ZANZIBAR-Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC),Jaji George Joseph Kazi amewataka wananchi waliotimiza sifa za kupiga kura kujitokeza katika zoezi la uandikishaji kwenye daftari la kudumu la mpiga kura ili waweze kushiriki katika uchaguzi ujao wa mwaka 2025.
Mwenyekiti ameyasema hayo wakati alipoanza ziara ya kutembelea vituo vya uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura wapya.
Akiwa ameambatana na Mkurugenzi wa Uchaguzi katika Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Thabit Idarous Faina ,Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi pamoja na Maafisa mbalimbali kutoka tume hiyo,Jaji George Kazi amesema zoezi la uandikishaji kwa Unguja ndio limeanza kwa Mkoa wa Kaskazini Unguja,Wilaya ya Kaskazini 'A'.
Pia, amesema zoezi hilo mpaka sasa linakwenda vizuri kwa mujibu wa wasimamizi wa vituo vya uandikishaji, na mawakala wa vyama vya siasa.
Maeneo 13 yaliyotembelewa na ujumne huo ni pamoja na Tumbatu, Mkokotoni, Potoa, Kidoti, Fukuchani, Tazari, Nungwi nakadhalika.
Akizungumza mara baada ya kuvitembelea vituo hivyo Mkurugenzi wa Uchaguzi, Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Thabit Idarous Faina amesema licha ya kuwepo kasoro ndogo ndogo hali ya kazi zoezi hilo kwa ujumla inaenda vizuri huku akizigusia baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na kutokusoma kwa alama ya vidole na Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi kwa baadhi ya waandikishwaji, ambapo masuala yote hayo huwa yanapatiwa ufumbuzi wa haraka.
Vile vile ametoa wito kwa wale wote wenye sifa na vigezo wajitokeze kwa wingi katika uandikishaji wa awamu hii ya kwanza kwa sababu maandalizi mazuri ni yale yanayofanywa mapema.
Zoezi hilo la uandikishaji wa wapiga kura wapya wenye sifa na vigezo ambalo lilianzia kisiwani Pemba tarehe 2 Desemba, 20023 na kuanza kwa Unguja tarehe 23 Desemba 2023 linatarajiwa kumalizika tarehe 15 Januari 2024 ikiwa ni sehemu ya matayarisho ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.