Elimu ni ufunguo, Rais Mwinyi kaanza

NA LWAGA MWAMBANDE

JANUARI 7,2024 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali imeweka kipaumbele namba moja katika sekta ya elimu imeongeza bajeti kutoka shilingi bilioni 265 mwaka 2021 hadi shilingi bilioni 457.
Amesema,lengo ni kuongeza juhudi katika sekta hiyo kwa ujenzi wa miundombinu ya kisasa ikiwemo skuli za msingi na sekondari za ghorofa zinazojumuisha maabara za kisasa, maktaba na vyumba vya kompyuta.

Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo alipofungua Skuli ya kisasa ya Msingi Fuoni Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Skuli hiyo ya mfano ya kisasa imejengwa kwa miezi mitano na Kampuni ya ROK Development B.V ya Uturuki na kusimamiwa na Wakala wa Majengo ya Serikali (ZBA) ambayo ni aina ya ghorofa mbili kwa ujenzi wa teknolojia ya PRE FABRICATION kwa fedha za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar shilingi bilioni 7.8.

Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa, Serikali itaendelea kuajiri walimu wa fani zote hususani wa masomo ya sayansi na hesabu ili waweze kutoa elimu bora na kwa mwaka huu itaajiri walimu 1,500. 
Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande licha ya kusisitiza kuwa elimu ni ufunguo, pia amempongeza Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi kwa jitihada kubwa anazofanya katika Sekta ya Elimu. Endelea;

1.Kipaumbele cha kwanza, huko Zenj ni elimu,
Rais Mwinyi kaanza, anafanya kwa awamu,
Watu waweze jifunza, masuala ya muhimu,
Elimu ni ufunguo, wa mambo mengine mengi.

2.Serikali yaongeza, matumizi ya elimu,
Miundombinu eneza, ile yote ya muhimu,
Ukisasa kukomaza, kwa masomo na nidhamu,
Elimu ni ufunguo, wa mambo mengine mengi.

3.Kwanza zinajengwa shule, za kufundisha walimu,
Za msingi hizo shule, na sekondari muhimu,
Tena kwa kuona mbele, za ghorofa ni adhimu,
Elimu ni ufunguo, wa mambo mengine mengi.

4.Rais kasisitiza, maabara za kudumu,
Maktaba kuwekeza, kompyuta ziwe rijamu,
Ili watoto kuweza, kusoma vema kwa zamu,
Elimu ni ufunguo, wa mambo mengine mengi.

5.Kasema hapo Fuoni, kwenye kazi ya elimu,
Skuli mpya ya Fuoni, majengo yamehitimu,
Kwa watoto udhamini, waweze pata elimu,
Elimu ni ufunguo, wa mambo mengine mengi.

6.Pamoja miundombinu, safi yote ya elimu,
Hii mpya nayo mbinu, iandike kwa kalamu,
Watoto wetu na wenu, watapatiwa walimu,
Elimu ni ufunguo, wa mambo mengine mengi.

7.Elfu moja mia tano, ajira zao walimu,
Hiyo taarifa nono, kote waliko walimu,
Wajishikao kiuno, bila kupangiwa zamu,
Elimu ni ufunguo, wa mambo mengine mengi.

8.Zanzibar yatambulika, Uchumi Buluu wadumu,
Itazidi changamka, ikiinuka elimu,
Kwa kweli itafunika, iweze tesa kwa zamu,
Elimu ni ufunguo, wa mambo mengine mengi.

9.Hussein Mwinyi Dokta, kwa kweli umehitimu,
Kazi njema twazichota, mambo ya kibinadamu,
Maendeleo twapata, twapanda zamu kwa zamu,
Elimu ni ufunguo, wa mambo mengine mengi.

10.Tuungane kwa kusema, Mapinduzi na yadumu,
Tuzidi kupata mema, miaka tukihitimu,
Na wala tusijekwama, wapo bora wahudumu,
Elimu ni ufunguo, wa mambo mengine mengi.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news