, ukatamataji huo mkubwa wa dawa ambazo hazijawahi kukamatwa hapa nchini umetokana na operesheni kubwa iliyofanyika jijini Dar es Salaam na mkoani Iringa.

Operesheni hiyo ilifanyika Desemba 5 hadi 23,2023 huku watu saba wakikamatwa ambapo kati yao wawili ni raia kutoka Asia.

Kamishna Jenerali alisema kuwa, dawa hizo zingefanikiwa kuingia mitaani zingeleta madhara kwa watu zaidi ya milioni 70 kutoka ndani na nje ya nchi.

“Ukamataji huu umehusisha kiasi kikubwa cha dawa za kulevya ambacho hakijawahi kukamatwa katika historia ya Tanzania tangu kuanza kwa shughuli za udhibiti wa dawa za kulevya.
"Hivyo, watuhumiwa waliokamatwa ni miongoni mwa mitandao mikubwa ya wauzaji wa dawa za kulevya inayofuatiliwa nchini na duniani.

"Kiasi cha dawa zilizokamatwa, endapo zingefanikiwa kuingia mtaani zingeweza kuathiri zaidi ya watu 76,368,000 kwa siku.

“Ukamataji huu umeokoa nguvu kazi ambayo ingeangamia kutokana na madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi,"alifafanua Kamishna Jenerali Lyimo.

Vile vile alisema, kiasi hicho cha dawa za kulevya kinajumuisha kilo 2,180.29 za dawa aina ya Methamphetamine na kilo 1,001.71 aina ya Heroin zilizokamatwa katika Wilaya ya Kigamboni, Ubungo na Kinondoni jijini Dar es Salaam pamoja na Wilaya ya Iringa mkoani Iringa.

Kamishna Jenerali Lyimo alisema kuwa, aina ya dawa ambazo wamezikamata zilikuwa zimefungashwa kwenye vifungashio vya bidhaa zenye chapa mbalimbali za majani ya chai na kahawa.
Mbali na hayo, Kamishna Jenerali Lyimo akizungumza na kamati hiyo, ameishukuru kwa kuwatia moyo na kuwapa nguvu ya kusonga mbele katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini.

“Ninakushukuru sana Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, pamoja na Kamati yako ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuja kutusapoti, kututia moyo, kutupa nguvu na sisi tumefarijika sana kuja kwako hapa.

“Na, tutaendelea kuifanya hii operesheni kwa nguvu zote kwa kushirikiana na kamati yako ya usalama kupitia Jeshi la Polisi na ninaamini kabisa, sasa hivi jijini Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla wauzaji wote wa dawa za kulevya, watumiaji wa dawa za kulevya huu sio wakati wao, ni bora wakaacha na wakaenda kufanya shughuli nyingine, na sio dawa za kulevya.

“Kwa hiyo, niwahakikishie Watanzania, tutahakikisha tunafanya hii kazi kwa uzalendo mkubwa ambayo tumeaminiwa na Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tutaifanya kwa umakini kwa kuhakikisha kwamba kila anayefanya biashara ya dawa za kulevya anakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria,”amefafanua Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo.

Wakati huo huo, Serikali imesema kuwa, itahakikisha dawa zote za kulevya zinazouzwa mitaani na vijiweni zinadhibitiwa ili kuwezesha Taifa na kizazi cha sasa na kijacho kuwa salama nchini.

Akizungumzia kuhusiana na miakakati waliyonayo ya kuhakikisha dawa za kulevya zinadhibitiwa ndani na nje ya Jiji la Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salam, Muliro Jumanne Muliro amesema,

“Vita ya dawa za kulevya ni vita kubwa ambayo sisi Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, lazima tuwaunge mkono ndugu zetu, maafisa wasimamizi wa sheria wanaotoka kwenye Mamlaka ya Dawa za Kulevya.

“Unachotufanyia na timu yako ni kukata mashina, mnachimba mizizi, mnakata mashina. Mimi nikuahidi, matawi yaliyopo kwenye mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, kwa kushirikiana na wenzagu ambao ni wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama ambao umewaona, sisi tunafanya kazi kwa pamoja, tutafanya kazi kubwa ya ziada.

….tutafanya kazi kubwa ya ziada kuhakikisha jambo hili la dawa za kulevya, kama ambavyo umetuongoza kuweka historia ya kukamata dawa nyingi, na sisi tunataka tuweke historia ya kuvunjavunja vijiwe vyote ambavyo vimekuwa ni maskani wakati mwingine wa kutumia dawa za kulevya. Kama sehemu ya sisi kukuunga mkono kwenye jitihada zako,”amefafanua kwa kina Kamanda Muliro.

Biskuti za bangi

Novemba, mwaka huu DCEA ilithibitisha kuwakamata watu mbalimbali wanaojihusisha na utengenezaji wa biskuti zilizochanganywa na bangi iliyosindikwa maarufu kama Skanka katika eneo la Kawe jijini Dar es Salaam.

Kamishna Jenerali, Aretas Lyimo alisema, watu hao walikamatwa baada ya kukutwa wakiendelea na uzalishaji wa biskuti hizo kwa kutumia mtambo mdogo wa kusaga Skankana vifaa vya kutengeneza biskuti za bangi.
Aidha, katika hatua nyingine mamlaka hiyo, ilibainisha kukamata bangi isiyosindikwa kilo 423.54 katika oparesheni maalum zilizofanyika hivi karibuni kwenye mipaka na fukwe za Bahari ya Hindi.

Kamishna Jenerali Lyimo alisema, kilo 158.54 zilikamatwa eneo la Kigamboni na Kawe, zilizokuwa zimehifadhiwa ndani ya mabegi ya nguo tayari kwa ajili ya kusafirishwa.

Huku kilo 265 zikiwa zilikatatwa katika matukio tofauti katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, zikiwa zimefichwa ndani ya magari huku zikichanganywa na bidhaa nyingine ikiwemo maboksi yenye matunda aina ya Apples’zikisafirishawa kuingia Dar es Salaam.
“Kutokana na jitihada ambazo mamlaka imeendelea kupambana na masuala ya dawa za kulevya na bangi, tumefanikiwa kukamata kilogramu 423.54 za bangi iliyosindikwa maarufu kama Skanka katika oparesheni maalumu zilizofanyika kwenye mipaka na fukwe za Bahari ya Hindi,” amesema.

Vile vile, Kamishna Jenerali Lyimo alitoa wito kwa wananchi hususani wanafunzi kuwa makini na vyakula wanavyovutumia na kuacha kufuata mikumbo isiyofaa ikiwemo kutumia vilevi na vitu wasivyovijua hali ambayo inaweza kuwaingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya.
Alisema, mamlaka hiyo imebaini kuwepo kwa watu wasiowaaminifu kwa kuchanganya Skanka kwenye vyakula kama Biskuti, Keki, Jamu, Sharubati, Tomato Sauce, pia kwenye sigara na shisha.

Kamishna Jenerali Lyimo alieleza kuwa, lengo la kufanya hivyo ni kurahisisha uuzaji wa dawa hizo kwa kificho na kuongeza idadi ya watumiaji wa dawa za kulevya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news