NA GODFREY NNKO
MKURUGENZI wa Utafiti na Sera za Uchumi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Suleiman Missango amesema,mwezi huu benki hiyo inatarajia kwa mara ya kwanza kuanza kutumia mfumo wa riba (Riba ya Benki Kuu) katika utekelezaji wa Sera ya Fedha.
Dkt.Missango ameyasema hayo leo kwenye semina ya siku moja kuhusu Mfumo Mpya wa Uandaaji wa Sera ya Fedha (Interest Rate-Based Monetary Policy Framework) na Ukusanyaji wa Sarafu.
Semina hiyo imeandaliwa na BoT kwa wahariri wa habari za biashara na uchumi huku ikifanyikia kwenye ukumbi wa benki hiyo jijini Dar es Salaam.
Dkt.Missango amesema, kuanzishwa kwa mfumo huo mpya kunafuta mfumo uliokuwepo wa ujazi wa fedha uliodumu tangu mwaka 1995 na umefikia kikomo mwaka jana.
"Lengo la Benki Kuu ni kudhibiti mfumuko wa bei ili kuwezesha ukuaji wa uchumi wa nchi, riba itakuwa ni kiashiria cha mwenendo wa uchumi wa nchi."
Dkt.Missango amesema,hatua hiyo inalenga kudhibiti mfumuko wa bei na kuwezesha ukuaji wa uchumi kwa kuzingatia mazingira ya kiuchumi ya ndani na nje.
"Kuhama kwenye mfumo wa ujazi kwenda kwenye riba ni sehemu ya uboreshaji wa Sera ya Fedha katika kufikia malengo ya Sera ya Fedha ambayo ni kudhibiti mfumuko wa bei na kusaidia ukuaji wa uchumi kulingana na mipango ya serikali.
“Mwezi huu wa Januari 2024, Benki Kuu itatangaza kwa mara ya kwanza kiwango cha riba chini ya utaratibu huu mpya,"amesema Dkt.Missango.
Vilevile amesema, sababu ya mabadiliko hayo ni kuboresha ufanisi wa utekelezaji wa Sera ya Fedha katika kusimamia malengo mapana ya kiuchumi ya kudumisha utulivu wa bei nchini.
Sambamba na kuongeza uwazi ikiwemo ukuaji wa uchumi hapa nchini.
Dkt.Missango amesema, utekelezaji wa Mfumo wa Riba ya Benki Kuu umeonesha matokeo mazuri katika usimamizi wa Sera ya Fedha.
Aidha,umeonesha kuimarisha misingi ya utekelezaji wake katika mazingira ya uwazi katika nchi mbalimbali duniani.
Dkt.Missango amesema, New Zealand, Uingereza, Afrika Kusini, Mauritius, Ghana na Uganda ni miongoni mwa mataifa ambayo yameona faida za mfumo huo duniani.
Pia, amesema mfumo huo mpya utazisaidia benki nchini kuimarika zaidi na kupanga riba.
Katika hatua nyingine, Dkt.Missango amesema,malengo ya Sera ya Fedha ni kuhakikisha kiwango cha fedha kilichopo kwenye uchumi kinakidhi mahitaji ya shughuli zinazoendana na uchumi nchini.
“Riba ya Benki Kuu itatumika kama kigezo cha kuweka viwango vya riba kwa wateja wa benki na taasisi nyingine za fedha nchini,”amesema.
Amesema kuwa, mabadiliko katika Riba ya Benki Kuu yataonesha mwelekeo wa Sera ya fedha ambapo ongezeko lake litamaanisha kupunguza ujazi wa fedha.
Dkt.Missango amesema, kupungua kwa riba hiyo kutamaanisha kuongeza ujazi wa fedha katika uchumi nchini.