Chuo Kikuu Huria cha Tanzania hakiachi yeyote nyuma, Manyara wafikiwa

MANYARA-Kitengo cha Mawasiliano na Masoko cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwa kushirikiana na kituo cha chuo hicho mkoa wa Manyara tumetembelea Shule ya Sekondari ya Babati Day iliyopo mjini Babati leo tarehe 19/01/2024.

Lengo la ziara hiyo ni kutoa elimu kwa umma na huduma kwa jamii kupitia wanafunzi wa kidato cha Tano na Sita pamoja na watumishi wa shule hiyo.

Tukiwa tumefuatana mimi Dkt. Mohamed Omary Maguo na Mwl. Ahmed Mussa ambaye ni Mkurugenzi wa kituo cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania mkoa wa Manyara tumefanya yafuatayo:
Mosi: Tumewaeleza wanafunzi wa kidato cha Tano na Sita ambao wote ni wasichana kuhusu umuhimu wa wao kujituma na kuongeza juhudi katika masomo yao. 

Tumewapatia hamasa ya kufanya vizuri katika masomo na kwamba jamii inawategemea katika kuleta maendeleo siku chache zijazo.

Pili: Tumewaeleza kuhusu Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwamba ni Chuo Kikuu cha serikali ambacho kimeanzishwa kwa sheria ya Bunge namba 17 ya mwaka 1992 kwa malengo ya kutoa elimu ya juu kuanzia ngazi ya cheti, Diploma, Shahada, Shahada za uzamili na uzamivu kwa njia za Huria, Masafa na Mtandao. Chuo hiki kipo kila mahali Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar katika kila mkoa.

Tatu: Tumewaeleza kwamba Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kinatoa elimu kwa kutumia mifumo ya kisasa kama mihadhara Mubashara kwa njia za ZOOM, majadiliano ya vikundi kwa njia za What's App Vimbwetta, ZOOM Vimbwetta, Maktaba mtandao, Mfumo wa ujifunzaji Kielekroniki (MOODLE) pamoja na mifumo ya Ana kwa ana ikihusisha mafunzo kwa vitendo.

Mwanafunzi anapodahiliwa hupata maelekezo jinsi ya kutumia mifumo hii na husoma akiwa popote anaendelea na shughuli zake.
Nne: Tumewaeleza kuhusu _Foundation_ _Program_ kwa wahitimu wa kidato cha Sita watakaopata ufaulu wa kuanzia Daraja la Tatu nukta 14 na kuendelea mpaka ufaulu wa E na S kwenye masomo mawili. 

Wenye ufaulu huo watasoma _foundation_ na wakimaliza watapata sifa ya kujiunga na masomo ya shahada ya kwanza kwenye vyuo mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi. _Foundation_ _Program_ husomwa kwa mwaka mmoja tu wa masomo kwenye vituo vyote vya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Tano: Tumewaeleza kuhusu ufadhili wa masomo kwa asilimia mia moja kwa wasichana wa masomo ya sayansi ambao wana sifa za kujiunga na _foundation_. 

Ufadhili huo unahusu ada ya masomo, kila mwanafunzi kupewa kishikwambi, gharama za malazi na chakula wakati wa mafunzo ya ana kwa ana, vitabu na _stationary_ kutaja kwa uchache.
Hata hivyo shule hii ya Babati Day ni ya wasichana kwa kidato cha Tano na Sita wa mkondo wa Sanaa lakini taarifa kuhusu ufadhili huo ambao ni kwa wale wa sayansi umewavutia sana na wameahidi kuusambaza kwa wenzao wa shule mbalimbali wanaosoma mkondo wa Sayansi.

Sita: Tulitoa nafasi ya maswali na majibu ili kuhakikisha ujumbe wetu na huduma tuliyoilenga imewafikia walengwa. 

Baada ya kipengele hiki tuliwaaga kwa beti za shairi tamu ambalo liliwaburudisha na kuwafurahisha sana lenye maudhui ya kuwahimiza kujitahidi katika masomo yao.
Saba: Tunatoa shukurani za dhati kwa uongozi wa shule ya sekondari ya Babati Day kwa kutupatia nafasi ya kutoa huduma na kupitia shule hii tunatoa elimu kwa umma wa Watanzania wote na wanafunzi wote wa kidato cha Tano na Sita popote pale walipo kwani makala haya tumeyasambaza kupitia vyombo mbalimbali.
Tunawakaribisha watu wote wanaotaka kujiunga na masomo kwenye ngazi zote kuanzia cheti, diploma, shahada na shahada za Uzamili na Uzamivu katika muhula wa Aprili 2024 watume maombi yao kupitia www.out.ac.tz sasa hivi dirisha la udahili lipo wazi.

WENU

Dkt. Mohamed Omary Maguo
Mhadhiri Mwandamizi
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania
Babati-Manyara
19/01/2024.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news