ZANZIBAR-Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Riziki Pembe Juma amelitaka Jeshi la Polisi Zanzibar kuharakisha masuala ya upelelezi kwa kesi za vitendo vya ukatili na udhalilishaji ili kuona zinamalizika ndani ya muda mfupi.
Maandamano ya Kilele cha Maadhimisho ya Kufunga Siku 16 za harati za kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto yaliyofanyika Muyuni, Wilaya ya Kusini Unguja, Desemba 11,2023.
Kauli hiyo aliitoa Desemba 11,2023 katika kilele cha maadhimisho ya kufunga siku 16 za harakati za kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto yaliyofanyika katika Kijiji cha Muyuni Wilaya ya Kusini Unguja.
Mheshimiwa Riziki amesema, taarifa za Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zinaonesha hali inatisha, kwani katika kipindi cha mwezi Januari hadi Oktoba 2023 jumla ya matukio 1,620 yameripotiwa ambapo matukio 1,360 yanahusu watoto, 194 wanawake na wanaume 77.
Alisema, pamoja na kazi kubwa inayofanywa na Jeshi la Polisi, lakini bado ucheleweshwaji wa upelelezi wa matukio hayo umekuwa mkubwa hali ambayo inapelekea kesi nyingi kukaa muda mrefu katika vituo vya Polisi Zanzibar.
Alisema, kuendelea kwa hali hiyo itaweza kuathiri malengo ya Serikali katika mapambano ya kuondoa vitendo hivyo pamoja na kuwatia hatiani watu wanaothibitika kutenda vitendo vya ukatili na kudhalilisha ndani ya nchi.
Aidha,alisema ipo haja ya kutambua na kuweka kampeni maalum za kuyakabili matendo ya udhalilishaji wa kijinsia kwa kuweka nguvu kazi na kampeni isemayo “Wekeza katika Kuzuia Ukatili Dhidi ya Watu Wenye Ulemavu” na “Nijuze Nijilinde Dhidi ya Ukatili wa Kijinsia”.
Alieleza kwamba, kundi hilo la watu wenye ulemavu limekuwa na changamoto kadhaa ambazo zimekuwa zikiwakabili na hivyo kuna haja ya kuwa na tafakuri ya kina inahitajika katika kumkomboa mtu mwenye ulemavu dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Watendaji wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, wanarakati wa kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji na wananchi mbalimbali wakiwa katika kilele cha maadhimisho ya kufungu siku 16 za harati za kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji kwa Wanawake na Watoto, yaliyofanyika Muyuni, Wilaya ya Kusini Unguja, Desemba 11,2023.
Mapema Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Abeida Rashid Abdalla, alisema bado matukio ya udhalilishaji yanaongezeka ikiwemo matukio ya kubaka, kunajisi ambapo Wilaya ya Mjini na Magharibi ‘A’ na ‘B’ zinaongoza kwa kesi hizo nyingi.
Alieleza kwamba wakiwa wanahitimisha kilele cha siku 16 lakini bado mapambano yanaendelea hivyo ni lazima jamii kwa pamoja wanaumme na wanawake wote wanalazimika kupambana na matendo hayo kwani bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha matendo hayo yanaondoka nchini.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Kusini Unguja, Bi.Radhia Rashid Haroub, aliipongeza Wizara hiyo kwa kuadhimisha siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji katika mkoa huo.
Alisema, bado nguvu za mapambano zinahitajika kwani Mkoa wa Kusini matukio hayo yameongezeka mwaka jana 2022 kulikua na jumla ya matukio 1,320 ambapo kwa mwaka huu yamefikia matukio 1,620 sawa na ongezeko la asilimia 16.
Kwa upande wa wanaharakati wa kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji akizungumza kwa niaba Bi.Amina Yussuf Ramadhani alisema,jamii imeshapata uelewa wa kuripoti matokeo hayo, lakini bado tatizo la muhali linaendelea kujitokeza na kusababisha baadhi ya kesi kusuluhishwa katika ngazi ya familia.