MWANZA-Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff ameagiza Daraja la Mwananchi lililopo Kata ya Mahina jijini Mwanza kuanza kukarabatiwa mara moja kufuatia kuharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha jijini hapa.
Mhandisi Seff ameyasema hayo jijini Mwanza alipofanya ukaguzi wa miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika Mkoa wa Mwanza.
“Daraja hili la Mwananchi ni kiungo muhimu kwa wafanya biashara na wakazi wa jiji la Mwanza katika kutekeleza shughuli zao mbalimbali za kijamii na kiuchumi , hivyo nakuagiza Meneja uanze ukarabati wa daraja hili mara moja,”ameagiza Mhandisi Seff.
Wakati huo huo Mhandisi Seff ameelekeza kilomita 4.5 za barabara ya Igongwe-Isanzu-Kabusungu wilaya ya Ilemela ziweke kwenye kipaumbele cha bajeti kwa ajili ya kujengwa kwa kiwango cha lami.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 5.8 inayoelekea hospitali mpya ya Wilaya ya Ilemela ambapo kilomita 1.3 zipo kwenye ujenzi wa kiwango cha lami.
“Ujenzi wa barabara hii utawarahisishia wananchi wa Ilemela kupata huduma za afya kwa wakati na kupunguza madhara na vifo vilivyokuwa vinatokana na kuchelewa kufika kupata huduma katika vituo vya afya kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara.”
Akiwa katika Halmashauri ya Sengerama, Mhandisi Seff alitembelea na kujionea ubovu wa barabara uliotokana na mvua katika barabara ya Tabaruka-Nyibanga-Kishinda kilomita 11 na Ibondo-Kasongamile-Chamabado kilomita 35 na kumuelekeza Meneja wa TARURA Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Makori Kisare kufanya tathimini ya uharibifu huo.
“Fanyeni tathimini ya uharibifu wa barabara hizi na muweze kurudisha mawasiliano kwa kufanya matengenezo ya maeneo korofi na kujenga Makalavati ili barabara hizi ziweze kupitika katika misimu yote ya mwaka,"amesisitiza Mhandisi Seff.
Vile vile, Mtendaji Mkuu huyo amewataka Mameneja wa Mikoa wote wa TARURA nchi nzima kufanya ukaguzi wa madaraja na mifereji kabla ya Majira ya mvua kuanza ili kupunguza au kuondoa kabisa madhara na uharibifu wa miundombinu ya barabara pindi mvua zitakaponyesha.