WANGAPI WAMEFUTIKA?

NA LWAGA MWAMBANDE

REJEA katika Biblia Takatifu kitabu cha 1Samweli 7:12...Ndipo, Samweli akachukua jiwe na kulisimamisha kati ya Mispa na Sheni. Akaliita Ebeneza, akisema, hata sasa BWANA ametusaidia".
Hakika ukiutafakari mstari huu kupitia neno hili la Mungu utaona wazi kuwa, baada ya Mungu kumsaidia Nabii Samweli na Israel kwa ujumla kuwapiga wafilisti, waliibuka na maombi ya kinabii wakisema, "Hata sasa BWANA ametusaidia".

Ni baada ya kipindi kirefu cha mapito na matengenezo kwa kanisa la Israel, kwani walipita katika kipindi cha kuanguka na kusimama.

Hayo yalikuwa ni mapito sawa sawa na ambayo pengine mimi na wewe katika mwaka 2023 tumeyapitia, kuna mahali tumeanguka, tumesimama tena kwa uwezo wa Mungu.

Kwa msingi huo, tunapofikia ukingoni mwa mwaka huu, na tukiwa tayari kwa mapokeo ya mwaka mpya 2024, tuendelee kusimama imara kwa kumtegemea Mungu wetu kwani, yeye ndiye huwa anatupa mahitaji ya mioyo yetu, afya, uzima na ulinzi katika maisha yetu.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa,hata sasa Mungu wetu, ameshatusaidia. Endelea;

1. Tunamalizia mwaka, kwa neema za Rabuka,
Jinsi hapa tunafika, hatuwezi kutamka,
Mungu wetu wa baraka, kwa mkono katushika,
Hata sasa Mungu wetu, umeshatusaidia.

2.Wangapi wamekatika, kuishi wamekuchoka?
Wangapi wamefutika, dunia imewachoka?
Wangapi wameondoka, na hata tukashituka?
Hata sasa Mungu wetu, umeshatusaidia.

3.Magonjwa yalitushika, kama yalivyowashika,
Ajali tulianguka, kama walivyoanguka,
Na tena tulipigika, kama walivyopigika,
Hata sasa Mungu wetu, umeshatusaidia.

4.Kwa watu tulifutika, kwa jinsi tulivyochoka,
Kifoni walituweka, ya kwamba watatuzika,
Lakini tumeamka, kwa rehema tunacheka,
Hata sasa Mungu wetu, umeshatusaidia.

5.Mipango ilipangika, kutuua kutuzika,
Wenyewe wameanguka, sisi bado twasikika,
Ni neema za Rabuka, haya yote kutufika,
Hata sasa Mungu wetu, umeshatusaidia.

6.Magonjwa ya kutajika, na sisi yalitushika,
Wengine wamekatika, sisi Mungu katushika,
Kweli tumebahatika, tu hai twaeleweka,
Hata sasa Mungu wetu, umeshatusaidia.

7.Wakubwa wameondoka, umri umeshafika,
Wadogo wamekatika, umri haujafika,
Wenzetu tumeshazika, sisi bado twadundika,
Hata sasa Mungu wetu, umeshatusaidia.

8.Tunalala twaamka, wanalala tunazika,
Twatembea tunafika, watembea waanguka,
Hata kama tumechoka, bado hatujafutika,
Hata sasa Mungu wetu, umeshatusaidia.

9.Mwaka unamalizika, tunapata mpya mwaka,
Tuombe kwake Rabuka, maisha yetu kushika,
Hata tutapokatika, yeye awe mhusika,
Hata sasa Mungu wetu, umeshatusaidia.

10.Wenzetu wametoweka, huzuni imetushika,
Ni mapenzi ya Rabuka, karuhusu kututoka,
Halali kusikitika, haya yaliyotufika,
Hata sasa Mungu wetu, umeshatusaidia.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news