DAR ES SALAAM-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema, amechukua angalizo lilitolewa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Jacob John Mkunda la kufanya mchakato wa kuchambua wakimbizi na kuona jinsi ya kuwarudisha kwao, ambapo amesema anakwenda kulifanyia kazi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akiteta jambo na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi wa Tanzania Jenerali Jacob John Mkunda wakati wa mkutano wa CDF na Makamanda kwa mwaka 2023 ambao ulifanyika Lugalo Jijini Dar es Salaam tarehe 22 Januari, 2024.
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameyasema hayo Januari 22,2023 wakati wa Mkutano wa Saba wa CDF na Makamanda jijini Dar es Salaam.
“Mimi kama Mkuu wa Nchi nimechukua lile angalizo ulilotupa CDF, la kufanya mchakato wa kuchambua wakimbizi hasa kutoka Burundi na DRC na kwingineko na kuona jinsi ya kuwarudisha.
"Tumefanya kazi hii kwa kiasi kikubwa kwa kushirikiana na lile Shirika linaloshughulika na Wakimbizi Duniani, lakini ukweli ni kwamba lile shirika sasa limeishiwa nguvu kwa hiyo ule moto wa kurudisha wakimbizi kama walivyokuwa wakifanya umepungua.
“Kwa hiyo tutaendelea na mazungumzo ya kisiasa baina yetu na nchi jirani ili tuone njia bora za kurudisha wakimbizi wale na kama ulivyosema wengine sio wakimbizi wanaishi kama raia na wanajiona kama Watanzania.
"Kwa hiyo hili kama angalizo tumelichukua na tunakwenda kulifanyia kazi, wito wangu ni kujiimarisha kiteknolojia,”amesema Rais Dkt.Samia.
Awali,Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF),Jenerali Jacob John Mkunda alitoa maoni kwamba, kuendelea kuwepo kwa muda mrefu kwa wakimbizi nanwaomba hifadhi nchini Tanzania ni tishio la kiusalama.
Vile vile amebainisha kuwa, taarifa zilizopo ni kwamba wapo wakimbizi na waomba hifadhi ambao wameajiriwa serikalini na wengine wamepewa teuzi serikalini katika nafasi zenye maamuzi.
“Changamoto kubwa katika mikoa yetu ya Magharibi kwa sasa ni uwepo wa wakimbizi na waomba hifadhi wa muda mrefu.
"Tanzania imekuwa ikipokea maombi ya wakimbizi na waomba hifadhi kutoka Burundi tangu mwaka 1972, Rwanda tangu mwaka 1994 na DRC tangu mwaka 1996.
"Idadi ya wakimbizi 27,000 kutoka Burundi wa mwaka 1972 hawakuwekwa katika kambi za wakimbizi badala yake Serikali iliamua kuwagawanya katika vijiji 73 vilivyopo Mkoa wa Kigoma.
“Wakimbizi hawa na familia zao bado wanaendelea kuishi katika vijiji hivyo na kwa kutumia mbinu mbalimbali uhakikisha uzao wao unapata uraia wa Tanzania bila kufuata sheria.
"Serikali ya Tanzania na Burundi zimekuwa zikiwashawishi wakimbizi hao kurejea mchini mwao bila mafanikio.
“Mheshimiwa Rais kuanzia Januari 1,2023 hadi Desemba 31,2023 jumla ya waomba hifadhi 138,149 walipokelewa Tanzania ambao sehemu kubwa ni kutoka DRC, Rwanda na Burundi.
"Kutokana na mahojiano ya awali imebainika kuwa waomba hifadhi wengi wamekuja Tanzania kwa sababu za kiuchumi,kwani Tanzania imebainika kuwa na fursa nyingi za kiuchumi kuliko nchi walizotoka.
"Hata hivyo sababu hizo zinazowafanya wakimbie nchi zao zinawakosesha sifa sa kupewa hadhi ya ukimbizi.
“Ni maoni yetu kwamba kuendelea kuwepo kwa muda mrefu kwa waomba hifadhi na wakimbizi hawa nchini ni tishio la kiusalama.
"Kwani taarifa zilizopo ni kwamba baadhi ya waomba hifadhi hao au wakimbizi au familia zao wameajiriwa serikalini kwa nafasi mbalimbali na wengine wamepewa teuzi serikalini katika nafasi zenye maamuzi,"amesema CDF Mkunda.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Jacob John Mkunda licha ya changamoto hizo, hali ya ulinzi na usalama nchini ni shwari.
“Hali ya ulinzi na usalama ndani ya nchi kwa ujumla ni shwari, licha ya uwepo wa matishio ya kiusalama hasa tishio la kigaidi na itikadi kali.
"Wanamtandao wa kigaidi wamekuwa wakiwalaghai vijana wetu wenye umri wa kati ya miaka 15 na 35 kisha kuwasafirisha kwenda kujiunga na vikundi vya kigaidi hususani katika nchi za DRC, Msumbiji na Somalia hali inayoonesha upo ukuaji wa tatizo hilo hapa nchini.
"Dawa za kulevya, matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na ongezekeo la wahamiaji haramu ni miongoni mwa masuala yanayohatarisha hali ya usalama ndani ya nchi yetu, hata hivyo matishio hayo yanaendelea kudhibitiwa kwa ushirikiano na vyombo vingine vya usalama,"amesema CDF Mkunda.