GEITA-Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamsaka Yotham Komba kwa tuhuma za kutapeli kiasi cha shilingi milioni 110 kwa mfanyabiashara wa madini Soko Kuu la Dhahabu Geita.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amethibitisha na kueleza tukio hilo liliripotiwa Januari 16, 2024 mjini Geita.
Amesema, mtuhumiwa anajihusisha na biashara ya madini na alifika soko la dhahabu Geita ofisi za Kampuni ya madini ya Sab Gold Limited na kuchukua fedha hizo akiahidi kupeleka kilo moja ya dhahabu.
“Kwenye soko la dhahabu kuna tabia unampa mtu pesa halafu ndio anaenda kuleta mzigo, kwa hiyo huyo mtu kwa sababu anafanya kazi kwenye ofisi, alienda ofisi nyingine kuomba kiasi hicho cha pesa,” amesema Kamanda na kuongeza kuwa baada ya kupatiwa kiasi hicho, mtuhumiwa alitoweka.
“Soko la dhahabu wanafanya biashara kwa kuaminiana na ndiyo staili yao, siyo tu shilingi milioni 110, hata milioni 300 mpaka 500, lakini wengi kwa kuaminiana huko wanaishia kutapeliana,” amesema na kuonya wasifanye makubaliano bila maandishi wala dhamana.