Burundi yakipongeza Chuo cha BoT kwa kustawisha Sekta ya Fedha

BUJUMBURA-Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT Academy) kimepongezwa kwa mchango wake katika kustawisha sekta ya fedha katika Ukanda wa Afrika Mashariki kupitia mafunzo ya muda mfupi na yale ya muda mrefu yanayotolewa na chuo hicho.
Pongezi hizo zimetolewa na Gavana wa Benki Kuu ya Burundi (BRB), Bw. Eduoard Bigendako, alipotembelewa na ujumbe kutoka Chuo cha Benki Kuu unaozuru nchini Burundi kuanzia tarehe 22 hadi 26 Januari 2024, kwa lengo la kuboresha mahusiano na benki hiyo na sekta ya fedha kwa ujumla pamoja na kutangaza mafunzo yanayotolewa na chuo hicho.
Gavana wa Benki Kuu ya Burundi (BRB), Bw. Eduoard Bigendako, akizungumza alipoukaribisha ofisini kwake ujumbe kutoka Chuo cha Benki Kuu.

Gavana Bigendako alisisitiza kuwa, mafunzo yanayotolewa na Chuo cha BoT yamekuwa nyenzo muhimu ya kuwajengea uwezo watu mbalimbali wenye dhamana ya kuendeleza sekta ya fedha.
Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Benki Kuu, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utumishi na Uendeshaji wa BoT, Bw. Kened Nyoni akizungumza katika mkutano na Gavana wa BRB, Bw. Eduoard Bigendako.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Benki Kuu, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utumishi na Uendeshaji wa BoT, Bw. Kened Nyoni, alimueleza Gavana Bigendako kuwa, BoT imeanza rasmi kutumia mfumo wa sera ya fedha unaotumia riba katika utekelezaji wa sera ya fedha nchini.

Aidha, aliongeza kuwa Tanzania kupitia usimamizi wa BoT imepiga hatua katika nyanja mbalimbali ikiwemo katika mifumo ya malipo na hivyo mafunzo yanayotolewa na Chuo cha Benki Kuu yatasaidia kuijengea uwezo BRB pamoja na mengine kutatua changamoto mbalimbali katika uendeshaji wa mifumo ya malipo nchini humo.

Naye Mkuu wa Chuo cha Benki Kuu, Dkt. Nicas Yabu, amesema chuo hicho kimekuwa kikipokea washiriki kutoka nchi mbalimbali barani Afrika ikiwemo Uganda, Kenya, Zimbabwe, Ghana, Zambia, Malawi na Sudani ya Kusini.

Dkt. Yabu aliongeza kuwa, ushiriki wa mataifa hayo kwenye mafunzo yanayotolewa na Chuo cha Benki Kuu umetengeneza mazingira mazuri ya kubadilishana uzoefu na kupata suluhu ya changamoto zinazokumba uchumi wa nchi hizo.
Gavana wa Benki Kuu ya Burundi, Bw. Eduoard Bigendako (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Chuo cha Benki Kuu. Kutoka Kushoto ni Mkuu wa Chuo cha Benki Kuu, Dkt. Nicas Yabu, Mratibu Mwandamizi na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Chuo cha Benki Kuu,Bi. Asumpta Muna, Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Benki Kuu, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utumishi na Uendeshaji wa BoT, Bw. Kened Nyoni, Naibu Gavana wa Kwanza wa Benki Kuu ya Burundi, Bi. Irene Kabura na Naibu Gavana wa Pili wa Benki Kuu ya Burundi,Bi. Marie- Goreth Ndayishimiye.

Pamoja na kukutana na uongozi wa Benki Kuu ya Burundi, ujumbe wa BoT unatarajia kukutana na mabenki ya biashara nchini humo kwa ajili ya kutangaza mafunzo yanayotolewa na chuo hicho.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news