Waziri Mhagama asema jambo mahafali Chuo cha Biblia Sakila

ARUSHA-Wahitimu wa Chuo cha Biblia Sakila jijini Arusha wameaswa kuwa askari wazuri wa vita dhidi ya mmomonyoko wa maadili ambao unaendelea kushamiri katika jamii zetu hususani kwa vijana.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe, Jenista Mhagama akiwatunuku vyeti wahitimu, wakati wa mahafali ya Chuo cha Biblia cha Evengelism Church yaliyofanyika, Sakila Katika wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu),Mhe, Jenista Mhagama wakati wa mahafali ya 83 ya chuo hicho yaliyofanyika, Sakila katika Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.

Waziri amewaambia wahitimu hao kwamba maendeleo ya taifa letu yanategemea sana nguvu kazi na nidhamu ya kazi, japo kuwa nchi yetu haiegemei upande wowote katika masuala ya dini, lakini sehemu kubwa ya watu wake wanaamini katika dini kupitia madhehebu mbalimbal

“Ni muhimu mkawe mabalozi wazuri katika vita hii na mkashirikiane na viongozi wengine wa dini na Serikali ili kwa pamoja tuhakikishe tunalilinda taifa letu dhidi ya upotofu huu wa maadili,” alibainisha.
Aidha, aliwasihi kuendelea kuliombea taifa amani, utulivu, upendo na mshikamano ili kulijenga taifa.

Waziri ametumia maandiko matakatifu, katika Injili ya Mathayo 5:13-16 ambayo yalisema,..nami pia niwasihi popote mnapokwenda, mkawe chumvi ya dunia na kamwe msipoteze ladha ya chumvi, lakini pia mkawe mwanga wa ulimwengu ukaangaze mbele ya watu ili wayaone matendo yenu mema wamtukuze baba yenu aliye mbinguni...

“Sina shaka kwamba, wote mkitoka hapa mtakwenda kutekeleza jukumu la kichungaji na kufundisha watu kwa upendo, uaminifu na kuwaongoza katika kweli maana huo ndio wito mlioitiwa,” alifafanua.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe, Jenista Mhagama akizungumza jambo Dkt. Eliud Issangya, Askofu Mkuu wa International Evangelism Church na Mkuu wa chuo cha Biblia Sakila.

Kwa upande wake Dkt. Eliud Issangya, Askofu Mkuu wa Kanisa la International Evangelism Church na Mkuu wa Chuo cha Biblia Sakila amesema, wahitimu wa chuo cha Biblia wanapaswa kwenda kuweka mkazo wa kufundisha maadili kwenye jamii.

“Msambaze maandiko kwa kulenga maadili na si kwa kutafuta mali, bali watu waweze kuishi kwa kuthaminiana na wawe watu wenye hekima,” alihimiza.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe, Jenista Mhagama akizungumza jambo na Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Mhe. Joshua Nassari wakati wa mahafali ya chuo hicho yaliyofanyika, Sakila Katika wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.

Awali mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe.Joshua Nassari ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Monduli alisema serikali ya mkoa wa Arusha itaendelea kutoa ushirikiano wa kiroho kwa chuo hicho cha Biblia na madhehebu mengine.

“Jamii yetu imekuwa ikipitia changamoto kubwa za mabadiliko ya kimadili na kitamaduni hivyo tujikite katika kufundisha maadili mema ya kitanzania na madili mema ya imani ili tuwe na jamii iliyostaarabika,”alihimiza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news