NA GODFREY NNKO
PIICHA NA SUNGMI KIM/STUFF.
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Jerry Silaa amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi, Bw.Deogratius Kalimenze kutokana na kuidhinisha waraka wa mwaka 2018 unaohalalisha uwepo wa vituo holela vya mafuta nchini.
PIICHA NA SUNGMI KIM/STUFF.
Mheshimiwa Waziri Silaa ametoa maelekezo hayo Desemba 22, 2023 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini, cha kutathimini siku 100 za uongozi wake tangu ateuliwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kuiongoza wizara hiyo.
“Katibu Mkuu umsimamishe Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi kwa ule waraka wake aliouandika ambao ulienda kutengeneza kadhia, lakini nilijiuliza siku ile tukiwa pale Dodoma, kwamba ni nani aliandaa kanuni za 2018?.
“Na mimi ninasema wazi hakuna watu wabaya kama watumishi wa umma,kwa sababu kanuni huwa ni za Waziri, kwa hiyo ukiuliza hizi kanuni zinatoka wapi, Mheshimiwa Waziri ni kanuni zako yaani kanuni za kutengeneza vituo vya ovyo ni za kwangu mimi Waziri.
“Ukiambiwa ni za kwako ukubali mawili, kuamua ni za kwangu mimi Jerry Silaa au kutafuta Waziri wa kumuangushia mzigo ambao sio utaratibu mzuri wa collective responsibility ya Serikali, lakini ni nani alipitisha Waziri akatia saini kwenye zile kanuni? Kwa hiyo, Katibu Mkuu hayo ndiyo maelekezo yangu.
“Ili nikianza kuchukua hatua kule nje, wale waliopata uhalali kwenye uharamu wajue, sasa tunafanya mabadiliko makubwa kwenye wizara yetu, lakini baya zaidi tunaweka vituo vya mafuta karibu na shule.
“Tunaweka vituo vya mafuta karibu na hospitali, tunaweka vituo vya mafuta karibu na maeneo ya mikusanyiko mkubwa wa watu, makanisa, misikiti kila mkoa umejaa vituo vya mafuta. Ipo siku huu mji utachomeka halafu tutasema bahati mbaya au mipango ya Mungu.”
Waziri Silaa amesema, hayo yatatokea kwa sababu wao kama wataalamu wameamua kufanya mambo ambayo hayaendani na taratibu huku akisisitiza kila jambo lazima lifuate kanuni na taratibu.