NA GODFREY NNKO
WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekata mirija ya ulaji kwa wenyeviti wa serikali za mitaa, vijiji na watendaji ambao walikuwa wanajihusisha na uuzaji wa ardhi katika maeneo mbalimbali nchini.
Uamuzi huo umefikiwa leo Desemba 22,2023 jijini Dar es Salaam na Waziri wa wizara hiyo, Mheshimiwa Jerry Silaa (Mb.) wakati akielezea tathimini ya siku 100 tangu aanze kuiongoza wizara hiyo kupitia kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini.
"Ninatoa maelekezo kuanzia leo (Desemba 22,2023) na ninaagiza watendaji wa Serikali za mitaa waache mara moja kujihusisha na masuala ya ardhi.
"Waache kuchukua asilimia 10 za wananchi kwenye ardhi. Maelekezo yangu ni kwamba kuanzia leo masuala yote yanayohusu ardhi yafanywe na maafisa wa ardhi waliopo kwenye eneo husika,”amesema Waziri huyo.
Waziri Silaa amesema kuwa, kumekuwa na malalamiko mengi ya wananchi katika ununuzi wa ardhi na kwamba viongozi hao wamekuwa wakihusishwa kwenye malalamiko kwa kuchukua asilimia 10 za wananchi wakati wa mauziano.
Pia, amesema watendaji wa Serikali za mitaa na vijiji hawana mamlaka ya kisheria kufanya hivyo na kwamba kuanzia sasa masuala yote yanayohusiana na ardhi yatafanywa na maafisa ardhi waliopo kwenye maeneo husika nchini.
"Niwatake wananchi wote waepuke kununua ardhi kwa Mwenyekiti wa Kijiji, Mwenyekiti wa Kijiji hana hayo mamlaka.
"Kwa wale wanaokwenda kununua viwanja vijijini hakikisha umeitishwa mkutano wa kijiji kwa ajili ya kujadiliwa na kutolewa uamuzi wa kupewa ardhi na ikiwezekana tumia simu kurekodi kwa kukubaliwa kupewa hilo eneo,"amefafanua.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Silaa amewataka wananchi kununua ardhi iliyopimwa na kupangwa ili kuepuka changamoto mbalimbali ikiwemo migogoro.
Vile vile,Mheshimiwa Silaa amesema, wizara yake inakusudia kufanya mageuzi makubwa ya kimfumo wa utendaji katika Sekta ya Ardhi nchini kwa lengo la kuboresha utendaji kazi katika utoaji huduma bora.
“Wizara inakusudia kufanya mageuzi makubwa ya kimfumo wa utendaji katika Sekta ya Ardhi nchini ambayo yanalenga kuboresha utendaji kazi katika utoaji huduma za sekta ya ardhi,"amesema Waziri Silaa.
Amesema, maboresho hayo ni Programu ya Kupanga, Kupima, Kumilikisha ardhi (KKK) kwa kushirikisha sekta binafsi na mamlaka za upangaji.
Waziri Silaa amesema,katika maboresho hayo yatafanya marekebisho ya utaratibu wa kukopesha fedha kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Viwanja utakaokuwa unatunza fedha na kukopesha fedha kwa ajili ya programu hiyo.
Amesema, wizara inakamilisha maboresho ya mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambao utaruhusu huduma na miamala ya sekta kuanza kutolewa kidigitali.
Silaa amesema, mfumo huo utaanza kutumika hivi karibuni kwa kuanza na mikoa ya Arusha, Tanga, Mwanza na Mbeya.
Pia amesema, wizara inafanya mabadiliko ya kimuundo na ya kiutendaji kwa kuanzisha mikoa maalumu ya ardhi katika maeneo yenye uhitaji mkubwa ukiwemo Mkoa wa Dar es Salaam na Dodoma.
"Tumeamua kuanzisha mikoa mipya ya ardhi, kutoka mikoa ya utawala 26 nchini. Dar es Salaam tunaanzisha Mkoa Maalum wa Ardhi, Kinondoni, Ilala, Kigamboni, Ubungo, Temeke.
"Jambo la kwanza ni kufanya mabadiliko ya kisheria, kisera na kimfumo. Ipo Sera ya Ardhi.
"La pili, tunazipitia sheria zote zinazohusu ardhi ili kuweza kuleta majibu ya changamoto ambazo zinawakabili wananchi katika sekta ya ardhi."
Amesema, maboresho hayo yanaweza kuendelea kufanyika katika mikoa yenye miamala mingi ya ardhi ikiwemo Mkoa wa Mwanza na Pwani.
Ameongeza kuwa, wizara itadhibiti ujenzi holela wa viwanda na kuelekeza viwanda kujengwa katika maeneo ya kongani za Viwanda na kuongeza maeneo ya kutosha kwa ajili ya Kongani za Viwanda mathalani Kongani ya Viwanda kama Mlandizi na Kwala Chalinze na SinoTan Kibaha.
Amesema,ndani ya siku 100 amefanya ziara kwenye mikoa 25, katika ziara hizo amekutana na wananchi kupitia kiliniki za ardhi.
