MOROGORO-Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel Ndyamukama ameagizwa kuanza mara moja usanifu wa barabara ya Magole Estate-Mfuru pamoja na ujenzi wa mifereji ya maji katika mji wa Kilosa.
Agizo hilo limetolewa na Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff wakati wa ukaguzi wa miundombinu ya barabara na mifereji ya maji iliyoathirika na mvua zinazoendelea kunyesha wilayani hapa ambapo katika ukaguzi huo aliongozana na Mbunge wa Jimbo la Kilosa Mhe. Prof.Palamagamba Kabudi.
Katika Kata ya Kitete walijionea uharibifu wa Barabara ya Magole Estate-Mfuru yenye urefu wa Km. 4.5 na Kata ya Mbuni walijionea mfereji wa maji unaosababisha mafuriko ya maji maeneo ya mjini.
Hata hivyo, Mhandisi Seff aliwataka wananchi wa mji wa Kilosa kuunda vikundi vya kijamii kwa ajili ya kufanya kazi za kusafisha barabara na mifereji ili waweze kutunza miundombinu wanayojengewa na Serikali lakini pia kuwaongezea vipato na kuondokana na umaskini.
Naye, Diwani wa Kata ya Mbuni, Shabani Maringo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa ujenzi wa mifereji ya maji katika mji wa Kilosa ambayo imepunguza madhara ya mafuriko kwa kiasi kikubwa katika mtaa wa Viwandani,Madaraka, Mjini, Makaburini na Shule ya Msingi Kichangani.
