Yajayo yafurahishe

NA LWAGA MWAMBANDE

REJEA Biblia Takatifu katika kitabu cha Mathayo 19:6..."Basi hawakuwa wawili tena, bali mwili mmoja. Basi alichounganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe".

Mhubiri 4:9..."Heri wawili kuliko mmoja; kwa kuwa wao wanapata thawabu nzuri kwa taabu yao."
Wanandoa wenye ndoa imara, wanajua umuhimu wa kushirikiana pamoja na kupata nguvu na faraja katika safari yao ya ndoa.

Ndiyo maana neno la Mungu kupitia Waefeso 4:32 linasema, "Nanyi mwende kwa wengine kwa fadhili, na rehema, na unyenyekevu, na upole."

Hii inamaanisha kwamba, kuwa na moyo wenye huruma na kuelewana ni nguzo muhimu katika ndoa kwa ustawi bora wa familia na Taifa kwa ujumla ili kuendelea kulifanya jina la Mungu liendelee kuhimidiwa milele daima.

Mshairi wa kisasa, lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, kama tulikotoka penzi liligawanyika, basi ni wakati wa kulikusanya ili 2024 iwe familia ya heri na baraka. Endelea;

1 Penzi lilogawanyika, ni muda kulikusanya,
Nyumba loparaganyika, ni muda kuikusanya,
Mwaka unamalizika, mema tuweze kufanya,
Yaliyopita sindwele, yajayo yafurahishe.

2. Yajayo yafurahishe, tunayokwenda kufanya,
Yote tuyaunganishe, yale tuliyotawanya,
Mabaya yasituchoshe, mwenzangu ninakukanya,
Yaliyopita sindwele, yajayo yafurahishe.

3. Yajayo yafurahishe, Mungu katupa kufanya,
Angetufanya tuishe, uhai akauminya,
Uhaia utuamshe, tufanye ya kukusanya,
Yaliyopita sindwele, yajayo yafurahishe.

4. Haipendezi kabisa, ugomvi ulivyofanya,
Nyumbani watoto sasa, hakuna wa kuwaonya,
Acha kupiga siasa, pataneni nawaonya,
Yaliyopita sindwele, yajayo yafurahishe.

5. Ndugu mliyekosana, lile jambo alifanya,
Ni muda wa kupatana, vile Mungu anafanya,
Sisi twamkosa sana, twatubu anatuponya,
Yaliyopita sindwele, yajayo yafurahishe.

6. Kama wampenda Mungu, yake lazima kufanya,
Ametuagiza Mungu, msamaha kuufanya,
Ili naye huyu Mungu, kwetu aweze ufanya,
Yaliyopita sindwele, yajayo yafurahishe.

7. Mwaka mpya unakuja, nini waenda kufanya,
Ile ndoa imechuja, bado hasira wafanya?
Msamaha nautaja, tunaopaswa kufanya,
Yaliyopita sindwele, yajayo yafurahishe.

8. Ubarikiwe na Mungu, uamuzi ukifanya,
Kuachana na uchungu, na mambo ya kutapanya,
Kuyatenda ya KiMungu, sawa Mungu anafanya,
Yaliyopita sindwele, yajayo yafurahishe.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news