NA HAPPINESS SHAYO
WAHITIMU wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) wametakiwa kuleta mageuzi katika utoaji huduma bora kwa watalii na wageni wanaotembelea nchini ili kuitangaza vyema Tanzania na kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini.
Hayo yamesemwa leo Desemba 12, 2023 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) kwenye mahafali ya 21 ya Chuo cha Taifa cha Utalii yaliyofanyika katika Ukumbi wa JNICC, jijini Dar es Salaam.
”Ninyi ambao mmepikwa katika Chuo bora cha utalii na ukarimu nchini nategemea mkalete mageuzi katika huduma mtakazotoa kwa watalii na wageni kwa ujumla, ili watalii na wageni wanaotembelea nchini wapate huduma kulingana na thamani ya fedha yao na pia washawishike kurejea nchini na kuitangaza Tanzania kwa ndugu na jamaa zao,” Mhe. Kairuki amesisitiza.

Amesema kwa kufanya hivyo watakuwa wamewezesha na kuongeza mchango wa Sekta ya Utalii katika Pato la Taifa sambamba na kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuitangaza Tanzania Kimataifa na kushawishi ongezeko kubwa la watalii kupitia Programu ya "Tanzania- the Royal Tour".
Aidha, amewasihi wahitimu hao kujiendeleza kielimu na kiujuzi ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia kwani Sekta ya Utalii na ukarimu inakua kwa kasi sana.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kairuki ametoa wito kwa wadau wa Sekta ya Utalii nchini kutumia huduma za Chuo hicho ili kuendelea kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na Chuo lakini pia kukiwezesha Chuo kuongeza mapato yake ya ndani ili kuendelea kuboresha na kuimarisha mafunzo ya nadharia na vitendo kwa kukidhi gharama za uendeshaji wa mafunzo hayo.

Naye, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Dkt. Florian Mtey amesema kuwa Chuo cha Taifa cha Utalii ni miongoni mwa vyuo vilivyo mstari wa mbele katika kuhakikisha ndoto ya Serikali ya kuongeza idadi ya watalii kufikia milioni 5 ifikapo 2025 na pia kuongeza idadi ya watoa huduma wenye ujuzi na weledi stahiki inatimia.

Chuo cha Taifa cha Utalii ni wakala ulio chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii wenye dhamana ya kutoa mafunzo, kutoa huduma ya Ushauri na kufanya tafiti katika fani ya ukarimu na utalii.