Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi akitoa hotuba ya kuaga mwaka 2023 na kuukaribisha mwaka mpya 2023 Ikulu jijini Zanzibar.
Ndugu Wananchi; Assalamu Aleikum Warahamatullah Wabarakatuh,
Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na afya njema na kutuwezesha kuifikia siku ya leo ya kuuaga mwaka 2023 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2024.
Ndugu Wananchi; Ni utaratibu tuliojiwekea katika nchi yetu inapofika siku kama hii kutoa risala ya kuuaga mwaka unaomalizika na kuukaribisha mwaka mpya kwa kueleza muhtasari na tathmini ya utendaji wetu, sambamba na mwelekeo wa nchi yetu kwa mwaka ujao.
Kwa hakika, tuna wajibu wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuukamilisha mwaka wa 2023 kwa amani na mafanikio.
Katika mwaka tunaoumaliza, tumefanikiwa katika kudumisha amani,umoja na mshikamano wa kitaifa hapa nchini.
Viongozi wa Serikali, viongozi wa kisiasa, asasi za kiraia tumeweza kushirikiana na wananchi katika masuala mbali mbali ya maendeleo, hatua ambayo imetuwezesha kutekeleza kwa mafanikio mipango yetu ya kukuza uchumi na kuimairisha huduma za jamii.
Aidha, hali hiyo imewavutia na kupelekea kuungwa mkono na washirika wetu wa maendeleo yakiwemo mashirika ya Kimataifa, Taasisi, mbali mbali, Balozi za nje na nchi marafiki.
Ndugu Wananchi; Katika mwaka tunaoukamilisha tumepata mafanikio katika kuimarisha ukuaji wa uchumi, uimarishaji wa miundombinu, biashara na uwekezaji, huduma za jamii zikiwemo elimu, afya, maji safi na salama, umeme na uimarishaji wa demokrasia na utawala bora.
Kwa jumla sekta zote zimeweza kupiga hatua kubwa za mafanikio kwa kuzingatia mipango yetu mikuu ya maendeleo; Ilani ya uchaguzi ya CCM 2020/2025, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar na Malengo mengine ya Kikanda na Kimataifa kama ambavyo imeelezwa kwa kina kupitia majukwaa mbali mbali na vyombo vya habari mwezi uliopita wakati nchi yetu inaadhimisha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Nane.
Napenda kutumia fursa hii kwa mara nyingine kutoa shukrani zangu za dhati kwa wananchi wote, Viongozi wa ngazi mbali mbali na watumishi wote wa Serikali, Viongozi wa Dini na Asasi za Kiraia, sekta binafsi na Washirika wetu wa Maendeleo wa ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushikiriano waliotupa na kuiwezesha Serikali kutekeleza mipango yake ya maendeleo kwa mafanikio.
Natoa shukrani maalum kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Viongozi na Watendaji wote wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano waliotupa katika kufanikisha shughuli za Serikali.
Naomba tuendeleze ushirikiano huo kwa mwaka mpya tunaoukaribisha na miaka ijayo ili nchi yetu izidi kupiga hatua za maendeleo katika kukuza uchumi na kuimarisha huduma na ustawi wa wananchi wetu.
Ndugu Wananchi; Katika mwaka unaomalizika, tumeshuhudia mafanikio makubwa katika utekelezaji wa miradi yetu mikubwa ya maendeleo ikiwemo uimarishaji wa miundombinu ya elimu kwa ujenzi wa Skuli mpya 62 za ngazi mbalimbali na kuzipatia vifaa.
Kukamilika na kuanza kutumika kwa hospitali mpya 10 za Wilaya zenye vifaa vya kisasa na hospitali moja ya mkoa ya Lumumba katika Mkoa wa Mjini Magharibi,
Ujenzi wa vituo vya wajasiriamali kila Wilaya na kuwapatia mikopo nafuu, kuwawezesha wavuvi wadogo na wakulima wa mwani kwa kuwapatia mikopo na vifaa na kuanza ujenzi wa barabara kuu km 103.5,
Barabara za ndani mjini na vijijini km 275 pamoja na ujenzi wa barabara za mjini km 100 na madaraja ya juu mawili (flyover) katika Manispaa ya Mji wa Zanzibar.
Mradi wa ujenzi wa bandari jumuishi ya Mangapwani nao umeshaanza kwa hatua mbali mbali zikiwemo za ujenzi wa miundombinu ya barabara, utengaji wa maeneo kwa shughuli mbali mbali na kuanza ujenzi wa nyumba za wananchi waliopisha utekelezaji wa mradi huo.
Pamoja na hayo, tumekamilisha ujenzi wa jengo la Terminal 3 katika Uwanja wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume na kuanza kutumika ambapo kumeimarisha huduma zinazotolewa kwa kuongeza idadi ya mashirika makubwa ya ndege yanayofanya safari zake nchini kufikia 10 kutoka matano pamoja na kuongeza mapato yanayokusanywa kutoka bilioni 6.11 mwaka 2019/2020 hadi bilioni 29.3 mwaka 2022/2023.
Hatua za ujenzi wa uwanja wa ndege Pemba zimeshaanza. Aidha, tunakamilisha ujenzi wa masoko makubwa ya kisasa yanayoweza kuhudumia watu wengi zaidi katika maeneo ya Mwanakwerekwe, Jumbi na Chuini ujenzi ambao unatarajiwa kukamilika mapema mwakani.
