Gavana Tutuba azindua rasmi Mfumo wa Sera ya Fedha unaotumia Riba ya Benki Kuu

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imezindua rasmi Mfumo wa Sera ya Fedha unaotumia Riba ya Benki Kuu.

Uzinduzi huo umefanyika leo Januari 19,2024 katika Ukumbi wa BoT jijini Dar es Salaam.

Katika uzinduzi huo ambao umewakutanisha pamoja Wajumbe wa Kamati ya Sera ya Fedha ya Bodi ya Benki Kuu,Wakuu wa Benki na Taasisi za Fedha,
Viongozi na wafanyakazi wa Benki Kuu,Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba amebainisha kuwa,hiyo ni hatua muhimu kwa Benki Kuu.

"Kama mnavyofahamu, tumekutana hapa leo kwa ajili ya kuzindua safari yetu mpya ya uandaaji na utekelezaji wa sera fedha nchini.

"Hii ni hatua muhimu kwa Benki Kuu ya Tanzania tunapoanza rasmi kutumia mfumo mpya wa sera ya fedha, unaojulikana kama Mfumo wa Sera ya Fedha Unaotumia Riba (the interest rate or price-based monetary policy framework).

"Hii inamaanisha kuwa tumehama rasmi kutoka mfumo wa sera ya fedha unaotumia ujazi wa fedha (Monetary Targeting Framework) na kwenda katika mfumo unaotumia Riba."

Gavana Tutuba amesema,hiyo ni sehemu ya maboresho katika sekta ya fedha, yenye lengo la kuongeza ufanisi wa sera ya fedha.

Pia,tukio hili limeenda sambamba na kutangaza Riba ya Benki Kuu (Central Bank Rate (CBR) or policy rate) kwa mara ya kwanza ambayo itakuwa asilimia 5.5 kwa robo mwaka ya kwanza 2024. Riba hiyo itakuwa baina ya Benki Kuu na mabenki nchini.

"Kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Benki Kuu, jukumu letu la msingi ni kuandaa na kutekeleza sera ya fedha yenye lengo la kudhibiti mfumuko wa bei na kuwezesha ukuaji endelevu wa uchumi.

"Kwa takribani miaka 28 sasa, jukumu hilli limekuwa likitekelezwa kwa kutumia mfumo wa ujazi wa fedha.

"Tulichagua kutumia mfumo huo kutokana na mazingira ya kiuchumi ya wakati huo. Mfumo huo ni rahisi kutumika kwa nchi zenye kiwango cha chini cha maendeleo ya masoko ya fedha na zenye changamoto ya upatikanaji wa takwimu za kutosha kwa ajili ya uchambuzi.

"Hata hivyo, ni vyema ikafahamika kuwa katika kipindi hiki Benki Kuu imeweza kufikia malengo yake ya kudhibiti mfumuko bei na kuchangia ukuaji wa uchumi, licha ya changamoto mbalimbali katika uchumi hususan zinazotoka nje ya nchi,"amefafanua Gavana Tutuba.

Vile vile, amesema licha ya mafanikio waliyoyapata chini ya mfumo unaotumia ujazi wa fedha, wamekumbana na changamoto kadhaa zilizopelekea mabadiliko haya.

"Moja ya changamoto kubwa tuliyokumbana nayo ilitokana na maendeleo katika sekta ya fedha, hususani kuongezeka kwa ubunifu na matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za kifedha.

"Hali hii imesababisha ugumu katika kukadiria kiwango cha ujazi wa fedha kinachoendana na mahitaji ya shughuli za kiuchumi nchini.

"Kutokana na hali hii, Benki Kuu ililazimika kutafuta mfumo mbadala wa sera ya fedha unaofaa katika wakati na mazingira ya sasa,"amesema Gavana Tutuba.

Katika kutafuta mfumo mbadala wa sera ya fedha,Gavana Tutuba amesema,waliamua kuchagua mfumo unaotumia riba.

Aidha,katika kutekeleza mfumo huu, Benki Kuu hutumia viwango vya riba vya muda mfupi kudhibiti ujazi wa fedha.

"Ni vyema ifahamike kuwa mfumo huu si mpya duniani kwani umekuwa ukitumiwa na benki kuu nyingine katika kutoa mwelekeo wa sera ya fedha.

"Mathalani, barani Afrika, mfumo huu unatumiwa na nchi mbalimbali ikiwemo Rwanda, Kenya, Zambia, Uganda, Ghana, na Afrika Kusini. Nje ya Afrika, mfumo huu unatumiwa na New Zealand, Canada, Japani, Uingereza, na nchi nyingine nyingi.

"Pamoja na kutumia mfumo huu ili kukabiliana na changamoto nilizoainisha hapo awali, mabadiliko haya yanafanyika ili kutekeleza itifaki ya kuanzisha Umoja wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, katika kuelekea kuwa na sarafu moja na Benki Kuu moja ya Afrika Mashariki."

Vilevile, Gavana Tutuba amesema,mabadiliko haya yanafanyika kwa mujibu makubaliano ya jumuiya nyingine za kikanda ambazo Tanzania ni mwanachama.

Amesema,mfumo huu wa utekelezaji wa Sera ya Fedha kwa kutumia riba hutegemea sana uwazi ili kufikia malengo yake ya kukabiliana na mfumuko wa bei na kuchangia ukuaji wa uchumi.

Wakati huo huo, Gavana Tutuba ametangaza rasmi Riba ya Benki Kuu ambayo ni asilimia 5.5.

"Ni matumaini yangu kuwa riba hii itatoa mwelekeo kwa taasisi za fedha katika utekelezaji wa shughuli zao, ikiwemo ukokotoaji wa riba za huduma zao.

"Hivyo kuongeza ufanisi wa sera ya fedha katika kudhibiti mfumuko wa bei na kuimarisha shughuli za kiuchumi.

"Ni vyema pia ikafahamika kuwa utekelezaji wa sera ya fedha kwa kutumia mfumo wa riba ya Benki Kuu haimaanishi kuweka ukomo kwa viwango vya riba zinazotozwa na benki na taasisi nyingine za fedha."

Amesema, riba zinazotozwa na taasisi hizi zitaendelea kuamuliwa na nguvu ya soko.

"Naomba kuwataarifu kuwa kuanzia sasa mikutano ya Kamati ya Sera ya Fedha itakuwa inafanyika kila baada ya robo mwaka (miezi mitatu).

"Aidha, baada ya mikutano hiyo tutakuwa tunakutana na vyombo vya habari ili kutangaza riba ya Benki Kuu.

"Pamoja na hayo, Benki Kuu pia itatoa Taarifa ya Kamati ya Sera ya Fedha na Kalenda ya mikutano ya Kamati ya Sera ya Fedha ili kuwasaidia kupangilia shughuli zenu kuendana na matukio haya,"amefafanua Gavana Tutuba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news