"Na sisi tumeona tuanzishe kiliniki za ardhi kwa sababu matatizo ya ardhi ni mengi.
"Moja kati ya sababu ya kuwa na kliniki za ardhi ni kuhakikisha tunahudumia wananchi wengi zaidi kuliko tunapofanya shughuli zetu za kila siku ofisini, lakini pia mwananchi anapofika pale anakutana na watendaji wote na inapofika jioni anatoka na hati yake jioni."
Pia amemuelekeza Katibu Mkuu kuhakikisha kliniki hizo zinafanyika chini ya hema na si ndani ya vyumba ili kuepuka vishawishi vya rushwa na hakutakuwa na siri.
Pia, amesema amemwelekeza Katibu Mkuu katika ofisi za ardhi pawe na kamera ambazo zitasaidia kuimarisha uwajibikaji kwa watumishi.
"Kliniki za ardhi kama nilivyosema zimefanyika pale Dodoma, lakini nimeagiza nchi nzima zifanyike ili wananchi waweze kupata fursa ya kuhudumiwa."
Amesema, baada ya kuapa kulikuwa na maelekezo ya jumla ambayo Mheshimiwa Rais alimpa na mengine ni kwa ajili ya umma ya nini hasa ambayo anataka kuyaona katika Wizara ya Ardhi.
Amesema, baada ya kuripoti wizarani Mtumba alitoa maelekezo kwa watendaji ambayo yalikuwa na vipaumbele 12.
"Na kila mtendaji nilimuelekeza ajipange kuona ni jinsi gani anatengeneza mfumo wa mabadiliko, kwamba ni kwa kiasi gani antekeleza yale maelekezo."
Wakati huo huo, Waziri Silaa amezindua rasmi mfumo wa Ardhi App ukiwa ni maalumu wa kupokea na kushughulikia malalamiko yote yatakayowasilishwa kiurahisi kwa kutumia simu ya kiganjani au kompyuta kuwahudumia watanzania katika sekta ya ardhi.
Amesema, kupitia programu tumishi mpya ya Kliniki mwananchi atakuwa huru kuwasilisha changamoto na malalamiko yake yanayomkabili kuhusu ardhi popote pale alipo nchini.
Mheshimiwa Silaa amesema, mfumo huo pia utawasaidia wananchi kutoa mrejesho wa ubora wa huduma walizopatiwa pamoja na kuwasilisha tena malalamiko husika pale ambapo hawajaridhika na majibu ama jinsi walivyohudumiwa.
Naibu Waziri
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Geophrey Pinda amempongeza, Mheshimiwa Waziri Silaa kwa kutimiza siku 100 za mafanikio.
"Wizara yetu ni dude kubwa sana, nikupongeze kwa kutimiza siku za kwanza, ninaamini awamu ijayo watakuona sana ili kuwaelezea mafanikio zaidi.
"Mheshimiwa Waziri siku 100 za kwako wizarani na sisi tulikuwa darasani, kwa hiyo Mheshimiwa siku 100 tumepata dira na mwelekeo wako wa wapi ambapo unataka wizara yako inataka ielekee, na sisi tunaahidi kila aina ya ushirikiano ambao utakuwa unahitajika katika kipindi chetu hiki cha uongozi.
"Ili kipindi kirefu au kifupi ambacho utakuwa hapa kiweze kuwa na matokeo mazuri,"amefafanua Naibu Waziri Pinda huku akimpongeza kwa kuwa na utaratibu muhimu wa kukutana na wahariri wa vyombo vya habari ili kuelezea kuhusu tathimini ya uongozi wake.
TEF
Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meema amesema kuwa, ni jambo la faraja kwa Waziri Silaa kutimiza ahadi yake ya kutoa mrejesho kwa siku 100 alizoahidi.
"Mheshimiwa Waziri nizungumzie mambo matatu, jambo la kwanza ni mipango miji, Tanzania kuna miji mingi inaanzishwa, kuna miji mingi, lakini ni donda ndugu huwa inaota tu,lakini haina mipango. Haipangwi, itaendelea vile siku ya siku inaibuka migogoro,"amesema Meena.
Amesema kuwa, kabla ya mji kuanza ni vema mipango yake ikaratibiwa vema ili kuepusha gharama mbalimbali na migogoro ambayo haina afya kwa ustawi wa jamii na Taifa.
Pia, ameishauri Serikali kuangalia namna ambavyo itakuwa na mfumo ambao kila mwenye kiwanja atakuwa na uwezo wa kufuatilia taarifa zake kupitia mtandao ili kuondokana na changamoto mbalimbali zinazohusiana na hati.
"Jambo la tatu, vituo vya mafuta. Kama mwezi mmoja uliopita tulikuwa na mkutano na watu wa EWURA, walijaribu kujieleza...lakini mwisho wa siku walisema kuwa wanaotoa kibali ni Wizara ya Ardhi.
"Hapa Dar es Salaam kuna vituo vya mafuta kila kona, Mheshimiwa Waziri hivi vituo ni vingi kuna siku vinaweza kulipuka,"amefafanua Meena.