Aldasgate yatembelewa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania

MANYARA-Leo Januari 20,2024 Kitengo cha Mawasiliano na Masoko cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwa kushirikiana na Kituo cha Mkoa wa Manyara cha chuo hicho wametembelea Shule ya Sekondari ya Aldasgate iliyopo mjini Babati na kuzungumza na wanafunzi wa kidato cha Tano na Sita.
Lengo kuu la ziara hiyo ni kutoa huduma kwa jamii na elimu kwa umma kuhusiana na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Yaliyozungumzwa ni pamoja na;

Mosi: Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Aldasgate wa kidato cha Tano na Sita ni wasichana na wavulana wanaosoma katika mikondo ya Sayansi na Sanaa.

Tulitoa hamasa kwao kwamba wao ni taifa la leo na kesho na taifa linawategea katika kukuza uchumi wa nchi yetu siku chache zijazo.

Hivyo,wanapaswa kulitambua hilo na kuongeza juhudi katika masomo yao ili wafaulu na kufuzu vizuri katika mitihani ya taifa wakiwa na ujuzi na maarifa ya kutosha kujitegemea.
Pili: Tuliwaeleza wanafunzi hao kuhusu Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwamba ni Chuo Kikuu cha serikali ambacho kimeanzishwa kwa sheria ya Bunge namba 17 ya mwaka 1992.

Chuo hiki ni kikubwa kikiwa na vituo katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.

Lengo kuu la kuanzishwa chuo hiki ni kutimiza azma ya serikali na viongozi waasisi wa nchi kwamba elimu ya juu iwafikie watu wote popote pale walipo bila vikwazo.

Azma hii inafikiwa kwa sababu chuo kinatoa elimu kwa njia za Huria, Masafa na Mtandao katika ngazi za cheti, diploma, shahada, shahada za umahiri na uzamivu.

Wananchi vijijini na mijini wanasoma chuo Kikuu wakiwa huko huko walipo wakiendelea na kazi zao.
Tatu: Tumewaeleza wanafunzi hao kwamba, ukijiunga na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania utafurahia sana ufundishaji na ujifunzaji ambao hufanyika kwa njia ya mifumo ya kisasa kufuatia maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Mihadhara hufanyika kupitia mtandao wa ZOOM ikiwa ni mubashara kila mwanafunzi akiwa huko alipo na mhadhiri akiwa sehemu yoyote katika vituo vya mikoa na uratibu nchini kote.

Ikiwa mwanafunzi muda huo hawezi kujiunga kwenye mhadhara kwa sababu yoyote ile basi atapata mhadhara uliorekodiwa.

Si hivyo tu bali pia, matini za kujisomea kuhusu mada mbalimbali za kozi husika hupatikana katika mfumo wa ufundishaji na ujifunzaji kielekroniki (MOODLE) zikiwa zimepangiliwa vizuri kwa kufuata muongozo wa kozi (course outline).

Kama hiyo haitoshi, maktaba ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ipo mtandaoni mwanafunzi anaweza kuingia na kujisomea akiwa popote wakati wowote iwe mchana, usiku na kuwe na mvua ama jua.

Mafunzo ya ana kwa ana kwa wanafunzi kufika vituoni pia hufanyika ikiwa ni pamoja na mafunzo ya vitendo.

Chuo kina maabara za sayansi na sasa zinajengwa mpya kwenye kanda saba. Chuo kina maktaba katika vituo vyote na maktaba kuu kwenye makao makuu ya chuo.

Wanafunzi hutumia miundombinu hii kujisomea wakati wowote.

Nne: Tumewaeleza wanafunzi hao kwamba, wanafunzi hufanya mijadala kupitia Vimbwetta vya mitandaoni kama ZOOM, What's App, Telegram, Google na katika Vimbwetta vya ana kwa ana vilivyopo kwenye vituo vya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Kupitia mijadala hiyo wanafunzi wanapeana maarifa wao kwa wao wakiunganisha na yale yanayotoka kwa walimu wanakuwa wamepata maarifa na ujuzi wa kutosha kabisa.

Tano: Tumewaeleza wanafunzi hao kuhusu sifa za kujiunga na shahada ya kwanza kwenye vyuo vikuu vyote Tanzania kwa mujibu wa Tume ya Vyuo vikuu nchini kwamba ufaulu wa mwisho ni angalau alama D mbili ambayo ni sawasawa na pointi 4.

Ikiwa mwanafunzi atapata chini ya hapo basi atalazimika kujiunga na Foundation Program ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na akihitimu atapata fursa ya kujiunga na shahada ya kwanza kwenye vyuo vikuu mbalimbali vya Tanzania na nje ya nchi.

Sifa za kujiunga na foundation ni kuanzia ufaulu wa daraja la Tatu pointi 14 na kuendelea mpaka ufaulu wa E na S kwenye masomo mawili ya kidato cha sita.

Programu hii inafundishwa katika vituo vyote vya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Sita: Hapa tuliwaeleza kuhusu ufadhili wa masomo ya Foundation kwa wasichana wa masomo ya sayansi.
Shule hii ina wanafunzi wasichana wanaosoma masomo ya sayansi.

Hivyo tuliwaeleza kwamba serikali kupitia mradi wa mageuzi ya uchumi kupitia elimu ya juu (HEET) imetoa ufadhili wa asilimia mia moja kwa wasichana wenye sifa za kujiunga na foundation ambao wanatoka kwenye familia zenye uhitaji.

Ufadhili huo unahusu ada, kupatiwa vishikwambi, fedha za kujikimu wakati wa mafunzo ya ana kwa ana, viandikwa na visomeo pamoja na nauli.

Tuliwaomba taarifa hizi wasifikishe kwa wenzao waliopo katika shule mbalimbali na ambao walishamaliza shule wapo nyumbani.
Saba: Katika nukta hii tuliweza kuwaeleza kwamba chuo Kikuu Huria cha Tanzania ni mahali pazuri kwa mhitimu wa kidato cha sita ambaye anapenda kusoma shahada ya kwanza na huku anaanza kufanya shughuli zake kama biashara, kilimo, ujasiriamali na ufungaji.

Hii humuwezesha kuanza kujitegemea mapema ikilinganishwa na mwanafunzi ambaye amejiunga na vyuo vikuu vya bweni.

Tuliwaeleza kwa kina hili linaweza kufanyika namna gani na walivutiwa sana.

Nane: Tulitoa fursa ya maswali na majibu na mwisho kama kawaida yetu tuliwaacha kwa beti za mistari ya shairi lililoibuwa shangwe kubwa kutoka kwa wanafunzi hao takribani 200.
Kwa dhati kabisa tunatoa shukurani kwa uongozi wa shule kutupatia nafasi ya kutoa huduma hii pamoja na elimu kwa umma itakayosambaa nchi nzima. Tunasema asante sana na kazi iendelee.

Tunapenda pia kuwakaribisha watu wote wanaopenda kujiendeleza katika ngazi mbalimbali kwamba sasa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kinapokea maombi ya muhula wa masomo wa Aprili 2024 kupitia www.out.ac.tz. Tuma maombi yako sasa ukiwa popote pale.

WENU

Dkt. Mohamed Omary Maguo
Mhadhiri Mwandamizi
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania
Babati-Manyara
20/01/2024

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news