Furahika Education College kuwafundisha vijana wasiojua kusoma na kuandika bure

DAR ES SALAAM-Chuo cha Ufundi Stadi cha Furahika cha Buguruni Malapa katika Halashauri ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam kimeazisha programu maalumu ya kuwafundisha vijana wasiojua kusoma na kuandika bure.
Hayo yamebainishwa chuoni hapo na Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Dkt.David Msuya wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amefafanua kuwa, kwa kozi hiyo wanapokea vijana kuanzia miaka 14 hadi 30.

“Kozi hiyo itaanza Februari, mwaka huu kwa muda wa mchana na itatolewa bure watakacholipia ni fomu ya usajili tu, hivyo tunawakaribisha wasichana kwa wavulana wasiojua kusoma na kuandika wajitokeza kwa wingi kujisajili ili tuanze masomo kulingana na ratiba.

“Hapa watafundishwa kuanzia hatua ya darasa la kwanza hadi la tano na tunaamini kwa muda huo watakuwa wanajua kusoma na kuandika vizuri na kuweza kuperuzi katika mitandao ya kijamii kupitia simu yake na kufahamu ulimwengu namna unavyokwenda bila tatizo,”amesema Dkt.Msuya.

Ameongeza kuwa, wameamua kuanzisha kozi hiyo baada ya kubaini kuwepo kwa kundi la vijana wasiojua kusoma na kuandika, hivyo wakifundishwa watakuwa wamewaondoa katika giza zito katika maisha yao ya kila siku.

Dkt.Msuya amefafanua kuwa, vijana walio katika kundi hilo wasione aibu kujiunga na Chuo cha Furahika kwa ajili ya kujifunza kusoma na kuandika kutokana na kwamba wapo wamefika hapo kutokana na kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo kufiwa na wazazi na kutopata mtu wa kumpeleka shule kwa wakati sahihi.

Pia kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii wanajipanga kutoa elimu ya malezi kwa walimu wa shule ya awali na jamii kwa muda wa miezi sita na mwaka mmoja ili waweze kutoa huduma bora kwa watoto wanaojiunga kwenye shule zao.

Dkt. Msuya amefafanua kuwa, elimu hiyo ambayo wanaitoa bure itakuwa ni moja ya fursa kwa watakaohitimu, kupata ajira kwenye shule mbalimbali nchini za awali.

Vile vile amesema, mkakati wao mwingine ni kufundisha wafanyakazi wa kazi za majumbani ili kuwapa uelewa mkubwa kuhusu namna ya kuhudumia familia na nyumba kwa ujumla.

“Wapo baadhi ya wafanyakazi wa ndani wanafanya kazi kwa mazoea huku wakiwa hawana ujuzi kitu ambacho wakati mwingine wanajikuta wakifanya ukatili kwa watoto pasipo kujua na kuingia kwenye matatizo, hivyo wakija kwetu tatizo la ukatili litaondoka ama kupungua kwa asilimia kubwa,” amesema.

Katika hatua nyingine, Dkt.Msuya ametoa ushauri kwa akina dada wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi ikiwemo nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu na Oman kabla ya kwenda huko wajiunge na Chuo cha Furahika ili kupata elimu na mafunzo sahihi juu ya namna ya kuhudumia nyumba na familia kwa ujumla ili kuondoa changamoto mbalimbali katika majukumu yao wanapokuwa huko nje.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news