NA GODFREY NNKO
WANAWAKE barani Afrika wametakiwa kushiriki katika biashara ikiwemo kutumia fursa mbalimbali za masoko zilizopo barani humo kwa ustawi bora wa biashara zao.
Hayo yamebainishwa Desemba 8, 2023 na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman wakati akifunga Kongamano la Eneo Huru la Biashara barani Afrika (AfCFTA) la Wanawake katika Biashara 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Amesema, katika siku tatu za kongamano hilo wanawake wamepata fursa ya kujadili, kuelimishana na kupeana mbinu zitakazoongeza ushiriki wao katika biashara ndani ya Eneo Huru la Biashara Afrika.
Mheshimiwa Othman amesema, fursa za masoko zilizopo kwa sasa zinahitaji ushiriki wa wanawake ili kujikwamua kiuchumi na pia kukuza biashara zao kupitia masoko ya nchi mbalimbali.
"Nitoe wito kwa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara barani Afrika kufanikisha makongamano haya kila mwaka, na niwahimize wadau wote kuendeleza moyo wa kushiriki kikamilifu katika mikusanyiko hii.
"Ili kuendelea kutoa msukumo wa makusudi utakaowezesha kufikia malengo ya ushiriki thabiti wa wanawake katika biahara na kwa ajili ua maendeleo ya bara lote la Afrika."
Vile vile amesema,dhima ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt,Samia Suluhu Hassan ni kuona wanawake wanashiriki kwenye biashara na hivyo kuwataka wanawake kuongeza ushiriki wao kwenye eneo hilo ili kumuunga mkono.
Mheshimiwa Othman ameeleza kuwa, kukiwa na nia thabiti ya utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa kutatoa hamasa kwa nchi rafiki na washirika wa maendeleo kwa kushirikiana na Bara la Afrika ili kufikia lengo la kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia ushiriki wao katika biashara ndani ya AfCTA.
“Ni matumaini yangu kwamba maazimio ya kongamano hili yatakuwa chachu ya kuandaa na kutekeleza Ajenda ya Dkt.Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kinara wa uhamasishaji wa ushiriki wa wanawake katika biashara ndani ya Eneo Huru la Biashara barani Afrika,”amesema Mheshimiwa Othman.
Pia, amesema utekelezaji wa maazimio ya kongamano hilo utaimarisha azma ya Afrika ya kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika kunufaika na Eneo Huru la Biashara barani Afrika.
Amesema, kupitia kongamano hilo la siku tatu ambalo lilianza Desemba 6 hadi 8, 2023 kwa kuwakutanisha wanawake kutoka mataifa 54 barani Afrika kupitia mijadala ya washiriki wamebainisha umuhimu wa mataifa ya Afrika kuharakisha uwekaji wa mazingira bora ya kuwezesha ushiriki thabiti wa wanawake katika biashara.
Lengo likiwa ni kuzalisha ajira nyingi na bora. "Na hatimaye kuyafikia maendeleo endelevu. Aidha, kongamano limetoa mwelekeo wa hatua zinazopaswa kuchukuliwa na nchi za Afrika ili kuwa na mabadiliko ya haraka ya kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika biashara ndani ya Eneo Huru la Biashara baranin Afrika."
Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Mhe. Riziki Pembe Juma amewataka wanawake nchini kuongeza kasi ya kuzalisha na kutafuta masoko ya ndani ya Bara la Afrika ili kukuza wigo wa biashara zao.
Mheshimiwa Pembe amesema kuwa,Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) ni eneo moja lenye kutoa fursa kwa wanawake kuuza bidhaa zao kwenye masoko ya Afrika bila kutozwa ushuru.
Wakati huo huo, amezipongeza Serikali zote mbili ikiwemo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara za Viwanda na Biashara, Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara barani Afrika, kamati ya maandalizi na wote waliohusika kufanikisha kongamano hilo kwa ufanisi.
"Mheshimiwa mgeni rasmi nipende kuwapa moyo wanawake wafanyabiashara ambao wamepata fursa ya kushiriki kongamano hili, wengine kwa mara yao ya kwanza, wengine kwa mara ya pili. Lakini, hata wale ambao hawakupata nafasi ya kushiriki katika kongamano hili tuendelee kuongeza kasi ya kuzalisha na kutafuta masoko ya ndani, na nje ya Tanzania.
"Lakini, soko letu la Afrika na ikiwezekana pia masoko nje ya bara letu la Afrika,katika siku hizi tatu za kongamano, mawasilisho mbalimbali na mijadala mbalimbali ilitolewa na imebainisha fursa za changamoto zinazowakabili wanawake kwenye Eneo Huru la Biashara barani Afrika.
"Kwa ajili ya kupeana uzoefu na kubainisha njia na mikakati ya kuzitatua kupitia Serikali na taasisi zake, washirika wa maendeleo pamoja na taasisi za fedha katika nchi wanachama wa Umoja wa Afrika."
Desemba 6, 2023 wakati akifungoa kongamano hilo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema, kufanyika kwa kongamano hilo kwa mara ya pili ni ishara tosha ya kuonesha dhamira ya nchi washiriki wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika kukuza ushiriki wa wanawake katika biashara chini ya eneo hilo.
“Kufanyika kwa makongamano haya kunatoa nafasi muhimu kwa wadau mbalimbali wa kuwawezesha wanawake kujadiliana na kutafuta ufumbuzi wa pamoja wa changamoto zinazokwamisha jitihada za wanawake katika biashara.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa miongoni mwa faida za kuwa na Eneo Huru la Biashara la Barani Afrika ni kusaidia kuongezeka kwa biashara baina ya nchi za Afrika kutokana na nchi kuondoleana ushuru wa forodha.
“Faida nyingine ni kushughulikia kwa pamoja vikwazo vya biashara visivyo vya kodi na kukuza uongezaji thamani wa malighafi zinazozalishwa ndani ya Afrika.”