WAZIRI MKUU ASHIRIKI SHEREHE ZA KUAPISHWA RAJOELINA

ANTANANARIVO-Waziri Kassim Majaliwa leo Jumamosi, Desemba 16, 2023 ameungana na Marais kutoka nchi sita barani Afrika kwenye sherehe za kumuapisha Rais wa Madagascar, Andry Rajoelina.
Waziri Mkuu ambaye amemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alikuwa miongoni mwa marais kutoka Comoro, Angola, Zimbabwe, Msumbiji, Mauritius, Guinea-Bissau na wawakilishi kutoka nchi zaidi ya 10 ambao wameshiriki sherehe za kuapishwa kwa Rais wa nchi hiyo zilizofanyika kwenye uwanja wa Barea, eneo la Mahamasina, jijini Antananarivo.

Viongozi walioziwakilisha nchi zao wanatoka China (CPPCC), Rwanda, Seychelles, Senegal, Côte d'Ivoire, India na mabalozi mbalimbali. Mbali na Marais wa AU na SADC, viongozi wengine walitoka Kamisheni ya Bahari ya Hindi (Indian Ocean Commission), COMESA na Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Mapema, akilihutubia Taifa hilo mara baada ya kuapishwa, Rais Andry Rajoelina alisema ana mapenzi ya dhati kwa nchi hiyo na wananchi wake na akawahakikishia kuwa atafanya kila awezalo ili kuendeleza umoja na mshikamano wa Taifa hilo.
Rais huyo ambaye anachukua kiti hicho kwa mara ya tatu alisema: “Hatutaki kuwa nchi ambayo haina utulivu. Tutasonga mbele kuhakikisha kila wilaya inapata maendeleo ya kiuchumi kwani tunayo maono (vision) na malengo tunayotaka kuyafikia.”

Katika hotuba yake iliyochukua dakika 20, Rais Rajoelina aliongea kwa Kimalagasi, ambayo ni lugha ya Taifa ya nchi hiyo. Alipomaliza, akatumia dakika saba kuhutubia kwa Kifaransa kwa ajili ya viongozi wa Kimataifa ambao waliohudhuria sherehe hiyo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimpogeza Rais wa Madagascar Andry Rajoelina katika dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa Ikulu ya Antananarivo. Waziri Mkuu alimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye sherehe za kumwapisha Rais huyo zilizofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Barea uliopo Mahamsina, Desemba 16, 2023. Kulia ni Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa, wa pili kulia ni Mke wa Rais wa Madagascar, Mialy Rajoelina na kushoto ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia Masuala ya Afrika Mashariki, Wakili Stephen Byabato. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Pia Rais Rajoelina alisisitiza kwamba atakuwa Rais wa watu ambaye anataka kuona ushirikishwaji wa kila mmoja katika kuleta maendeleo ya nchi hiyo.

Kabla ya kuondoka uwanjani, Rais Rajoelina alishuhudia bahati nasibu ikichezeshwa na kisha akakabidhi funguo za nyumba ya kisasa iliyowekewa samani zote iliyoko Lake Village eneo la Ivato, kwa mshindi wa bahati nasibu hiyo. Ujenzi wa makazi bora ni moja ya malengo ya 13 ambayo Rais huyo amejiwekea.
Malengo mengine ni Amani na Ulinzi; Nishati na Maji; Mapambano dhidi ya Rushwa na kuleta Usawa; Elimu na Utamaduni; Afya kwa Wote; Ajira bora kwa wote; Uwekezaji na Viwanda; Mustakabali wa Vijana na Wanawake na Uzalishaji wa Chakula cha Kutosha. Mengine ni Menejimenti Endelevu ya Maliasili; Ujenzi wa Makazi bora na Ukuzaji wa Miji; Uwezeshaji na Uwajibikaji na Michezo kwa Wote.

Rais Rajoelina ambaye alishika madaraka ya nchi hiyo mwaka 2009-2014 na 2019-2023 ni kiongozi wa Chama cha Young Malagasies Determined (TGV) ambacho itikadi yake ni mageuzi (reformism), uwazi wa Serikali (government transparency) na demokrasia ya kijamii (social democracy).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news