NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza mabadiliko ya mfumo wa utekelezaji wa Sera ya Fedha nchini.
"Kama ilivyoainishwa katika Taarifa kwa umma ya tarehe 28 Juni 2023, Tamko la Sera ya Fedha la Benki Kuu ya Tanzania kwa mwaka 2023/24, na taarifa mbalimbali zilizotolewa kwa wadau,
"Benki Kuu ya Tanzania inautaarifu umma kwamba kuanzia mwezi Januari 2024 itaanza kutumia mfumo unaotumia riba katika kutekeleza Sera ya Fedha, badala ya mfumo unaotumia ujazi wa fedha."
Gavana Tutuba amefafanua kuwa,mabadiliko haya yanalenga kuongeza ufanisi wa sera ya fedha katika kudhibiti mfumuko wa bei na kuimarisha shughuli za kiuchumi.
Aidha, mabadiliko haya yanaendana na makubaliano ya kutumia mfumo mmoja wa utekelezaji wa sera ya fedha katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na jumuiya nyingine za kiuchumi ambazo Tanzania ni mwanachama.
"Kupitia mfumo huu, Benki Kuu ya Tanzania itakuwa inatoa mwelekeo wa riba itakayotumika katika soko la fedha baina ya mabenki.
"Riba hiyo itajulikana kama Riba ya Benki Kuu. Riba ya Benki Kuu, italenga kuwezesha ukwasi katika uchumi unaendana na malengo ya kudhibiti mfumuko wa bei na kuwezesha ukuaji wa Uchumi.
"Kwa muktadha huu, mabadiliko ya Riba ya Benki Kuu yatakuwa yanaashiria mwelekeo wa Sera ya Fedha katika kipindi husika.
"Riba hiyo pia itatumika kama kiashiria kimojawapo katika upangaji wa riba zinazotozwa na mabenki na taasisi nyingine za fedha nchini."
Aidha, wananchi wanaarifiwa kwamba mabadiliko ya utekelezaji wa Sera ya Fedha kwa kutumia mfumo wa riba haimaanishi kuweka ukomo katika viwango vya ribazinazotozwa na benki na taasisi nyingine za fedha nchini.
"Riba zinazotozwa na taasisi hizo zitaendelea kuamuliwa na nguvu ya soko, kuendana na sera nyingine za kiuchumi nchini,"amefafanua Gavana Tutuba.
Maelezo ya kina kuhusu mfumo huu mpya wa sera ya fedha yanapatikana kwenye tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania: www.bot.go.tz, au barua pepe:botcommunications@bot.go.tz.