Waziri Mkuu aipongeza Kampuni ya Azam Media Limited

DAR ES SALAAM-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewapongeza viongozi na wafanyakazi wa kampuni ya Azam Media Limited kwa mafanikio lukuki waliyopata katika kipindi cha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake.
Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akipokea Tuzo Maalum ya Azam Media kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Azam Media, Abubakar Bakhresa wakati alipofunga Maadhimisho ya Miaka 10 ya Azam Media kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam Desemba 17, 2023.

Amesema kupitia urushaji wa matangazo yake, kampuni hiyo imeweza kuwa mzalishaji mkubwa wa ajira kwa mawakala, wanataaluma mbalimbali, imeinua wanamichezo katika soka, masumbwi, mbio za magari na pikipiki, waigizaji wa filamu na wasanii wa muziki.

“Pia mmedhamini baadhi ya vilabu nchini, kuweka taa kwenye baadhi viwanja vya michezo hali ambayo imewezesha mechi za soka kuchezwa usiku. Msione hili kuwa ni jambo dogo, AZAM mko mbali sana. AZAM mko juu,” alisema.

Alitoa pongezi hizo jana usiku Jumapili, Desemba 17, 2023 wakati akifunga maadhimisho ya miaka 10 ya Kampuni ya Azam Media Limited yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

“Ninawapongeza Azam Media Limited kwa kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ajira kwa Watanzania kuanzia mawakala hadi watangazaji. Tunakutambua Azam Media Limited kama mdau mkubwa wa kutoa ajira,” alisema.

“Ninawapongeza pia kwa kubeba dhima ya kutunza mazingira kupitia kampeni yenu ya ‘Mito ni Maisha Yetu.’ Ninawapongeza kwa kuona maeneo nyeti na kuyaingiza kwenye mpango wenu wa mwaka yakiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 ya Azam Media Limited,” alisema.

Alisema, kupitia kampeni hiyo, walihamasisha makundi ya jamii ili yashiriki kwenye uhifadhi na utunzaji wa vyanzo vya maji. “Lengo lilikuwa ni kujenga uelewa ili jamii ifanye shughuli zao za kibinadamu kwa kuzingatia umuhimu wa kutunza mito ambayo ni tegemeo kubwa kwa viwanda, kilimo, uzalishaji wa umeme na matumizi ya nyumbani. Naungana nanyi katika hili kwani haya ndiyo mambo ambayo Watanzania wanatakiwa kuyasikia na kuyazingatia wakati wote.”

Mapema, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye aliwapongeza wafayakazi wa kampuni hiyo kwa kuzingatia weledi katika utendaji kazi wao.

“Azam Media ni miongoni mwa vyombo ambavyo vinanipa usingizi mzuri kutokana na umahiri wao wa kazi, lakini pia niwapongeze kwa uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na kampuni hii ili kuhakikisha matangazo yao yanafika maeneo mengi.”

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa AZAM Media Limited (AML), Tido Mhando alisema maadhimisho hayo yalianza Januari Mosi 2023 na waliyapanga yafanyike kwa mwaka mzima ili waweze kuufahamisha umma nini kimefanyika ndani ya miaka hiyo 10.

Alisema katika kipindi hicho, wameweza kujijenga kwa kiwango kikubwa na kwamba hivi sasa wanasikika kote Afrika Mashariki na Kati

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa makampuni yanayounda Bakhresa Group, Abubakar Bakhresa aliwashukuru Watanzania wote kwa jinsi walivyoipokea kampuni ya AZAM na bidhaa zake.

“Tunaishukuru Serikali kwa kuweka milango yake wazi wakati wote. Pia tunawashukuru wadau wetu tunaofanya nao kazi kama Bodi ya Filamu, BASATA na wengineo,” alisema

Alisema miaka 10 ya mwanzo ilikuwa ya kujifunza, ninaamini miaka 10 ijayo, itakuwa ya kuboresha na kuongeza mchango zaidi kukuza michezo na sekta nyingine.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news