Pia, kazi ya kulifanyia matengenezo makubwa soko la mboga Mombasa nayo imeshaanza. Vile vile, Serikali iko katika hatua za mwisho ya kukamilisha ujenzi wa miradi mikubwa ya maji safi na salama kote Unguja na Pemba ili kuondoa kabisa changamoto ya upatikanaji wa hudumu hii.
Miradi hiyo ni ya Uimarishaji wa Mfumo wa Usambazaji Maji wa Exim Bank ya India ambao umehusisha ujenzi wa matangi 25 yenye uwezo wa kuhifadhi lita 134,000.000 za maji na Mradi wa Uimarishaji Maji Zanzibar wa Ahueni ya Uviko 19 uliojumuisha ujenzi wa matangi 10 ya kuhifadhia maji yenye uwezo wa kuhifadhi lita 10,000.000. Miradi hii miwili italeta unafuu mkubwa katika kukabiliana na changamoto ya uhaba wa huduma ya maji nchini.
Ndugu Wananchi; Kwa madhumuni ya kuimarisha hduma ya usafiri wa jamii katika mwaka unaomalizika tumeanza kazi ya ujenzi wa maegesho Kijangwani na Malindi.
Aidha, ili kuimarisha makazi bora kwa wananchi tumeanza ujenzi wa nyumba za kisasa Kwa Mchina na Tomondo katika Mkoa wa Mjini Magharibi.
Vile vile, tumeshuhudia mafanikio makubwa katika uimarishaji wa sekta ya michezo nchini kwa kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya mchezo ikiwemo ujenzi mkubwa uliofanyika wa uwanja wa Amani na kuufanya uwe na hadhi ya Kimataifa kazi ambayo tutaifanya pia kwa uwanja wa Gombani kule Pemba.
Maelezo ya kina ya mafanikio tuliyoyapata kwa sekta mbali mbali kwa mwaka huu unaomalizika na katika kipindi chote tokea kufanyika kwa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964, yameendelea kutolewa na Waheshimiwa Mawaziri wa kila sekta kupitia vipindi maalum vya redio, televisheni na mitandao ya kijamii.
Tuendelee kufuatilia vipindi hivyo. Ahadi yangu ni kuwa, Serikali itayaendeleza mafanikio hayo katika mwaka ujao kwa kuikamilisha miradi yote iliyoanza na kuanzisha miradi mipya ya maendeleo.
Ndugu Wananchi, Pamoja na mafanikio tuliyoyapata katika mwaka tunaoumaliza, natoa wito kwa mwaka mpya tunaoukaribisha wa 2024, kuongeza mshikamano wetu katika kudumisha amani na umoja katika nchi yetu.
Bila ya amani na umoja 6 hakuna mafanikio yatakayopatikana. Vile vile, tufanye kazi kwa bidii na kuongeza jitihada zetu katika mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji, matumizi ya dawa za kulevya, uharibifu wa mazingira, rushwa na uhujumu wa uchumi.
Kwa hakika mapambano haya yanahitaji mchango wa kila mmoja wetu kwa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya sheria. Ndugu Wananchi, Tarehe 12 Januari 2024, Zanzibar inatimiza miaka 60 ya Mapinduzi.
Kipindi cha miaka 60 ni kikubwa ambapo nchi yetu pia imeweza kupata mafanikio makubwa ya maendeleo katika kipindi hicho. Serikali imeamua kuyafanya maadhimisho haya ya miaka 60 yenye kauli mbiu isemayo: “Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar: Tuimarishe Uchumi, Uzalendo, Amani na Maendeleo ya Taifa letu”.
Katika kufanikisha maadhimisho haya, shughuli mbali mbali zimeandaliwa ikiwemo ufunguzi wa miradi ya maendeleo na uwekaji wa mawe ya msingi, usafi wa mazingira, makongamano, maonesho, matamasha ya burudani na michezo, fashfash na sherehe maalum za siku ya kilele katika Uwanja wa Amani ambao kama mnavyojua umejengwa upya na kuwa wa kisasa.
Katika Maadhimisho haya ya miaka 60 ya Mapinduzi, tunatarajia pia kupata wageni mashuhuri wakiwemo baadhi ya Viongozi wa nchi jirani.
Wito wangu kwenu wananchi wenzangu kila mmoja wetu ajitahidi kushiriki katika maadhimisho haya ambayo yanatanguliwa na shamra shamra mbali mbali kote Unguja na Pemba.
Ushiriki wetu ni muhimu katika kusherehekea Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na kuthamini jitihada za waasisi wa 7 Mapinduzi kujitoa muhanga ili kuikomboa nchi yetu kwa lengo la kujitawala na kujiletea maendeleo.
Ndugu Wananchi, Namalizia risala yangu kwa kutoa salamu za mwaka mpya kwa wananchi wote wa Zanzibar, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndugu, jamaa na marafiki wote popote walipo.
Pia, natoa salamu kwa viongozi wa Serikali wa nchi rafiki, Taasisi za Kimataifa na Washirika wetu mbali mbali wa maendeleo. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aujaalie kheri na baraka nyingi mwaka mpya wa 2024.
Aizidishie Amani, Umoja na Mshikamano nchi yetu. Mola wetu atupe uwezo wa kuitekeleza kwa mafanikio zaidi mipango yetu ya maendeleo ili tukuze uchumi na ustawi wa nchi yetu.
KHERI YA MWAKA WA 2024
Asanteni kwa kunisikiliza.