MANYARA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewatembelea watu walioathiriwa na mafuriko ya tope na mawe katika mji mdogo wa Katesh, wilaya ya Hanang, mkoani Manyara na kuwapa salamu za pole kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza nao kwa nyakati tofauti, leo mchana Jumanne, Desemba 5, 2023 kwenye shule ya sekondari ya kidato cha tano na sita ya Katesh, Waziri Mkuu amewaomba wawe watulivu wakati Serikali ikiendelea kuratibu maafa hayo.
Amewaomba wawe watulivu kwani watakuwa hapo shuleni kwa muda wakati Serikali ikiwatafutia sehemu mbadala. “Ninawaomba muendelee kutulia wakati Serikali bado inaratibu maafa haya kama ambavyo Mheshimiwa Rais Samia ameelekeza.”
Akielezea hali ilivyokuwa, mmoja wa manusura hao, Mzee Martin Daniel Kessy alisema Jumapili asubuhi alipotaka kutoka ndani akakuta maji mengi na mengine yanaingia ndani.
"Wakati nahangaika kuzuia maji, nikasikia wajukuu wakiniita babu, babu, maji yanajaa, ikabidi niwape nyundo watoboe dari na bati. Walipokuwa juu salama, nami nikaweza ngazi na kupanda juu na kusubiri msaada sababu hapo chini maji yalishanifika kifuani," alisema.
Mzee Kessy ambaye pia ni Balozi wa mtaa wa Katesh A Sokoni, amethibitisha Waziri Mkuu kwamba katika mtaa wake hakuna watu waliopoteza maisha isipokuwa wote walishindwa kuokoa mali zao.
"Nilicheki na watu wangu wote wako salama lakini hakuna aliyetoka na kitu, si magodoro wala mahindi, hakuna aliyetoka na kitu chochote ndani ya nyumba," amesema Mzee Kessy ambaye mtaa wake ulikuwa na kaya 40.
Naye kijana Khalid Salehe ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi ya Katesh B, alimweleza Waziri Mkuu kwamba mama, kaka na dada zake wote ni wazima na kwamba wamenusurika kwenye mafuriko hayo.
Alipoulizwa na Waziri Mkuu kama baba yake naye amenusurika, Khakid alijibu kuwa baba yao alikuwa amesafiri na yuko Iringa.
Kijana mwingine ambaye anasoma darasa la nne na Khalid na yupo kwenye kambi hiyo, Omari Miraji alisema kuwa wazazi wake, kaka na dada zake wote wamesalimika. Alipoulizwa kama kuna rafiki zao au wanafunzi wenzao waliopotea kutokana na mafuriko hayo, alijibu kwamba hakuna aliyepotea.
Mapema, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga alimweleza Waziri Mkuu kwamba katika shule hiyo wametenga chumba cha kutunza misaada wanayoipokea. Alisema hadi sasa wameshapokea, magodoro 200, mashuka, mablanketi, mikeka, maji, unga, mchele, mabeseni, ndoo na baadhi ya nguo za watoto.